HISIA ZANGU: Simba Day ni kama shoo za Diamond Platinumz tu

MASHABIKI wanaosogea Uwanja wa Taifa kuitazama Simba wanakuwa na hamu ya kuiona timu yao kama mashabiki wa Mwanamuziki wa Kizazi kipya, Diamond Platinumz. Kuna mfanano fulani hivi ambao ni rahisi kuugundua.

Simba wanaifanya timu yao kuwa na thamani. Wanaijengea thamani. Mara nyingi wanasafiri kidogo na kutoweka machoni mwa mashabiki wao. Inawaisaidia. Kinachobakia hapo ni matangazo mengi ya siku yenyewe. Mashabiki wanapatwa na shauku.

Hata katika misimu minne mfululizo ambayo Simba ilifanya vibaya kwa mujibu wa viwango walivyojiwekea huku Yanga na Azam FC wakitawala, bado Simba Day ilikuwa siku nzuri kwa shabiki kwenda kuwatazama. Waliitengeneza siku iwe na mbwembwe.

Diamond wa zamani sio wa leo. Ameacha maisha yake ya Kiswahili ameingia katika maisha ya kimuziki ya kistaa. Anajua jinsi ya kucheza na wateja wake. Haumwoni Diamond kirahisi mpaka uende katika shoo zake. Anatembea na baunsa, anaposti maendeleo yake mitandaoni, haumkuti sehemu za starehe.

Matokeo yake ukitaka kumwona Diamond inabidi ulipe kwenda kumtazama katika shoo zake. Ametengeneza ukubwa wa jina lake kwa makusudi tu. Anataka umsikie kila siku lakini usimwone mpaka uende katika kazi yake.

Simba huwa wanatengeneza mazingira haya wakati ikikaribia Siku ya Simba Day. Popote wanakopotelea huwa wanakwenda kutengeneza mazingira wana timu mpya, wamejifua, wana maisha mapya tofauti na yale ya msimu uliopita. Mashabiki wanajaa hamu na wanatiririka uwanjani kuitazama timu yao.

Hivi ndivyo soka letu inavyobidi liwe kwa wakati wote. Bahati mbaya hatuna weledi wa namna hii wakati wote. Kwa mfano, muda si mrefu wachezaji wa Simba hawatakuwa bidhaa adimu yetu. Utawaona kina Shiza Kichuya wakizurura ovyo mitaani.

Utaona wachezaji wetu wakilikacha basi la timu na kudai wamepewa ruhusa na uongozi kwa ajili ya kwenda kumsalimia mama.

Hapo ndio unakuta anaondoka na bodaboda uwanjani na kila shabiki anamfikia kwa urahisi.

Miundo ya viwanja vyetu siyo rafiki kuwafanya wachezaji na timu kwa jumla iwe bidhaa adimu. Timu inaonekana wakati inashuka katika basi. Komandoo au shabiki wa kawaida anaweza kumsimamisha mchezaji akapiga naye stori moja ya haraka haraka.

Kwa wenzetu hali sio hii. Wachezaji ni bidhaa adimu katika makazi yao, kisha katika muundo wa kuingia na kuondoka uwanjani. Siku ukiambiwa unapewa zawadi ya kupiga picha na Emmanuel Okwi unaamini umepewa fursa ya kufanya kitu adimu.

Kwa sasa Simba wakiendesha zoezi ambalo zawadi yake ni kupiga picha na Emmanuel Okwi sidhani kama watu wengi watalipapatikia hilo shindano kwa sababu katika maisha ya kawaida wengi wanaweza kunusa na kujua wapi Okwi anapatikana.

Tatizo jingine kubwa ambalo limekuwa ni utamaduni wa kijinga wa soka letu ni kuruhusu mashabiki kutazama mazoezi ya klabu zao kila siku.

Wazungu wana siku moja tu maandalizi ya msimu mpya ambapo wanaruhusu mashabiki waende uwanjani kutazama mazoezi ya timu yao.

Siku nyingine zote ni siri. Unawafundishaje wachezaji mbinu huku uwanja ukiwa umejaa mashabiki ambao ndani yao kunaweza kuwa na mashushushu wa timu pinzani? Lakini achilia hilo kuna mambo mengi kando yake.

Kwa kufanya hivyo wanashusha presha ya kocha katika upangaji wa kikosi. Ni rahisi kwa mashabiki kumshinikiza kocha ampange fulani na fulani kwa sababu wanaona viwango vyao katika mazoezi hadi katika mechi.

Hata hivyo, kubwa zaidi ni hili la kulinda thamani ya wachezaji wenyewe. Shabiki mwenye uhakika wa kuwaona wachezaji mazoezini hana hamu ya kuwatazama sana wachezaji hao katika mechi.

Zamani tulikuwa tunafanya hivi kwa sababu ya kutafuta pesa za viingilio, lakini huo ni mfumo ambao umepitwa na wakati.

Kwa mfano, mashabiki wengi wa Simba wanaamini wataona mambo mengi mapya katika kikosi hiki hata kama walikitazama kikosi chao katika mechi za SportPesa na Kagame. Kisa? Kwa sababu timu imeondoka katika macho yao na hawana uwezo hata wa kuiona mazoezini.

Tuanze kutafakari upya weledi wa soka letu. Tuzitunze njaa zetu kidogo kwa ajili ya kutengeneza ughali wa soka letu. Ndicho alichofanya Diamond Platinumz kwa ajili ya kutunza ukubwa wa jina lake. Ameficha kila ubaya wake kwa kutoonekana hadharani mara kwa mara kwa ajili ya kuhakikisha mashabiki wanakuwa na hamu naye. Ndivyo ilivyo wakati mwingine.

Kuanzia mchezaji mmoja mmoja hadi timu kwa jumla tunapaswa kuwa na weledi huu. Zamani kuna wachezaji mahiri walikuwa hawachezi mechi za mitaani zilizokuwa zinajulikana kama ndondo. Usingeweza kuwaona kina Sekilojo Chambua, Hussein Marsha au George Masatu wakicheza mechi hizo. Leo kuna wachezaji wa timu ya taifa wanacheza mechi hizo. Nani atakuwa na hamu ya kwenda kuwatazama.

Tubadilike.