Hivi ndio viatu vya Mercurial vitakavyopamba Russia 2018

Muktasari:

Katika fainali zijazo zitakazofanyika huko Russia miezi miwili ijayo, Nike imekuja na dizaini tano tofauti za viatu ambavyo watapewa mastaa kuvaa kwa ajili ya fainali hizo tu.

RUSSIA, MOSCOW

FAINALI za Kombe la Dunia zinapofika huwa zina utamu wake. Huwa zina mambo yake yanayovutia.

Katika fainali zijazo zitakazofanyika huko Russia miezi miwili ijayo, Nike imekuja na dizaini tano tofauti za viatu ambavyo watapewa mastaa kuvaa kwa ajili ya fainali hizo tu.

Nike ina mastaa wake wanaovaa viatu vyao, hivyo mtindo mpya wa viatu vitakavyotumika kwenye fainali hizo za Russia, ni maboresho ya viatu vilivyowahi kutumika kwenye fainali tano za Kombe la Dunia zilizopita, ambavyo vilivaliwa na kina Ronaldo wawili, yule Ronaldo orijino wa Brazil na Cristiano Ronaldo wa Ureno.

Matoleo hayo matano ya viatu vipya vitakavyotumika kwenye fainali hizo vitahusu dizaini ya Mercurial, ambavyo matoleo matatu yalivaliwa na Ronaldo wa Brazil katika fainali za Kombe la Dunia 1998 zilizofanyika Ufaransa, fainali za 2002 zilizofanyika Korea Kusini na Japan na fainali za 2006 zilizofanyika Ujerumani.

Dizaini nyingine ya Mercurial iliyoboresha inahusu viatu alivyovaa Ronaldo wa Ureno katika fainali za Kombe la Dunia 2010 zilizofanyika Afrika Kusini na Kombe la Dunia 2014, ambapo fainali zake zilifanyika Brazil.

Viatu hivyo sasa vimetengenezwa kisasa, vikipunguzwa uzito na kuwekewa nyuzi vizuri, lakini ni dizaini ileile ya Mercurial, ambayo imekuwa ikitamba kwenye soka kwa miaka 20 sasa tangu ilipozinduliwa kwa mara ya kwanza.

Dizaini ya kwanza kabisa ya Mercurial ilivaliwa na Ronaldo wa Brazil katika fainali za Kombe la Dunia 1998, zilizofanyika Ufaransa ambapo wenyeji wa fainali hizo, Les Bleus waliichapa Brazil 3-0 na kunyakua ubingwa.

Kiatu chenyewe kilikuwa na rangi ya bendera ya Brazil, bluu na njano na nembo ya Nike, ikiwekwa juu yake, ambayo ina rangi za bendera ya wacheza Samba.

Katika fainali za Kombe la Dunia 2002 zilizofanyika Korea Kusini na Japan, Nike ilikuja na dizaini nyingine ya Mercurial na kumvisha tena supastaa Ronaldo, ambaye aliing’arisha Brazil kubeba ubingwa kwa kuichapa Ujerumani katika fainali, huko staa huyo alikipiga mabao mawili pekee yake kwenye ushindi wa 2-0. Safari hii viatu hivyo vilikuwa na rangi ya fedha na kuwekwa ukijani kwa ndani ambao ni rangi ya bendera pia ya Brazil. Viatu hivyo vilikuwa na bahati sana na Ronaldo, ambapo aliibuka kinara wa mabao katika fainali hizo zilizofanyika Bara la Asia.

Miaka minne baadaye, zilipokuja fainali nyingine za Kombe la Dunia huko Ujerumani, Nike ilitoa mzigo mwingine wa viatu vya Mercurial na kumvisha tena Ronaldo wa Brazil. Dizaini hiyo ya viatu vya Kombe la Dunia 2006, vilikuwa na rangi ya njano na ukijani fulani hivi, huku nembo yake ya Nike ikiwa nyeusi. Akiwa na buti hizo, Ronaldo aliweka rekodi kwenye fainali hizo kwa kufikisha mabao 15 ambayo yalidumu kwa muda mrefu sana kuja kufikiwa, hadi alipokuja kufanya hivyo Miroslav Klose wa Ujerumani kwenye fainali za Brazil 2014. Katika fainali hizo za Ujerumani, Brazil iliishia hatua ya robo fainali baada ya kuchapwa na Ufaransa ya Zinedine Zidane.

Ilipokuja zamu ya fainali za Kombe la Dunia 2010 huko Afrika Kusini, Nike iliamua kuhamia kwa Ronaldo mwingine, ilipomvisha dizaini mpya Mercurial kwa ajili ya fainali hizo tu.

Kiatu alichovaa CR7 katika fainali hizo za Afrika Kusini kilikuwa na rangi ya udongo na orenji. Akiwa na buti hizo, Ronaldo aliisaidia Ureno kufika hatua ya 16 bora kwenye fainali hizo na kusukumwa nje baada ya kuchapwa 1-0 na majirani zao, Hispania, ambao walikwenda kuwa mabingwa.

Huko na huko zikafika fainali za Kombe la Dunia 2014, zilizofanyika kwenye ardhi ya Brazil na Ujerumani kubeba ubingwa kwa kuichapa Argentina kwenye mechi ya fainali. Kwenye mikikimiki hiyo, ambapo mpira uliokuwa ukitumika ulifahamika kwa jina la Brazuca, Nike ilitoa dizaini mpya ya Mercurial na kumvisha tena Ronaldo wa Ureno. Safari hii kiatu hicho kilikuwa na rangi nyekundu na njano kulingana na bendera ya Ureno. Hata hivyo, mambo ya Ronaldo hayakuwa mazuri, ambapo Ureno yake iliishia hatua ya makundi ikishindwa kutamba mbele ya Ujerumani na Marekani.