Sarri atahitaji muda Chelsea

MSIMU mpya wa soka umeanza, ambapo kwa hapa London palikuwapo mechi kubwa ya kufungua pazia lenyewe baina ya Chelsea na Manchester City ambao ni mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya England (EPL).

Wakati Man City wakianza msimu wakiwa na nguvu ya kikosi kile kile cha msimu uliopita na kocha wao Pep Guardiola, Chelsea wanaanzia kwa tabu kidogo kwa sababu bado hawajaimarisha kikosi lakini pia wamebadilisha kocha. Ajabu ni kwamba walishindwa kujipanga mapema, wakamfukuza Antonio Conte wakati maandalizi ya msimu mpya yakiwa ndio yanaanza, hiyo ikimaanisha kwamba kwa ujumla wote – wachezaji na benchi la ufundi walikuwa juu juu. Conte ameondoka na malalamiko yake ya tangu mwanzoni mwa msimu uliopita kwamba hakupatiwa wachezaji aliowahitaji na timu ilimaliza katika nafasi ya tano, wakishindwa kufuzu kwa mashindano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya (UCL). Waliachwa mbali sana na City, lakini pia wakazidiwa nguvu na Manchester United, Liverpool na Tottenham Hotspur.

Bosi mpya, Mtaliano pia kama Conte, Maurizio Sarri ameanza kazi huku kukiwapo mshindilio wa mambo mengi, ikiwa ni uhitaji wa wachezaji, kujaribu kushawishi waandamizi kama Thibaut Courtois, Willian na Eden Hazard wasiondoke lakini pia kuijenga timu icheze katika mfumo anaoutaka yeye.

Haya yote yangewezekana iwapo angeingia Stamford Bridge mara tu baada ya EPL kumalizika msimu uliopita. Hata hivyo, uwapo wa fainali za Kombe la Dunia nao uliathiri kwa kiasi fulani, maana baadhi ya wachezaji walikuwa huko hivyo kuhitaji mapumziko.

Iwe iwavyo, Waswahili husema maji ukiyavulia nguo sharti uyaoge na sasa hana la kufanya zaidi ya kushughulika na timu yake, lakini itachukua muda kuweza kutulia kwa sababu bado Chelsea si wazuri na walionesha hivyo kwenye mechi hiyo ya Ngao ya Jamii ambapo walilala 2-0.

Ana kazi kubwa Sarri ya kuwabadilisha Chelsea ili wawe washindani wa kweli wa ubingwa wa England na kufuzu kwa UCL. Alhamisi wiki hii ndio mwisho wa dirisha la usajili kwa hiyo pia hana muda mwingi wa kufanya usajili kama anataka kuongeza wachezaji. Ikiwa wachezaji hao watatu wangebaki, basi Sarri hangekuwa na shida sana, kwa sababu anaweza kuwatumia vyema katika mfumo wake anaoupenda wa 4-3-3.

Sari ana mashimo makubwa anayotakiwa kufukia wiki hii kwa hakika kabla ya mechi yake ya kwanza ya EPL, ikiwa ni pamoja na kuwajenga zaidi wachezaji walioanza kuonesha watakuwa wazuri wakinolewa; mfano Callum Hudson-Odoi kwenye wingi ya kushoto, pengine Hazard akiondoka basi huyu wa umri wa miaka 17 apewe fursa, japokuwa ni ngumu kuenea viatu vya Mbelgiji huyo.

Ni wazi kwamba Courtois, Willian na Hazard ni wa kiwango cha kimataifa, hivyo kupoteza yeyote au hata wawili ni pigo. Kinachofanya mambo kuwa magumu zaidi ni kwamba klabu kubwa kwingineko Ulaya, tofauti na England, zinaweza kuendelea na usajili hadi mwisho wa mwezi huu wakati England wanachoweza ni kuuza tu. Kwa msingi huo klabu kubwa za Ujerumani, Hispania, Italia, Ufaransa na kwingineko wanaweza kuendelea na ushawishi kwa wachezaji hawa, maana yake ni kwamba hali itabaki kuwa tete Stamford Bridge hata baada ya kuanza kwa ligi kuu, wakiwa na hofu ya kupoteza wachezaji wao, kama hawatakuwa wamewapoteza tayari.

Kwenye ushambuliaji kuna walakini; bado waliopo si wa uhakika sana, kama ilivyokuwa msimu uliopita licha ya ongezo la Olivier Giroud kutoka Arsenal Januari na uwapo wa Alvaro Morata aliyekuwa si mzuri msimu uliopita.

Giroud alifanya vyema kwenye fainali za Kombe la Dunia na kutwaa ubingwa na Ufaransa, labda atafanya hivyo katika ngazi ya klabu akipewa nafasi. Anaweza kuanza msimu kwa kujiamini sana na akiwa hivyo nadhani Sarri atampa nafasi ya kuwa mshambuliaji kiongozi japokuwa hakufunga bao lolote Urusi.

Katika ulinzi kuna kazi kubwa ya kufanya, kwa sababu Sarri anataka kutumia walinzi wanne badala ya watatu. Kwa kutumia mfumo huo, anaacha maswali pia juu ya David Luiz ambaye huwa si mzuri kama beki nne zinatumika; anafaa zaidi kwenye tatu. Chelsea walipomsajili kwa mara ya pili, alikuwa na msimu mzuri wa 2016/17 chini ya Conte lakini ulikuwa mfumo wa 3-4-3. Kwa msingi huo anao Luiz, Antonio Rudiger, Gary Cahil na Andreas Christensen. Si wote wanaweza kuwa na ushirika mzuri uwanjani, hivyo lazima Sarri ajue nani na nani wanafiti. Bado tukizungumzia kwenye ukuta, kuna hilo tatizo la kipa ambapo wakala wa Courtois ameshasema anataka kwenda Real Madrid.

Sarri alionesha kujiamini kwamba Willian hangeondoka, kwamba angezungumza na Courtois baada ya Jumatatu wiki hii, lakini akasema anataka kubaki na wachezaji wenye nia ya kweli ya kucheza chini yake na si kuwalazimisha. Chelsea wamemsajili kipa wa zamani wa kimataifa wa England, Robert Green, 38. Sari atatakiwa apate ufumbuzi wa haya wiki hii, na kama atamuuza, ni wazi atapata fedha nyingi ambazo huenda ikamlazimu kununua kipa mwingine, lakini ni yupi katika dakika hizi za mwisho? Imemchukua Pep miaka miwili kuwa na timu bora, je, Sarri itamchukua muda gani au ataruka kwenye meli?