Simba itamtimua Lechantre kwa sababu za kimpira

Muktasari:

Habari za ndani zinadai kuwa kocha huyo analipwa mshahara wa kiasi cha Sh30 milioni kwa mwezi.

KITI kimeanza kuwa cha moto kwa Kocha Pierre Lechantre ndani ya kikosi cha Simba licha ya kuiwezesha kutwaa Ubingwa wa Ligi Kuu msimu huu.

Inasemekana sababu hasa za Simba kutaka kuachana na kocha huyo baada ya mkataba wake wa miezi sita kumalizika ni gharama kubwa ambayo mabingwa hao wa Ligi Kuu wanatumia katika kumhudumia kila mwezi.

Anaishi kwenye moja ya hoteli za kifahari jijini Dar es Salaam ambayo gharama za kulala usiku mmoja ni zinakaribia kulingana na mshahara wa mwalimu wa chekechea. Kocha huyo katika safari zake zote anatumia daraja la kwanza la usafiri wa ndege, akilipiwa pia na klabu hiyo lakini pia analipwa kiasi kikubwa cha mshahara na posho pengine kuliko makocha wote waliowahi kuifundisha timu hiyo.

Habari za ndani zinadai kuwa kocha huyo analipwa mshahara wa kiasi cha Sh30 milioni kwa mwezi.

Kwa uhalisia ni gharama za kawaida ambazo ilikuwa ni lazima Simba ikutane nazo kwa kumhudumia kocha mwenye jina na heshima kubwa kama Lechantre.

Unapata wapi ujasiri wa kutotumia gharama kubwa kiasi hicho kumhudumia kocha kama Lechantre ambaye nyumbani kwake ana medali ya dhahabu ya ubingwa wa Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) ambayo aliipata akiwa na Cameroon kama kocha mkuu mwaka 2000?

Hata hivyo, ukiweka kando suala hilo la gharama, bado Simba itakuwa na sababu za kiufundi ambazo inaweza kujitetea nazo iwapo itaamua kuachana na Lechantre.

Tangu alivyokamata rasmi mamlaka ya kusimamia benchi la ufundi la Simba, Mfaransa huyo anaonekana kuhusudu zaidi soka la kujilinda tofauti na kile ambacho timu hiyo ilikitegemea kutoka kwake. Hapa alikuwa anajikaanga kwa mafuta yake mwenyewe kwa sababu aliikuta Simba ambayo ilikuwa inafurahia soka safi la kushambulia kutoka kwa Masoud Djuma ambaye akikaimu kwa muda nafasi ya ukocha mkuu baada ya Joseph Omog kutimuliwa.

Ingawa Lechantre aliamua kuendelea na mfumo wa 3-5-2 ambao Djuma aliutambulisha kwenye timu hiyo, alionekana kuwa mwoga zaidi kwa kujaza idadi kubwa ya wachezaji ambao kiasili wana uwezo mkubwa katika kujilinda. Hii ilikuwa tofauti na Djuma ambaye alianza na kiungo mmoja tu wa ukabaji ambaye ni Jonas Mkude huku akitumia idadi ya viungo washambuliaji kama Said Ndemla na Mzamiru Yassin ambao waliifanya Simba kutengeneza idadi kubwa ya nafasi za mabao na kupata mabao mengi kwenye mechi zake. Lechantre alichokifanya ni kumchukua Shomary Kapombe na kumuweka nyuma ya washambuliaji wawili mahiri wa Simba msimu huu, John Bocco na Emmanuel Okwi akiamini Kapombe atasaidia zaidi katika kutengeneza balansi ya timu katika kujilinda.

Hapa alifanikiwa kuifanya Simba kuwa imara kwenye safu yake ya ulinzi lakini kwa kiasi kikubwa ilikosa ubunifu mbele na kwa asilimia kubwa ilitegemea uwezo binafsi wa Okwi na Bocco kuamua mechi kwani haikuwa inatengeneza nafasi nzuri kwenda kwa washambuliaji hao.

Inawezekana Lechantre hakufahamu pamoja na kuwa alikuwa akipata matokeo, mbinu ya kujilinda haikuwa inawafurahisha Wana Simba na ndio ilichangia hata kuondoka kwa mtangulizi wake, Joseph Omog.

Simba na Yanga zinaweza kutwaa ubingwa huo bila hata kuwa na kocha anayeeleweka na pia kigezo cha kuchukua ubingwa hakijawahi kuwa kikwazo kwao katika kuachana na makocha.

Milovan Cirkovic, Sam Timbe, Ernie Brandts na hata marehemu James Siang’a waliwahi kukutana na rungu la kutimuliwa licha kuziongoza Simba na Yanga kutwaa ubingwa. Lakini kingine ambacho Lechantre ameonekana kushindwa kukifanya tofauti na msaidizi wake, Masoud Djuma ni kile cha kutoa nafasi ya kucheza kwa kundi kubwa la nyota wa kikosi chake.

Lechantre alionekana kama amekariri kikosi kilekile siku zote na hata zile mechi ambazo zilionekana ni za kawaida, bado alishindwa kuwaamini nyota wengine kikosini. Ilikuwa tofauti na Djuma ambaye alijitahidi kutoa nafasi kwa kundi kubwa la nyota wake na bado Simba ilipata matokeo. Upande ambao Lechantre anaonekana kufanikiwa zaidi ni ule wa nidhamu ambao ameonekana amemudu vilivyo kuimarisha nidhamu ya wachezaji wa Simba tofauti na ilivyokuwa siku za nyuma. Hata hivyo, kwa kocha mwenye jina, heshima na thamani kubwa kama yeye kuliko wengine waliopo nchini kwa sasa, mafanikio yake hayakupaswa kuishia kwenye nidhamu pekee.

Matarajio ya Wana Simba na wadau wa soka kwake yalikuwa ni kuona akiifanya Simba kuwa tishio katika mechi za mashindano ya ndani na nje ya nchi huku ikicheza soka la kuvutia.

Unaweza kumuelewa Lechantre kama Simba ikicheza kwa kujilinda dhidi ya Al-Masry, Difaa Jadida au Mamelodi Sundowns, lakini ni vigumu kwa kocha kuwaaminisha watu kuwa Simba inapaswa kupaki basi dhidi ya timu kama Ndanda FC tena ikicheza kwenye uwanja wake wa nyumbani wa Taifa.