Hongera Yanga, mjipange kwa hatua ya makundi sasa

Muktasari:

  • Hakika ni jambo linalostahili pongezi kubwa kwani siyo kazi rahisi kufika hatua ya makundi ya michuano hiyo ya pili kwa ukubwa hapa Afrika.

HATIMAYE wawakilishi pekee wa Tanzania kwenye mashindano ya Kimataifa, Yanga wameweka historia mpya ya kufuzu kwa mara nyingine kwenye hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Hakika ni jambo linalostahili pongezi kubwa kwani siyo kazi rahisi kufika hatua ya makundi ya michuano hiyo ya pili kwa ukubwa hapa Afrika.

Hakuna ubishi kuwa Yanga ilisimama na kupambana kiume licha ya changamoto nyingi zilizokuwa zikiwazunguka hasa ukata pamoja na majeruhi ya mara kwa mara ya mastaa wake.

Kutokana na ufinyu wa bajeti yake, Yanga ilicheza huku wachezaji wake pamoja na mastaa wengine wakiwa hawajalipwa mishahara yao ya miezi kadhaa.

Ilifikia hatua mbaya ya aliyekuwa kocha wao, George Lwandamina kuwakimbia, jambo ambalo liliwaongezea msongo wa mawazo hasa katika wakati ambao walikuwa wakikabiliwa na mchezo mgumu wa marudiano dhidi ya Welaytta Dicha ya Ethiopia.

Yanga ilizichanga karata zake vyema hapa nyumbani ikishinda kwa mabao 2-0 jambo ambalo lilipunguza presha ya mchezo wa marudiano ambao walifungwa bao 1-0 hivyo kufanya matokeo ya jumla kuwa 2-1.

Hakuna ubishi kuwa Yanga imeanza kuwa na uzoefu wa mashindano hayo kwani pamoja na changamoto hizo imefanya jambo ambalo limezishinda timu nyingine nyingi tu Afrika.

Tunapenda kutumia fursa hii kuwapongeza Yanga kwa kupeperusha viruzi bendera ya Tanzania ambapo sasa watakabiliwa na changamoto nyingine ya kufanya vizuri kwenye hatua ya makundi.

Tunawakumbusha Yanga kuwa safari ndio kwanza imeanza na hiki walichokifanya sasa ni sehemu ndogo tu ya kazi kubwa ambayo wanapaswa kuifanya ili kufika mbali zaidi.

Yanga sasa inakabiliwa na mechi sita ngumu za hatua ya makundi ambazo inapaswa kuzicheza vizuri ili kupata tiketi ya robo fainali.

Wakati huu tukisubiri droo ya hatua ya makundi ambayo itapangwa kesho Jumamosi, ni vizuri tukawakumbusha Yanga juu ya umuhimu wa maandalizi ya mechi zinazofuata ili iweze kufika mbali.

Kumekuwa na kasumba ya timu za Tanzania kuridhika na mafanikio ya kufika hatua ya makundi hivyo kusahau kabisa kuwa kuna safari nyingine mbele ambayo wanapaswa kuipigania.

Yanga inapaswa kufahamu kuwa sasa zile mechi za mtoano zimekwisha na inapaswa kucheza kwa kukusanya pointi kwenye hatua ya makundi ili kuwa kwenye nafasi nzuri ya kutinga robo fainali.

Mechi ya hatua ya makundi ni tofauti kabisa na zile za mtoano kwani mabao yana sehemu ndogo, kinachopaswa ni kutazama zaidi alama zinazopatikana ili kuwa nazo za kuweza kusonga mbele.

Yanga inapaswa kucheza vizuri mechi zake za nyumbani na pia za ugenini ili kukusanya pointi nyingi ambazo zinaweza kuwafikisha kwenye hatua hiyo inayofuata.

Tusingependa kuona makosa kama yale ya mwaka juzi yakijirudia tena mwaka huu.

Mwaka juzi Yanga ilifuzu hatua ya makundi ya michuano hiyo lakini ilimaliza ikiwa mkiani baada ya kushindwa kucheza vizuri mechi zake.

Mwaka 2003 Simba ilifika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika na kumaliza katika nafasi ya tatu ambayo haikuwa na faida yoyote kwao.

Vivo hivyo kwa Yanga iliyomaliza tena mkiani mwa kundi lao mwaka 1998 na mwaka huo wa 2016.

Tungependa kuona mageuzi makubwa yakifanyika kwa mwaka huu na Yanga ikicheza kwa ushindani mkubwa ili kusonga mbela zaidi katika michuano hiyo.

Yote kwa yote tunapenda kuitakia mema Yanga katika mechi zilizosalia ili iweze kuwa na nyota njema kwa Watanzania na kufungua milango zaidi ya kufanya vizuri kwenye michuano hiyo katika siku zijazo.

Tunaamini kuwa kitakachofanywa na Yanga mwaka huu kinaweza kuwa sehemu kubwa ya mageuzi ya soka letu ambalo limeanza kuonyesha mwelekeo katika siku za karibuni.

Huu ni wakati wachezaji wenyewe kujipanga na kuonyesha kuwa hawakubahatisha kuingia hatua ya makundi na walistahili.

Kucheza kwa kujituma na zaidi fedha zilizopatikana, zikiongezwa na za nusu fainali, shida zitasahaulika tu.