‘Mjukuu’ wa Ferguson aliyemzima Leroy Sane

Muktasari:

  • Jina lake kamili ni Trent John Alexander-Arnold na alizaliwa Oktoba 7, 1998 katika Jiji la Liverpool eneo la West Derby. Alijiunga na Shule ya Soka ya Liverpool mwaka 2004 akiwa na miaka sita tu.

LIVERPOOL, ENGLAND

MMOJA kati ya mastaa wa Liverpool waliowashangaza mashabiki katika pambano la Jumanne usiku ni kinda Alexander-Arnold. Alimkaba vilivyo winga, Leroy Sane na akaidhibiti vilivyo safu ya ushambuliaji ya Manchester City katika kiwango cha kushangaza. Jikumbushe kuhusu kinda huyu alikotokea.

Atinga Liverpool akiwa na miaka sita

Jina lake kamili ni Trent John Alexander-Arnold na alizaliwa Oktoba 7, 1998 katika Jiji la Liverpool eneo la West Derby. Alijiunga na Shule ya Soka ya Liverpool mwaka 2004 akiwa na miaka sita tu.

Ilikuwa ni baada ya kuonwa na kocha wa timu hiyo ya watoto ya Liverpool, Ian Barrigan.

Uwezo wake ulimfanya awe nahodha wa timu ya vijana chini ya umri wa miaka 16 na baadaye akawa nahodha wa chini ya umri wa miaka 18 katika kikosi kilichokuwa chini ya Pep Lijnders.

Alifanya vizuri katika shule hiyo na mwaka 2015 nahodha wa zamani wa Liverpool, Steven Gerrard alimtaja katika kitabu chake kama kinda ambaye atakuja kufanya mambo makubwa usoni.

Msimu huu 2015/16, Alexander-Arnold alichaguliwa katika kikosi cha kwanza cha Kocha, Brendan Rodgers ambacho kilicheza pambano la mwisho la maandalizi ya msimu mpya dhidi ya Swindon Town huku Liverpool ikishinda 2-1.

Msimu uliopita, Alexander-Arnold alichukuliwa katika ziara ya Liverpool Marekani kwa ajili ya maandalizi ya msimu mpya. Alicheza mechi yake ya kwanza katika kikosi cha wakubwa katika pambano la Kombe la Ligi dhidi ya Tottenham Oktoba 2016.

Katika pambano hilo alipewa kadi ya njano kwa kumchezea rafu, Ben Davies na baadaye akatolewa huku nafasi yake ikachukuliwa na beki chaguo la kwanza, Nathaniel Clyne katika dakika ya 68. Baada ya pambano hilo, nahodha wa zamani wa Liverpool, Graeme Souness alimsifu Alexander-Arnold akidai ‘alikuwa na sifa zote za kuwa mchezaji wa kiwango cha juu.”

Novemba 8, 2016 Liverpool ilitangaza Alexander-Arnold, pamoja na makinda wengine, Kevin Stewart na Ben Woodburn, walikuwa wamepewa mikataba ya muda mrefu klabuni hapo. Alianza tena katika mechi iliyofuata Kombe la Ligi dhidi ya Leeds United na kupika bao la Divork Origi katika ushindi wa mabao 2-0. Katika pambano hilo alichaguliwa kuwa mchezaji bora wa mechi.

Alicheza mechi yake ya kwanza ya ligi Desemba 14 katika pambano dhidi ya Middlesbrough ambalo walishinda 3-0. Katika pambano hilo aliingia kuchukua nafasi ya Origi. Akaanza mechi yake ya kwanza ya ligi Januari 15, 2017 katika pambano gumu dhidi ya Manchester United.

Aweka rekodi Ulaya

Mei 9, 2017 alitajwa kuwa Mchezaji Bora Chipukizi wa Mwaka wa Liverpool. Msimu wake wa kwanza alijikuta akicheza mechi 12 katika michuano mbalimbali. Katika maandalizi ya msimu huu Liverpool ilimpa mkataba mwingine mrefu na Agosti 15 alifunga bao lake la kwanza la msimu Ulaya kwa mpira wa adhabu katika pambano la kufuzu Ligi ya Mabingwa dhidi ya Hoffenheim waliloshinda 2-1

Kwa kufunga bao hilo aliweka rekodi ya kuwa mchezaji mdogo wa tatu kuifungia Liverpool katika michuano ya Ulaya mechi yake ya kwanza. Waliomtangulia ni Michael Owen na David Fairclough. Katika hatua ya makundi Alexander-Arnold alifunga tena katika ushindi wa mabao 7-0 dhidi ya Maribor Oktoba.

Akafunga bao jingine siku moja baada ya Sikukuu ya Krismasi katika ushindi wa mabao 5-0 dhidi ya Swansea City uwanjani Anfield. katika pambano la Jumanne usiku dhidi ya Manchester City, kinda huyu aliweka rekodi ya kuwa mchezaji mdogo wa Kiingereza kuanza katika mechi ya robo fainali Ligi ya Mabingwa.

Katika mchezo huo, Alexander-Arnold aling’ara vilivyo kiasi cha kutajwa kuwa mchezaji bora wa mechi na alimzima kabisa winga wa City, Leroy Sane ambaye msimu huu amezidi kuwa msumbufu kwa mabeki i anaokutana nao.

Bibi yake atembea na Ferguson

Katika historia ya kusisimua ya Alexander-Arnold, bibi yake, Dooreen Carling aliwahi kuwa mpenzi wa kocha wa zamani wa Manchester United, Sir Alex Ferguson. Baadaye bibi huyo alitimkia Marekani katika Jiji la New York.

Hadi sasa Alexander-Arnold ana haki ya kuichezea Timu ya Taifa ya Marekani kutokana na asili hiyo ya bibi yake. Hata hivyo, hadi sasa ameichezea Timu ya Taifa ya Vijana ya England U-21 na kabla ya hapo alipita katika ngazi nyingine.

Mechi yake ya kwanza cha U-21 ilikuwa Septemba 5 katika pambano dhidi ya Latvia lililochezwa Bournemouth.

Akiwa bado katika kikosi hicho, alialikwa kufanya mazoezi na kikosi cha wakubwa Machi, mwaka huu wakati wakijiandaa na mechi za kirafiki dhidi ya Italia na Uholanzi.