Mkimzingua Zahera, inakula kwenu mjue-2

Tuesday May 15 2018

 

By KHATIMU NAHEKA NA THOMAS NG’ITUDAR ES SALAAM

JANA Jumatatu katika makala ya mahojiano maalumu na Kocha Mkuu Mpya wa Yanga, Mwinyi Zahera, kocha huyo aliweka bayana jinsi alivyobaini uimara na udhaifu wa kikosi cha Yanga na mipango yake ya kutaka kuifanya iwe tishio ndani na nje ya Tanzania.

Pia alifichua namna ambavyo anashindwa kumuelewa kipa, Youthe Rostand jinsi anavyofungwa mabao ya aina moja na kufichua namna alivyokaa na Kocha wa Makipa, Juma Pondamali. Tiririka naye akisisitiza anavyotaka Rostand awe sambamba na kufichua mipango zaidi ya kuibadilisha Yanga ili kuleta ushindani katika Ligi Kuu na anga za kimataifa. Endelea...!

“Nimeshaanza kulifanyia kazi hilo nimeongea na kocha wa makipa (Juma Pondamali) ameniambia tatizo ni kipa mwenyewe habadiliki, nimepanga kukutana na uongozi kujadiliana nao hili waliniambia kuna dawa wanaitafuta juu ya kukabiliana na hili tatizo.

“Kwa sasa siwezi kusema nitasajili kipa mwingine kwa kuwa kuna yule kipa mdogo nimeangalia upungufu wake ni mchache kuliko wa huyu kipa wa kwanza (Rostand) lakini anahitaji muda kuwa na uzoefu wa kutosha pia kuna kipa namba mbili nimeambiwa ni mzuri tatizo anaumwa nitamwangalia naye ubora wake.”

YUPO KIMATAIFA ZAIDI

Alipoulizwa nafasi ya Yanga katika ushiriki wake wa Kombe la Shirikisho Afrika ikiwa Kundi D na hasa baaada ya kuchezea kipigo cha mabao 4-0 toka USM Alger, Kocha Zahera anafunguka akisema;

“Yanga bado ina nafasi hii ni mechi moja ambayo tumepoteza, kumbuka tumecheza mechi ile bila ya wachezaji muhimu na tegemeo, kuna mambo mengi ambayo yalitokea kabla na katika mchezo huo lakini ukiondoa Alger ambayo ina pointi tatu wengine wana pointi moja na sisi hatuna pointi.

“Hii ndio iliyonifanya nikibakishe kikosi changu kamili Dar na kupelekea kikosi cha pili kule Mbeya na hata Morogoro, kwa nia ya kuhakikisha mechi yetu ijayo dhidi ya Rayon tunafanya vizuri kutengeneza nafasi ya kumaliza wa pili kundini.”

Zahera anasema ni muhimu mno kwa Yanga kupata matokeo mazuri nyumbani katika mchezo huo wa kesho Jumatano, ili kusubiri kujua majaliwa yao kwa mechi zitakazosalia zikiwamo mbili za ugenini dhidi ya Rayon na Gor Mahia.

TIZI LA AKILI JANGWANI

Akizungumzia jinsi atakavyoanza kugawa dozi ya mazoezi kwa vijana wake, Kocha Zahera anasema ili Yanga iweze kuiva ni lazima kuwe na vipindi viwili vya mazoezi ambapo muda wa sasa wa mazoezi hawezi kukubaliana nao. “Unajua mechi moja inachezwa kwa dakika 90, lakini hakuna timu ambayo imetumia muda wote huo kucheza, kawaida katika dakika 90 wachezaji wanatumika kwa dakika 75 huo ndiyo muda ambao wachezaji hukimbia, dakika zilizosalia 15 hupotea katika kupiga kona na faulo zingine na matukio mengine.

