INAWEZEKANA: Unapokosea kwenye usajili lazima itakula kwako

MSOMAJI, Sevilla ni timu ambayo katika miaka ya hivi karibuni imepata mafanikio makubwa sana. Walishinda Ligi ya Ulaya maarufu kama Europa League mara tatu mfululizo katika misimu ya 2013/2014—2014/2015 na 2015/2016. Hakika, Sevilla wamekuwa na makocha wazuri kama Unai Emery na Jorge Sampaoli ambao wamekuwa sababu kubwa ya mafanikio ya Sevilla.

Lakini, sababu nyingine ya Sevilla kufanya vizuri katika miaka ya hivi karibuni ni mwenyekiti wao wa usajili wa zamani Monchi.

Tangu Monchi alipopewa cheo cha mwenyekiti wa usajili katika klabu ya Sevilla mwaka 2000 timu hiyo iliweza kusajili wachezaji wengi wenye kiwango kikubwa kwa bei nafuu na kuwauza kwa bei kubwa.

Ni wachezaji kama Dani Alves, Adriano, Ivan Rakitic, Alvaro Negredo na Seydou Keita. Bila shaka,

Monchi ana jicho zuri la kusajili wachezaji wenye vipaji vikubwa na ndio maana mashabiki wa AS Roma walifurahi sana Monchi alipotangaza kwamba atakuwa mwenyekiti mpya wa usajili wa timu hiyo mwezi wa nne mwaka jana.

Roma ni klabu ambayo katika misimu ya hivi karibuni imeanza kuwapa Juventus upinzani katika Ligi Kuu ya Italia lakini kabla msimu uliopita walihitaji kusajili wachezaji wapya katika safu ya katikati na safu ya ushambuliaji kama kweli walikuwa na nia ya kupiga hatua kimpira.

Mashabiki wengi wa Roma wamekuwa na matarajio makubwa kwamba Monchi ataweza kusajili wachezaji wazuri na kuifanya timu ya Roma kuwa imara zaidi.

Lakini, katika dirisha kubwa la uhamisho mwaka jana Roma pamoja na Monchi waliamua kumuuza winga wa timu hiyo Mohamed Salah kwa klabu ya Liverpool.

Na bila shaka, ni wazi kwamba uamuzi wa Monchi haukuwa sahihi kwa kuwa Salah aliendelea zaidi kimpira msimu uliopita na amekuwa kati ya wachezaji bora zaidi barani Ulaya.

Hata hivyo, ni muhimu kukumbuka kwamba ilikuwa lazima kwa Monchi kumuuza mchezaji kama Salah kutokana na madeni makubwa ya Roma na mshahara mkubwa wa mchezaji huyu.

Hata kama Monchi alikuwa na bajeti ndogo kusajili wachezaji katika dirisha kubwa la uhamisho mwaka jana, alisajili wachezaji wenye umri mdogo kama Schick, Fazio na Juan Jesus ambao wote walikuwa wachezaji muhimu sana katika mafanikio ya Roma katika Ligi ya Mabingwa msimu uliopita.

Katika dirisha hili la uhamisho Monchi alilazimika kumuuza kipa na nyota wa AS Roma, Allison Becker.

Lakini, kwa mtazamo wangu uamuzi wa Monchi kumsajili kipa wa timu ya taifa wa Sweden, Robin Olsen ni uamuzi mzuri kwa kuwa kipa huyu alikuwa kati ya makipa bora zaidi katika Kombe la Dunia na bado alisajiliwa kwa bei nafuu.

Pia Monchi amesajili wachezaji katika dirisha hili wenye vipaji vikubwa na uwezo wa kuendelea kimpira. Ni wachezaji kama Justin Kluivert ambaye ana miaka 19 na Ante Coric ambaye ana miaka 21.

Wakati Juventus wamesajili wachezaji wakubwa katika dirisha hili la uhamisho kama Cristiano Ronaldo, Roma wanajaribu kusajili wachezaji wenye uwezo wa kuendelea kimpira na kuwa kati ya wachezaji bora zaidi duniani ndani ya misimu michache.

Ni mikakati ambayo huenda haitawapa Roma ubingwa katika Ligi Kuu ya Italia msimu ujao lakini naamini kwamba tutaona matunda ya mipango ya Monchi katika miaka ijayo.