Vichaka vya Gareth Bale msimu ujao

Muktasari:

Kinachoelezwa kwa sasa ni kwamba kuna uwezekano mkubwa wa supastaa huyo wa Wales akaondoka kwenye kikosi hicho wakati dirisha lijalo la uhamisho wa wachezaji la majira ya kiangazi litakapofunguliwa.

LONDON, ENGLAND

KAMA maneno yanayosemwa yatakuwa kweli, basi Gareth Bale hatakuwapo kwenye kikosi cha Real Madrid baada ya msimu huu kumalizika. Kinachoelezwa kwa sasa ni kwamba kuna uwezekano mkubwa wa supastaa huyo wa Wales akaondoka kwenye kikosi hicho wakati dirisha lijalo la uhamisho wa wachezaji la majira ya kiangazi litakapofunguliwa.

Kocha Zinedine Zidane anaripotiwa kumtazama Bale kama mchezaji wa kawaida sana, kwamba hayupo kwenye mipango yake na hilo ndilo linaloweka mkazo na kutiliwa nguvu kwamba staa huyo wa zamani wa Tottenham Hotspur habaki. Lakini, jambo hilo linakwenda sambamba na maswali mengi ni wapi atakokwenda Bale baada ya kuondoka Bernabeu. Cheki hizi hapa njia anazoweza kupita Bale baada ya kuachana na wababe hao wa Bernabeu ikihusisha pia Paris Saint-Germain, ambao suala la kusajili mastaa wenye majina makubwa imekuwa kawaida kwa miaka ya karibuni.

Man United

Kwa muda mrefu sana na kwa kujirudiarudia, Manchester United wamekuwa wakihusishwa na mpango wa kumsajili Bale na jambo hilo linadaiwa kwenye dirisha lijalo linaweza likatimia. Taarifa zinadai kuna nafasi kubwa ya staa huyo kutua Old Trafford kabla ya Septemba 3 mwaka huu.

Kocha Jose Mourinho anataka kutengeneza kikosi chake kuwa na uwezo wa kushindana na mahasimu wao Manchester City katika mbio za ubingwa wa Ligi Kuu England msimu ujao. Kitu kingine ni kwamba Man United ndio zao kusajili wachezaji wenye majina.

Tottenham

Kama kweli Bale ataamua kuondoka Real Madrid, basi Tottenham wanaweza kufanya kila wanaloweza kumrudisha supastaa huyo kwenye kikosi chao. Kwa sasa, Spurs wamekuwa wakimtumia Erik Lamela kwenye winga ya kulia, hivyo Bale anahitajika zaidi kutua kwenye timu hiyo kuja kufanya mambo makubwa kama ilivyokuwa awali kabla ya Real Madrid hawajaja na pesa ndefu kunasa huduma yake. Ujio wa Bale utaifanya Spurs kuwa na nguvu ya kuwa washindaji kwenye kufukuzia ubingwa wa Ligi Kuu England kwa sababu atakuja kuunda fowadi matata kabisa sambamba na Harry Kane.

Liverpool

Uwezekano wa kumwona Bale kwenye kikosi cha Liverpool huko Anfield ni finyu, lakini kwenye mchezo wa soka kamwe hupaswi kusema haiwezekani.

Liverpool wanaweza kujizuia kwenda moja kwa moja huko Real Madrid na ofa yao ya kumtaka Bale kwa sababu watageuziwa kibao kwamba wababe hao wa Barnebau nao watamtaka Mohamed Salah.

Lakini, kama Madrid wanamhitaji Salah na mchezaji huyo akiwa tayari kuhamia Hispania, basi Liverpool nao kwa upande wao wanaweza kudai Bale ajumuishwe kwenye dili hilo na hapo ndipo itakapotokea nafasi ya staa huyo wa Wales kutua huko Anfield.

Chelsea

Licha ya kuwapo na hali ya sintofahamu kuhusu kocha huko Stamford Bridge, hakuna ubishi kocha yeyote atakayetua hapo hatakuwa na chaguo jingine zaidi ya kuingia sokoni kwa dirisha lijalo kusajili.

Kiwango cha Chelsea kwa siku za karibuni kinaonekana kusuasua na hakuna ubishi kwamba wanahitaji huduma ya wachezaji mahiri kabisa kama Bale hasa kwa kipindi hiki ambacho staa wao Eden Hazard anahusishwa na mpango wa kutimkia huko Real Madrid kwenye dirisha lijalo la usajili.

Shida ya Chelsea ni kwamba Bale anaweza kukataa kwenda kucheza michuano ya Europa League.

Man City

Licha ya kutumia pesa nyingi kiasi gani kusajili wachezaji wapya, hakuna ubishi Manchester City haitapoteza fursa ya kusajili wachezaji mahiri inapoona inawezekana.

Kocha Pep Guardiola atahitaji kukiboresha kikosi chake kwa ajili ya kufanya vizuri kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya kunyakua ubingwa kwenye Ligi Kuu England msimu huu.

Bale ni moja ya wachezaji ambao wanakufanya kuwa na uhakika wa kufanya vizuri kwenye michuano mikubwa na staili ya soka lenye kasi kubwa linamfanya Bale kuwa na nafasi ya kuingia kwenye kikosi cha Guardiola kama ilivyo kwa Leroy Sane kwa sasa.