Huu mchongo wa Abdul Hilal upo hivi unaambiwa

Monday May 7 2018

 

By ELIYA SOLOMON

UPENYO mdogo unaweza kukufanya utoboe. Usichukulie poa aisee, kwa sababu kutoka kisoka kwa hata nyota wa zamani wa Chelsea, Didier Drogba, kulichangiwa na safari ya kwenda Ufaransa kwa mjomba wake.

Drogba ambaye ni mzaliwa wa Abidjan, Ivory Coast alisafirishwa na wazazi wake akiwa na miaka mitano kwenda kwa mjomba wake, Michel Goba.

Lakini alirejeshwa Abidjan kutokana na kuumwa kwake. Kipaji chake cha soka kilionekana miaka mitatu baadaye pale ambapo mama yake, Clotilde alipokuwa akimkataza kucheza soka kila siku kwenye pakingi ya magari yao.

Kupoteza kazi kwa wazazi wake wote wawili, ulikuwa ni upenyo mwingine wa Drogba kupelekwa tena Ufaransa, ili akaishi na Goba kutokana na hali ya maisha ya wazazi wake.

Huo ndio ukawa mwanzo wa straika huyo ambaye kwa sasa anaichezea timu yake anayoimiliki ya Phoenix Rising kutoboa kwa kucheza soka la vijana nchini humo kabla ya kufanya makubwa na Chelsea, 2004–2012.

Unatamani kujua mikasa ya nyota wa Kitanzania ambao wanacheza soka nje ya nchi ilivyokuwa mpaka wakatoboa? Nje ya Bongo ipo kwa ajili yako kukuletea mikasa hiyo.

Leo tunaye winga, Abdul Hilal (23) wa Tusker ya Kenya ambaye kwa sasa anacheza kwa mkopo Chemelil Sugar wakati huo akiwa amesaini mkataba wa awali wa kujiunga na Zanaco ya Zambia.

Abdul anasema alianza kucheza soka kwenye Kituo cha D.Y.O.C kilichopo maeneo ya Sigara TCC Chang’ombe chini ya makocha, Rmadhani Aluko, Sizza Mpunda na Brown Ernest.

“Nilikaa kwenye hicho kituo kwa miaka minane tangu 2001 baada ya hapo maisha yalisogea na nikapata nafasi ya kuwa miongoni mwa wachezaji ambao walichanguliwa kwa ajili ya mashindano ya Copa Cocaccola 2010 nikitokea Temeke.

“Hakutufanya vizuri na tukaambulia nafasi ya tatu, baada ya mashindano nikajiunga na African Lyon, kwa mara ya kwanza nilisaini mkataba wa miaka 2.

“Nilikuwa mdogo, lakini nilikuwa napata nafasi ya kucheza mara kwa mara kikosi cha kwanza, kipindi hicho timu ikiwa Ligi Kuu Bara ,” anasema winga huyo wa Tusker.

Maisha yake yaliendelea akiwa na Lyon lakini anadai ndoto yake ilikuwa ni kucheza soka nje ya nchi, hivyo ilibidi aanze mchakato wa kwenda kufanya majaribio kwa gharama zake mwenyewe.

“Nilianza DR Congo kwenye timu ya FC Lupopo, nilifanya majaribio kwa wiki mbili na kufanya vizuri lakini changamoto iliyojitokeza ni kwamba kicho kipindi kilikuwa ni cha uchaguzi wa viongozi wapya ndani ya klabu hiyo.

“Mambo yalienda fyongo na aliingia Rais mwingine aliyeingia na mipango yake mingine na hata suala langu la kusajiliwa liliwekwa kando, ilibidi nijiongeze kwenda Kenya kujiunga Tusker.

“Sikupata wakati mgumu Kenya kwa sababu nilipogusa mpira wangu wa kwanza waligundua kuwa mimi ni mchezaji, hivyo waliamua kuniweka pembeni,” anasema Hilal.

Winga huyo anasema baada ya kukatishwa kuendelea na majaribio yale, alijikuta akipewa mkataba wa kuichezea Tusker aliyopanga kutumia nafasi kama njia ya kupenya.

Akiongelea uamuzi wake wa kuomba kutolewa kwa mkopo na Tusker msimu huu wa 2017/ 2018 huku akidaiwa kuingia mkataba wa awali wa kujiunga na Zanaco, Hilal anafafanua.

“Huu msimu sikuuanza vizuri Tusker, nimejikuta napoteza nafasi ya kucheza mara kwa mara kwa hiyo niliona ni bora niombe kutolewa kwa mkopo ili nirudishe makali yangu.

“Sina mapango wa kuendelea kucheza zaidi Kenya na ndio maana nimeingia mkataba wa awali na Zanaco, kanuni zinaniruhusu kwa sababu makataba wangu na Tusker unamalizika mwishoni mwa msimu.

“Nimepanga kucheza Zambia msimu ujao maana nimemalizana nao bado kusaini mkataba rasmi, nachotaka ni kupambana ili nicheze ligi kubwa zaidi na zenye ushindani,” anasema nyota huyo aliyeifungia Chemelil ambayo amejiunga nayo mwaka huu mabao saba.

Kama akitua rasmi Zambia, Hilal atakuwa Mtanzania wa pili kucheza Ligi Kuu nchini humo, David Naftal ni kiraka wa Kitanzania anayetesa na Kabwe Warrios ya huko.

Drogba aliweza kwa namna yake kutoboa, basi hata wachezaji wa Kitanzania wanaweza kufika mbali na kucheza ligi kubwa zenye ushindani barani Ulaya kama ilivyo kwa wachezaji wengi wa mataifa ya Afrika Magharibi.

Hii ndio safari ya Hilali na bado inaendelea kuelekea kwenye mafanikio.