Huyu One punch! achana naye kabisa

Muktasari:

Kipaji chake kiliibuliwa na kocha Rama Jaha, enzi hizo Mfaume alikuwa mshambuliaji wa timu ya soka ya Faru Dume, kocha akamwambia “Dogo huko kwenye soka sawa cheza ila ukiingia kwenye ndondi utakuwa mtamu zaidi”.

JINA lake la utani ni ‘One Punch’ akimaanisha ngumi moja tu ‘chali’ japo wengi wanamfahamu kama Mfaume Mfaume jina lake halisi ni Mfaume Ahmad Said.

Kipaji chake kiliibuliwa na kocha Rama Jaha, enzi hizo Mfaume alikuwa mshambuliaji wa timu ya soka ya Faru Dume, kocha akamwambia “Dogo huko kwenye soka sawa cheza ila ukiingia kwenye ndondi utakuwa mtamu zaidi”.

Mambo yalianza hivi

“Sikuwa nauelewa na uchezaji wa ngumi, sikujua kupiga jebu, kujipanga wala mbinu yoyote ya ngumi, japo nilikuwa nikiufuatilia mchezo huo lakini kipindi hicho nilikuwa namba tisa wa timu ya soka ya Faru Dume.

“Ilikuwa mwaka 2011, kocha Rama Jaha alinifuata na kuniambia Mfaume nataka uingie kwenye ngumi, kwa kuwa nilikuwa nazipenda ila sikujua nianzie wapi wala sikujivunga, nikajiunga fasta kwenye kambi ya Nakos ya Mabibo.

Huko Nakos camp Pengo hakumkubali hata kidogo

Kujiunga kwa Mfaume Nakos kulichafua hali ya hewa sio kidogo kwani anakwambia haikuchukua muda mrefu, kocha akaanza kukubali kiwango chake ila akakutana na kigingi cha nahodha wa kambi, Habibu Pengo.

“Katika vitu ambavyo vilimfurahisha kocha ni kujituma kwangu, kitu ambacho Pengo hakupendezwa nacho, kilichomchukiza zaidi ni mimi kupewa unahodha wa Nakos.

“Pengo aliamua kuhama ‘camp’ na kutimkia Manzese lakini bado uhasama ulibaki pale pale na ulikolezwa zaidi kwenye pambano langu na Jonas Segu.

“Nilishinda pambano lile kitu ambacho Pengo hakukubaliana nacho kwani yeye aliwahi kupigwa na Segu, ilifikia mahali akawa anatoa maneno ya ‘shombo’ kwangu na kujitangaza kuwa ndiye rais wa ndondi Manzese baada ya kukimbia Mabibo.

“Tulikubaliana atakayeshinda mbali na ubingwa ndiye awe rais wa ngumi Manzese na Mabibo,” anasema Mfaume.

Kumbe kocha alipanga matokeo

Katika vitu ambavyo viliwasumbua mashabiki wa Mfaume ni uchezaji wake wa kumdharau Pengo hadi walipomaliza raundi zote 10 na Mfaume kutawazwa kuwa bingwa wa Afrika Mashariki na Kati.

“Lile pambano nilikuwa na uwezo wa kushinda kwa KO (knock out) lakini kocha (Rama Jaha) alinikataza, aliniambia Mfaume nenda kacheze ngumi zote nilizokufundisha, mdharau mpinzani wako vile unavyoweza, lakini tu usimpe KO.

“Sikuwa na namna zaidi ya kusikiliza maelekezo ya kocha, ingawa nilikuwa na uwezo wa kumaliza pambano raundi ya pili, lakini sikutaka kwenda kinyume na maelekezo ya kocha,” anasema.

Anavyolikumbuka pambano na Matumla Jr

Huku akionyesha sura ya huzuni, Pengo anasema kabla ya pambano lake na Mohamed Matumla Jr hilo lililofanyika Februari 5 mwaka jana alikwenda kupiga kambi milimani.

“Nilijiandaa, nilijua ni pambano gumu kutokana na familia anayotoka Muddy kuwa ya ndondi, nilijua kweli kweli, lakini sikutarajia kama itatokea hadi Muddy awe katika hali ile,” anasema.

Katika pambano hilo, Matumla Jr alipigwa kwa Knock Out (KO) na kupoteza fahamu ulingoni ambako alikimbizwa hospitali ya Temeke kabla ya kuhamishiwa Muhimbili ambako ilibainika amepata ufa kwenye fuvu la kichwa hivyo kutakiwa kuwa nje ya ulingo kwa miaka miwili.

“Ni tukio ambalo sipendi kulikumbuka, lakini lilitokea katika hali ya mchezo,” alisema Mfaume kwa masikitiko.

Maisha ya Mfaume nje ya ngumi

Mfaume ni bachela, hana mke wala mtoto anaishi kwao Mabibo na wazazi wake.

“Sijabahatika kupata mali kupitia ngumi, bado ngumi zinanidai ila ninaamini nikikaza buti maisha yatanyooka tu,” anasema Mfaume.

Anasema kwa elimu yake na jinsi anavyoishi ni tofauti kwani bila ngumi uenda mambo yangekuwa magumu, lakini fedha kidogo anayopata kwenye masumbwi anaendesha maisha siku zinakwenda ingawa anaamini kwa kujituma ipo siku ngumi zitamtoa.

Rekodi ya Mfaume kwenye ndondi

Mfaume alianza kwa ushindi wa TKO katika pambano lake la kwanza la ndondi za kulipwa dhidi ya Omari Tindikali kwenye uzani wa light lililofanyika Juni 28, 2014 jijini Dar es Salaam.

Hadi sasa amekwishashinda mapambano 12 (4 kwa KO), ametoka sare mara mbili na mabondia waliowahi kumpiga tangu 2014 ni Georgi Chelokhsaev na Gabor Veto na kwa Tanzania amepigwa na Cosmas Cheka pekee.

Sikia hii ya Mayweather sasa

Mashabiki wa Mfaume wanatamani kushuhudia pambano dhidi ya Ibrahim Class, lakini Mfaume mwenyewe anakwambia sio Class tu hata akija Floyd Mayweather yuko tayari kuzichapa.

“Niko tayari kuzichapa na bondia yoyote, ni kweli mashabaiki wanatamani kuona pambano langu na Class ingawa sina uhakika kama atakubali.

“Ila mimi niko tayari kucheza na bondia yeyote yule hata ikitokea nimepata bahati ya kupigana na Mayweather, wala sita paniki, nitacheza vizuri tu,” anasema.

Msikie kocha wake

Rama Jaha ndiye kocha anayemnoa Mfaume, kocha huyu amewaibua mabondia wengi nchini na wengine hivi sasa ni makocha, lakini anakwambia kwa Mfaume ‘amelamba dume’.

“Katika vitu ninavyojivunia kwenye ngumi na Mfaume, ‘dogo’ kwanza ana nidhamu ya mchezo, hatumii nguvu ya ziada kupata ‘stimu’ za kupigana, yuko vizuri, anafundishika na kwa jinsi anavyokwenda atafika mbali,” anasema.