Maajabu ya Sergio Kun Aguero katika jezi ya Man City

MIGUU ina maajabu ambayo Manchester City haikuwahi kuiona kwa mchezaji yeyote aliyewahi kuvaa jezi yake kabla ya hapo. Sergio Aguero Kun juzi alifunga mabao mawili katika pambano la ufunguzi wa msimu dhidi ya Chelsea. Mabao hayo yamekuja na maajabu yake.

Bao lake la kwanza lilikuwa la 200 katika historia yake na Man City. Bao lake la pili lilikuwa la 201. Kwa jumla, Aguero ambaye ni staa wa kimataifa wa Argentina anakuwa mchezaji wa kwanza katika historia kufunga mabao 200 klabuni hapo. Hakuna aliyewahi kufanya hivyo.

Aguero, 30, alijiunga na City mwaka 2011 akitokea Atletico Madrid ya Hispania na katika kila msimu amekuwa akitisha kwa kufunga mabao. Huu utakuwa msimu wake wa nane na kwa misimu yake misimu yake saba iliyopita Aguero amefunga mabao 23, 12, 17, 26, 24, 20 na 21 katika ligi.

Novemba mwaka jana, Aguero alivunja rekodi ya miaka mingi iliyowekwa na staa wa zamani wa City, Eric Brook ambaye alikuwa anaongoza kwa kufunga mabao mengi zaidi katika historia ya klabu hiyo pinzani ya Manchester United.

Brook alifunga mabao 177 lakini wakati Aguero alipofunga bao katika ushindi wa mabao 4-2 dhidi ya Napoli katika michuano ya Ligi ya Mabingwa wa Ulaya, alikuwa ameifikia rekodi ya mkongwe huyo aliyefariki mwaka 1965 na kuacha rekodi hiyo imara kwa miaka 78.

Baada ya kuivunja rekodi hiyo, Aguero alianza kazi ya kuifukuzia rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza kufunga mabao 200 klabuni hapo. Mbio zake kwa msimu ulioisha zilimalizika kwa kufunga bao la 199 katika pambano la fainali Kombe la Ligi dhidi ya Arsenal Februari 25.

Mabao yake mawili aliyofunga dhidi ya Chelsea ni mwendelezo tu wa kuionea timu hiyo ya London ambayo katika rekodi inakuwa timu ya pili kwa kufungwa sana na mshambuliaji huyo mfupi. Timu ya kwanza kwa kufungwa sana na Aguero ni Newcastle iliyofungwa mabao 14.

Timu ya pili ambayo imefungwa mabao mengi na Aguero ni Chelsea ambayo imepigwa mabao 10 baada ya mabao mawili ya juzi. Anaelekea katika msimu mpya akiwa amebakiza mabao saba tu kufunga mabao 150 ya Ligi Kuu.

Kwa jumla katika mabao 201 aliyofunga mpaka sasa kwa City, mabao 147 amefunga kwa mguu wake wa kulia ambao anautumia mara nyingi zaidi wakati mabao 35 tu ndio ambayo ameyafunga kwa kutumia mguu wake wa kushoto.

Aguero ambaye ni mmoja kati ya washambuliaji wafupi duniani amefunga mabao 19 tu kwa kutumia kichwa. Katika idadi ya mabao 201 aliyofunga, mabao 182 ameyafunga akiwa ndani ya boksi la adui wakati mchezaji aliyechangia mabao mengi katika idadi ya mabao ya Aguero ni kiungo wa kimataifa wa Hispania, David Silva ambaye amempikia mabao 19.

Beki wa zamani wa Manchester United na Timu ya Taifa ya England, Rio Ferdinand amedai muda wowote ule ukimwambia achugue mshambuliaji mmoja katika timu yake kati ya Aguero au Harry Kane, basi angependa kumchagua Aguero.

“Kuifungia Manchester City mabao 22 nadhani ni kitu cha ajabu, na nadhani yeye ndiye mshambuliaji bora zaidi Ligi Kuu ya England. Alikuwa ni mchezaji mgumu ambaye nimewahi kucheza naye, anajua jinsi ya kutoroka, ana kasi na yupo makini,” alisema Ferdinand.

“Ningemchagua yeye kuliko Harry Kane. Ninapozungumzia kuwa ni mchezaji mgumu kucheza naye namaanisha jinsi anavyoweza kutumia miguu yake yote miwili, mwendo wake na kasi vyote vinaleta matatizo. Kane ni mchezaji mzuri, lakini Aguero ana kila kitu,” alisema Ferdinand.

Aguero aliyezaliwa Juni 2, 1988 katika mji mkuu wa Argentina, Buenos Aires, alinunuliwa na City kwa dau la Pauni 38 milioni mwaka 2011 akitokea Atletico Madrid ambayo ndio ambayo ilimleta Ulaya baada ya kumnunua kutoka Argentina katika klabu ya Independiente kwa dau la Euro 20 milioni ambalo lilikuwa rekodi ya uhamisho ya Atletico wakati huo.