Michongo yote ya fedha NDO ipo hivi!

Muktasari:

Leo katika muendelezo wa chapisho la Katiba hiyo tunaangazia masuala ya fedha na mapato ya klabu hiyo. Haya ndio masuala nyeti kabisa kwenye taasisi yoyote, je mchongo mzima ukoje ndani ya Simba? Endelea nayo...!

KATIKA mfululizo wa chapisho la Katiba Mpya ya Simba ya mwaka 2018, jana Jumatatu tuliona katiba hiyo ilivyoainisha sifa za wanachama wa matawi ya klabu hiyo na muundo wake kuanzia wilayani hadi mkoani.

Pia, imefafanua ni mambo gani yanayoweza kumnyima sifa za mwanachama kuendelea kutambuliwa na tawi lake na hata klabu nzima ya Simba.

Leo katika muendelezo wa chapisho la Katiba hiyo tunaangazia masuala ya fedha na mapato ya klabu hiyo. Haya ndio masuala nyeti kabisa kwenye taasisi yoyote, je mchongo mzima ukoje ndani ya Simba? Endelea nayo...!

SEHEMU YA IV: FEDHA

Ibara ya 41: Mwaka wa Fedha wa Simba Sports Club utaanza na utaendana na Mwaka wa Fedha wa Simba Sports Club Company Limited.

IBARA YA 42: Simba Sports Club itapata ruzuku ya kuendesha shughuli zake kutoka Simba Sports Club Company Limited.

IBARA YA 43: Matumizi Simba Sports Club itakuwa na matumizi yafuatayo;

1. Matumizi yaliyotajwa katika bajeti

2. Matumizi mengine yaliyothibitishwa na Mkutano Mkuu na yale ambayo Bodi ya Wakurugenzi inastahiki kufanya ndani ya eneo la mamlaka yake.

3. Matumizi mengine yote kulingana na mipango na malengo ya Simba Sports Club.

SEHEMU YA V: MIPANGO BINAFSI

IBARA YA 44: Sheria za Michezo wa Mpira wa Miguu

Simba Sports Club itajiendesha kwa mujibu wa Sheria na kanuni za mchezo wa mpira wa miguu zilizotangazwa rasmi na IFAB na Vyama vya mpira TFF, CAF na FIFA.

IBARA YA 45: Mwenendo wa Viongozi na vyombo wa klabu Vyombo na viongozi wa Simba Sports Club lazima wafuate Katiba ya Simba Sports Club, Uamuzi na Kanuni za Maadili za Simba Sports Club Company Limited katika utendaji wa majukumu yao. Bodi ya Wakurugenzi itatayarisha Kanuni za maadili kwa kuzingatia Kanuni za Maadili za TFF.

IBARA YA 46: Kufukuza uanachama

1. Bodi ya Wakurugenzi ndiyo yenye mamlaka ya kupeleka ajenda ya kufukuzwa uanachama kwenye vyombo vya haki (Kamati ya Nidhamu au Kamati ya Maadili).

2. Vyombo vya Haki vitampa mwanachama ambaye hoja ya kufukuzwa imepelekwa na Bodi ya Wakurugenzi nafasi ya kusikilizwa kwa kutumia kanuni zinazosimamia vyombo hivyo vya haki.

3. Mwanachama atakayefukuzwa lazima avuliwe majukumu yake mara moja.

IBARA YA 47: Migogoro ya Kisheria

Hairuhusiwi kutafuta msaada katika mahakama za kawaida za sheria dhidi ya maamuzi yaliyochukuliwa na vyombo vya Simba Sports Club na Simba Sports Club Company Limited. Maamuzi ya aina hiyo hayana budi kuwasilishwa katika vyombo vya haki kwa mujibu wa Katiba ya Simba, TFF na FIFA. Ukiukwaji wa kanuni hii utasababisha kufukuzwa uanachama kutoka Simba Sports Club.

IBARA YA 48: Leseni kwa Vilabu (Club Licensing)

Simba Sports Club itafuata utaratibu wa TFF, CAF na FIFA juu ya utoaji wa leseni za klabu (Club Licensing System).

SEHEMU YA VI:

MASHARTI YA MUDA NA MWISHO

IBARA YA 49: Mipango ya Utendaji

Bodi ya Wakurugenzi itahakikisha kuwa Katiba inatumika na itapitisha mipango ya utendaji inayotakiwa kwa ajili ya kutumika.

IBARA YA 50: Masuala yasiyoelezwa katika Katiba

Suala lolote lisiloelezwa katika Katiba hii au kwa mambo yasiyozuilika lazima yashughulikiwe na Bodi ya Wakurugenzi. Hakuna Rufaa itakayokatwa dhidi ya maamuzi yatakayotolewa na Bodi ya Wakurugenzi.

IBARA YA 51: Masharti ya kutoa huduma katika kipindi cha mpito

Jambo lolote litakalofanyika kabla na wakati wa kuanza kutumika kwa Katiba hii kuhusu kazi yoyote au jambo linaloweza kufanyika kwa mujibu wa Katiba hii litahesabiwa limefanyika kihalali kwa mujibu au kufuatana na Katiba.

IBARA YA 52: Kupitishwa na tarehe ya kuanza kutumika

Katiba hii imepitishwa katika Mkutano wa Katiba ya Simba Sports Club tarehe 20/05/2018.

Si unajua ishu za kutimuana ndani ya Simba na klabu zingine ikiwemo Yanga, sasa unazijua kanuni za Mkutano Mkuu wa Simba na mwanachama anayezingua mkutano unaweza kumchukulia hatua gani za kinidhamu. Na huyu mwanachama akitaka kukata rufani ni hatua gani za kufuata ili kuhakikisha anapata haki yake? Majibu yapo katika hitimisho la mfululizo wa chapisho hili. Fuatilia sehemu hii muhimu kabisa Alhamisi.