“Hivyo unapokuja katika mazoezi ni lazima ujue kuwatumikisha wachezaji wawe tayari kwa zaidi ya dakika 90, ili wawe tayari kumudu kukimbia kwa zaidi ya dakika 75, hapa Yanga nimelikuta ukiangalia mazoezi yao wakati nafika nilikuta kuna mazingira ya kupoteza muda sasa kwa mazingira yale ni lazima vijana wawe na mapungufu hayo.

“Tutarekebisha mambo na lazima tuwe na muda zaidi wa mazoezi ikiwezekana hata vipindi viwili, ili vijana waive na kufanya makubwa uwanjani,” anasema.

HATAKI MIZINGUO

Akizungumzia aina ya adhabu atakazokuwa akitoa kwa wale watakaomzingua, anasema hawezi kuwa mkali kwa haraka ambapo atakachofanya anaweza kumsamehe mchezaji kwa kosa la kwanza, ila lakini akirudia lazima ampe displini kali.

“Ikitokea mchezaji kakosea mara ya kwanza nitamsamehe, ila akirudia tena kwa kosa lile lile yaani kwa amekosa mazoezi bila kutoa taarifa kwa meneja wa timu au daktari nitaagiza uongozi ukate sehemu ya mshahara wake, nitaomba mikataba yao nijue ikoje kama haitakuwa na adhabu za namna hiyo tutaziweka ili ziweze kufahamika kwao.

“Anayerudia kwa hakika sitaweza kumvumilia nitamtimua na akitokea kiongozi akimrudisha nitaondoka mimi,” .

KABWILI, ABDUL CHUPUCHUPU

Kocha Zahera anasema; “Hivi karibuni lilitokea kosa moja kwa Juma (Abdul) na yule kipa mdogo (Ramadhan Kabwili) walitakiwa waende Mbeya na timu walitangaziwa hilo lakini niliambiwa hawakwenda, nilikasirika sana nikataka kujua sababu.

“Niliwauliza uongozi bahati yao kumbe walitoa ruhusa sikutaka kuona mambo kama haya yanatokea katika timu yangu kama wangekosa sababu ya msingi nisingewaruhusu kujiunga na timu bila kupewa adhabu niliona kama walitaka kufanya dharau, tunafanya hivyo ili kuweka uwajibikaji.”

HAKI ZA WACHEZAJI

Kocha Zahera anafahamu ndani ya Yanga mambo sio mazuri kifedha, lakini anatoa njia ya kukabiliana na changamoto hiyo, ili kutoyumbisha wachezaji.

“Hili ni soka la Afrika wakati nafika hapa nilishajiandaa kisaikolojia lakini nitawaambia uongozi ili kazi ifanyike vizuri maslahi ya wachezaji yanatakiwa kuzingatiwa. Hilo likikaa sawa kwangu itakuwa rahisi kuwabana wachezaji, vinginevyo ni tatizo,”

AMEIONAJE SIMBA?

Kocha Zahera alikuwapo wakati Yanga ikipokea kichapo cha bao 1-0 toka kwa watani wao wa Simba, alikuwa jukwaani alipoulizwa amewaonaje mabingwa hao wapya wa ligi msimu huu?

“Nimeiona Simba hasa kwenye pambano lile la watani. Kwa hakika ni timu nzuri naiheshimu, lakini sio ngumu wala inayotisha, sikuona kitu tishio kutoka kwao, japo ilitufunga, ni mapungufu ya Yanga sio kitu kingine.

“Kifupi niliiona ni timu inayojua kukimbia sana na kutumia makosa ya wapinzani, ila kwa kuwa nipo nitawafuatilia zaidi na kuona namna ya kuidhibiti tutakaopokuja kukutana tena, kama Yanga ingekuwa imara sidhani kama Simba ingeshinda.”

Kocha Zahera amefichua aina ya soka analotaka timu yake icheze na kudokeza usajili atakaoufanya. Je, unajua mipango yake kwa benchi hilo ni ipi na wachezaji gani anaowataka? Ungana naye Alhamisi upate majibu. Itaendelea...