Bocco kanikumbusha hadithi ya straika Robin Van Persie

Muktasari:

Wenger anaondoka akiwa na heshima japo mwishoni aliitia doa. Anakumbukwa kwa kubadili soka la Arsenal na soka la Kiingereza kwa jumla. Ni mwanamapinduzi wa soka.

KISIKI kimeondoka. Ni Arsene Wenger. Ni baada ya maisha ya shaka kati yake na mashabiki wa Arsenal tangu mwaka 2004 wakati Arsena; ilipochukua ubingwa wa England kwa mara mwisho. Tangu hapo mashabiki wamemdai Arsene ubingwa mpaka wamechoka.

Wenger anaondoka akiwa na heshima japo mwishoni aliitia doa. Anakumbukwa kwa kubadili soka la Arsenal na soka la Kiingereza kwa jumla. Ni mwanamapinduzi wa soka.

Hata hivyo, miaka yake ya mwisho pale Arsenal alionekana kuishiwa maarifa. Alionekana kuchemka katika suala la menejimenti. Wachezaji wake walifanikiwa kufika katika mwaka wa mwisho wa mikataba yao bila ya kupewa mikataba mipya. Ni kama ilivyotokea kwa Robin van Persie, Samir Nasri, Alexis Sanchez, Aaron Ramsey mkataba wake unamalizika mwisho mwa msimu ujao. Jack Wilshere ataondoka bure mwishoni mwa msimu huu.

Mwaka 2012 alilazimika kumuuza Van Persie kwenda Manchester United kwa sababu alikuwa amebakiza mwaka mmoja na angeweza kuondoka bure. Ni Van Persie ndiye ambaye alikuja kumrudi Wenger baadaye.

Kwanini umuache staa wako aende kuongeza nguvu kwa jirani? Kwanini umpe silaha adui yako? Fanya fitina yoyote kadiri unavyoweza kuhakikisha kuhakikisha adui yako hachukui silaha kutoka kwako. Acha akachukue kwingine.

Unapompa adui yako silaha unafanya mambo mawili. Kwanza unampa nguvu, halafu unajiondolea nguvu. Hiki ndicho ilichokifanya Azam wakati iliporuhusu mastaa wake wanne, John Bocco, Aishi Manula, Shomari Kapombe na Erasto Nyoni kwenda Simba.

Aliyewadhuru zaidi ni Bocco. Kule Msimbazi Bocco amefunga mabao 14 katika ligi mpaka sasa. Na kama ilivyo kwa Van Persie, Bocco yuko njiani akienda kuwapa ubingwa watoto wa Msimbazi. Mabao yake na ya staa mwingine, Emmanuel Okwi ni chanzo kikubwa cha ubingwa Msimbazi.

Kama tuliwahi kuwalaumu Simba kwa kumuachia Amiss Tambwe aende Yanga ambako aliwapa mafanikio katika ligi na michuano mingine, kwanini tusiwalaumu Azam kwa kuipa Simba Bocco bure bure kabisa? Lazima tufanye hivi. Kwanza unawapongeza Simba kwa kumuamini Bocco, halafu hapo hapo unawacheka Azam kwa kuhamishia mabao Msimbazi.

Wafungaji bora wa Azam katika Ligi Kuu msimu huu, Mbaraka Yusuph na Yahaya Zayed kila mmoja ana mabao manne. Ina maana wote wana mabao manane. Ni karibu ya nusu tu ya mabao ambao Bocco amefunga pale Msimbazi.

Nina uhakika matajiri wa Azam walijaribu kudanganywa kuja na falsafa mpya ya soka katika klabu yao ya kuamini zaidi vijana. Hata hivyo, kuna maeneo ambayo unaweza kuamini vijana lakini kamwe hauwezi kuyatoa mabao yako kwenda kwa adui.

Pamoja na kutamani falsafa hii, lakini ni wazi Azam ilikuwa inautaka ubingwa. Hauwezi kuutaka ubingwa kwa kuachana na Kapombe, Bocco, Nyoni na Manula ndani ya dirisha moja la usajili. Ni makosa. Wangeweza kupishana lakini sio kuwapeleka Simba katika dirisha moja.

Bahati nzuri Simba haijafanya makosa na wachezaji hawa. Wote wanacheza katika kikosi cha kwanza. Wote wamekuwa nguzo katika mbio hizi za ubingwa. Kapombe aliumia kwa muda mrefu lakini amerudi akiwa imara zaidi.

Msimu uliopita Simba ilikuwa imejaza wachezaji wengi wavulana.

Msimu huu imechukua wachezaji wengi wanaume na katikati hao wanne wametoka Azam huku Azam yenyewe ikijaribu kuamini wavulana katika safari yao ya mafanikio.

Duniani kote katika timu kubwa mpira unachezwa na wanaume. Arsene Wenger alijaribu kupambana na falsafa ya vijana lakini alichemsha. Dunia ya soka ya leo ipo kwa ajili ya wachezaji ambao wapo tayari. Wavulana wanaweza kupelekwa kwa mkopo kwingineko mpaka wakiwa tayari.

Unapoachana na Van Persie na kumpeleka Manchester United huku ukitazamia nafasi yake izibwe vema na Yaya Sanogo huku ni kujidanganya tu. Walau Sanogo angekwenda kwingine na kufunga mabao 15 ya ligi kabla ya kuaminiwa kupewa nafasi klabuni.

Kijana aliye tayari ni yule mwenye tabia za kiume ambaye ameipambania nafasi yake katika mazoezi kisha kumng’oa kigogo mwenye namba yake. Vijana wa siku hizi tunajaribu kuwapa nafasi mezani bila ya kuthibitisha uwezo wao.

Alipaswa kutokea kijana wa kufunga mabao 15 ya ligi ndani ya msimu mmoja katika jezi ya Azam ndipo unaweza kumruhusu Bocco kuondoka na kuhamia mtaa wa wapinzani.

Vinginevyo ni kujidanganya tu kuwa unaweza kufanya maajabu ya kuhamisha mabao ya Bocco kupeleka Msimbazi na bado ukapambana na timu yake kuwania ubingwa.

Endapo Bocco atamalizia kazi kwa kuipa Simba ubingwa, basi mkasa wake utanikumbusha Van Persie.

Mpaka leo mashabiki wa Arsenal hawajaacha kuulaumu uongozi wa Wenger kwa kuipa silaha Manchester United ambayo ilikwenda kutwaa ubingwa wa England na mshambuliaji huyo wa Kidachi.

Pauni 24 milioni ambazo Sir Alex Ferguson alitumia kumnunua Van Persie zilirudi hapohapo mwishoni mwa msimu.