Warithi wa Cannavaro Yanga

Muktasari:

  • Msemo huu ndio unamnyemelea beki mkongwe wa Yanga, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ ambaye amedumu katika timu hiyo kwa miaka 12 sasa.

WAHENGA walisema hakuna marefu yasiyokuwa na ncha. Walikuwa na maana ya kwamba hakuna jambo lenye mwanzo likakosa mwisho. Ni kama ilivyo mwisho wa maisha tunayoishi ni kifo.

Msemo huu ndio unamnyemelea beki mkongwe wa Yanga, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ ambaye amedumu katika timu hiyo kwa miaka 12 sasa.

Cannavaro ambaye alikuwa akicheza kwa maelewano makubwa na beki mwenzake, Kelvin Yondani ndani ya Yanga na Taifa Stars, kwa sasa ana umri wa miaka 36 na huenda akaamua kuachana na soka ndani ya miaka michache tu ijayo.

Kwa sasa ndiye nahodha wa Yanga lakini amekuwa na nafasi finyu ya kuanza katika kikosi cha kwanza kutokana na kasi yake kushuka huku akikumbwa na majeraha ya mara kwa mara.

Nafasi ya beki wa kati imekuwa ikichezwa na Yondan ambaye naye umri unasogea licha ya kuwa katika kiwango bora, Andrew Vincente ‘Dante’, Abdallah Shaibu ‘Ninja’, Said Juma ‘Makapu’ na Pato Ngonyani..

Makala haya yanakuletea mabeki ambao wanaweza kuchukua mikoba ya mkongwe huyo mzaliwa wa Zanzibar.

Ally Ally-Stand United

Huyu naye ni Mzanzibari kutoka Pemba. Ndiye beki wa kati wa Stand United kwa sasa na kiwango chake kimewakosha wengi. Ally alicheza vizuri mechi dhidi ya Simba na Yanga ambazo ndiyo kipimo halisi cha mchezaji mzuri kwa Tanzania.

Katika mechi ya Simba ambayo ilimalizika kwa sare ya mabao 3-3, Ally alifanya kazi kubwa kwa kuwazuia washambuliaji wa Juma Liuzio, Laudit Mavugo na Nicholas Gyan ambao licha ya kufunga walipata wakati mgumu kwenye mechi hiyo.

Katika mechi dhidi ya Yanga, Ally alicheza sambamba na Obrey Chirwa akitembea naye kila mahali japokuwa baadaye alimzidi akili na kufunga bao moja. Kama mambo yatamnyookea vizuri akatua Jangwani halafu akapigwa msasa na kocha wa viwango vya juu, huenda wakamsahau kabisa Cannavaro.

Yussuf Ndikumana-Mbao

Nahodha huyu wa Mbao FC alikuwa akihusishwa kujiunga na Simba na Yanga tangu msimu uliopita lakini hakuweza kuondoka klabuni hapo kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo ile ya maslahi.

Ndikumana amekuwa mhimili mkubwa katika kikosi cha Mbao tangu msimu uliopita akicheza na Asante Kwasi ambaye kwa sasa yupo Simba na waliweza kuwadhibiti washambuliaji wasumbufu kama Donald Ngoma, Amiss Tambwe wa Yanga, Mavugo na Fredrick Blagnon ambaye alikuwa Simba msimu uliopita.

Msimu huu Ndikumana ameendeleza ubabe wake katika mechi zote ngumu jambo ambalo bado linaweza kuwashawishi mabosi wa Yanga kumsajili.

Hakuna ubishi kuwa kama Yanga itamchukua beki huyu Mrundi anaweza kuwa mbadala wa muda mrefu wa Cannavaro ambaye ameshinda mataji saba ya Ligi Kuu na timu hiyo.

Nurdin Chona-Prisons

Beki kisiki wa kati wa Tanzania Prisons, Nurdin Chona ni mmoja kati ya wachezaji wazoefu katika Ligi Kuu Bara, na amekuwa akicheza katika kiwango ambacho hakishuki kwa wakati wote.

Chona ni aina ya mabeki wagumu ambao wapo wachache Ligi Kuu na kwa mahitaji ya Yanga katika nafasi ya beki wa kati anaweza kucheza tena kwa muda mrefu tu.

Kama Cannavaro ataondoka katika kikosi hicho, Chona atakuwa mtu sahihi kwa uwezo wake wa kuzuia washambuliaji tena akiwa anashirikiana na Dante, Yondan na Ninja mbona mambo yatakuwa mswano.

Hassan Isihaka

Beki wa zamani wa Simba, Hassan Isihaka naye anaweza kuwa mbadala wa muda mrefu wa Cannavaro. Kwanza kabisa ana uzoefu wa kucheza timu kubwa ya Simba na kufikia kiwango cha kuwa nahodha, hivyo Yanga haiwezi kumsumbua hata kidogo.

Isihaka baada ya kuachwa na Simba alijiunga na African Lyon msimu uliopita kabla ya kushuka daraja kisha kutimkia Mtibwa Sugar anayoichezea kwa msimu huu.

Isihaka wa sasa ameimarika zaidi ya yule wa Simba hasa baada ya Kocha wa Mtibwa, Zubery Katwila kumwamini na kumpa nafasi ya kucheza mara kwa mara.

Hakuna dhambi kwa mtu aliyewahi kucheza Simba kutua Yanga, hivyo kwa Isihaka anaweza kuwa mbadala wa muda mrefu tu wa Cannavaro.

Erick Mlilo

Beki mwingine wa kati wa Stand United, Erick Mlilo naye amekuwa akicheza vizuri na kwa maelewano na Ally ambaye tangu wameanza kucheza pamoja wameisaidia timu kwa kuitoa katika nafasi za mkiani mpaka kuifikisha katika nafasi ya 12, kwenye msimamo wa Ligi Kuu.

Mlilo na Ally wametengeneza ukuta mgumu na kuifanya Stand kuwa miongoni mwa timu ambazo zimefungwa mabao machache kwenye mzunguko wa pili wa Ligi Kuu.

Kwa namna beki huyo alivyocheza katika mechi za Ligi Kuu hata zile kubwa za Simba, Yanga na Azam anaweza kabisa kucheza timu kubwa na kwa kiwango cha juu.