Unatokaje Sare Nyumbani na Timu Zisizoeleweka?

Friday April 13 2018

 

MWAKA 2018 unakwenda kasi kuliko hata yale mabasi ya mwendokasi pale Dar es Salaam.

Kama ulikuwa umezubaa fahamu mwaka ndio hivyo unaelekea katikati, hii ni dalili ya siku si nyingi mipango na mikakati mbalimbali ya maendeleo ikiwa ni pamoja na Bunge la Bajeti inatakiwa kwenda sawa.

Bado kidogo mipango ya 2018/19 itapangwa, katika tasnia ya michezo tunatakiwa kutafakari 2017/18 tumefanya nini? Na tumevuna au kupata nini?

Kila mwanamichezo kwa vyovyote vile atajikuta anajiuliza swali moja au mawili iwapo ana hulka ya kutaka kuyajadili mafanikio kwa mapana yake au hata kuutathimini mchezo mmoja tu anaoupenda.

Mtazamo wangu ninauelekeza katika soka, na hii ni kwa sababu Watanzania tulio wengi tunaupenda mchezo huu. Kimsingi ninahisi na kuamini mwaka ukiwa unazidi kukatika sioni dalili zozote za kupata mafanikio ya kujivunia sisi kama taifa licha ya kuthubutu kuingia katika ratiba za mashindano mbalimbali ya kimataifa, kuanzia yale yanayoandaliwa na Cecafa pamoja na CAF.

Hapa nyumbani Ligi Kuu inashika kasi ikiwa katika mzunguko wa 23, hii ikiwa na maana msimu wa 2017/18 unaelekea kumalizika ili tupate wawakilishi wapya katika ngazi ya klabu watakaoshiriki mashindano ya kimataifa mwakani.

Hii ni kawaida na imekuwa ni desturi yetu miaka yote kutii na kufuata utaratibu kwa mujibu wa mzunguko wa kalenda za Cecafa, CAF na Fifa.

Kwa wakati huu macho na masikio ya Watanzania yamebakia kuelekezwa kwenye timu ya U-17 kule Burundi lakini kimsingi ni timu moja tu ya vijana chini ya miaka 20 Ngorongoro Heroes, tena katika mchezo mmoja tu uliobaki dhidi ya vijana wenzao wa DR Congo utakaopigwa ugenini.

Kama wanamichezo tena wazalendo tuna wajibu wa kupeana moyo na kuwatia moyo wa matumaini ya kupata ushindi vijana wetu watakaotuwakilisha huko, lakini kwa jicho la kiufundi tuna nafasi finyu sana ya kufanya vizuri na hatimaye kusonga mbele kwenda Niger.

Mtiririko wa matokeo mabaya ya timu zetu zote zilizoshiriki mashindano makubwa mwaka huu katika ngazi ya klabu na timu zetu za taifa (wakubwa, vijana, wanawake) umechangiwa kwa kiasi kikubwa na mambo makuu mawili. Moja ni maandalizi hafifu na pili kushindwa kupata ushindi kwenye michezo ya nyumbani. Huu umekuwa ni ugonjwa sugu katika michezo ya kimataifa. Unatoaje sare na mwendawazimu nyumbani?

Rekodi zipo nyingi, lakini chache za mwaka huu kuanzia Januari hadi Aprili zinatosha kuthibitisha hali halisi ya timu zetu kushindwa kulibeba soka letu. Klabu zetu za Simba na Yanga zimekutana na kikwazo kutoka kwa timu za Misri na Botswana.

Yanga imepata nafasi ya kikanuni ya kushiriki kwenye Kombe la Shirikisho na tayari imecheza mchezo wa kwanza dhidi ya Welaytta Dicha ya Ethiopia, na inasubiri mchezo wa marudiano huko ugenini.

Ni faraja kwa Wanayanga na Watanzania timu imepata ushindi wa mabao mawili, ni vizuri ijipange kwa nguvu kwa ajili ya kuvuka hatua hii na kuingia makundi.

Tumeshuhudia kilichoikuta Twiga Stars wiki ilyopita kushindwa kuvuka kwenye mchezo wa kwanza dhidi ya Zambia (Chipolopolo), wengi waliweka matumaini kwa timu hiyo lakini maandalizi yasiyokidhi mahitaji ya kiufundi na matarajio ya walimu wa timu yetu ya wanawake yamesababisha ipate matokeo ya sare hapa nyumbani ya mabao 3-3.

Sare hiyo haikustahili kama vijana wetu wangesimama imara. Matokeo yake Jumapili iliyopita ya sare katika mchezo wa pili kule Zambia yamekuwa ni faida kwa wapinzani wetu kusonga mbele.

Huu ni utamaduni unaoumiza na kuzidi kufifisha moyo wa wapenzi wa mpira kukata tamaa dhidi ya soka la Tanzania.

Katika suala zima la kubadilisha sura na taswira ya soka letu, ni wajibu na jukumu la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kufanya na kujenga mikakati ya kubadilisha hali hii.

Kushindwa kufanya vizuri kwa timu zetu katika michuano mbalimbali kumesababishwa na mazingira yanayofanana, hii ina maana kuna uhusiano wa karibu kati ya matokeo, usimamizi wa timu na mtizamo wa watendaji katika timu zetu.

Lakini pia ipo haja ya kuangalia ni kitu gani kinachokwamisha timu zetu kufanya vizuri, haiwezekani kupata matokeo kama haya halafu tuyaone ya kawaida katika michezo kisha tukaridhika tu, bila kuchukua hatua za kutafuta sababu.

Zipo nadharia nyigi ambazo zinajaribu kutoa nafasi ya wadau kuridhika na aina yoyote ya matokeo mfano; michezo ina matokeo matatu (kushinda, kushindwa au sare) au asiyekubali kushindwa si mshindani.

Binafsi si vibaya tukakubaliana na falsafa hizi lakini ni vema tupime na kutathimini ili kujua ni kwa kiasi gani au kiwango gani timu zetu zinaangukia upande upi katika mizani kushindwa ua kushinda ili itusaidie kuamua ni wapi tuweke nguvu zaidi.

Wakati ligi ikielekea mwishoni na timu zetu za Simba, Twiga Stars zimetolewa. TFF na wadau tuendelee kufikiria ujio wa fainali za vijana za Afrika U-17, huo ni mtihani mgumu unaohitaji juhudi za kutosha ili tuhakikishe tunafanya vizuri.

Pia, klabu zetu zitakazoshiriki michezo mikubwa ya kimataifa, timu za taifa kwa ngazi zote pia. Aibu na machungu ya mwaka huu tusingependa yatukute tena msimu ujao.