Yaani bila kujipodoa hawatoki ndani

Muktasari:

  • Ila wapo pia mastaa wanaopenda kutumia mekapu hata katika matembezi yao ya kawaida, yaani bila kujisiriba hayo mambo hujiona hawapo poa.

IMEKUWA kawaida kwa mastaa wetu pindi wanapokuwa katika harakati za upigaji picha za filamu au masuala ya muziki hupenda kutumia mekapu (make up) ili kuwapa mvuto ulio tofauti na uhalisi wa sura au mwonekano wao uliozoeleka.

Ila wapo pia mastaa wanaopenda kutumia mekapu hata katika matembezi yao ya kawaida, yaani bila kujisiriba hayo mambo hujiona hawapo poa.

Mekapu inawafanya kuonekana vizuri na kwa jinsi walivyojizoesha hivyo, hata siku itokee hawajapaka hiyo kitu na kutembea mitaani kisha akaonwa na mashabiki wake wakati mwingine huwa gumzo na kugeuzwa kituko.

Mwanaspoti linakuletea baadhi ya mastaa wa kike wanaopenda kutumia mekapu katika matembezi yao na wenyewe kufichua kwa nini wanapenda kufanya hivyo.

JOKATE MWEGELO

Mwanamitindo huyu maarufu nchini anatajwa kuwa staa mwenye mvuto zaidi, lakini ni kama vile haamini mwonekane wake wa urembo mpaka afanye mekapu.

“Yaa, mekapu inamfanya mtu aonekane na sura nzuri laini na yenye mvuto, nami napenda kwa sababu napenda urembo na hiyo ni moja ya urembo wa ngozi ya mwanamke.”

HAMISA MOBETO

Mwanamitindo huyu mwingine aliye pia mwigizaji wa filamu anatajwa kuwa na mvuto na uzuri wa asili, ila inasemekana uzuri wake wa asili ndio unaompa jeuri mjini, huku ukimpa dili kibao za filamu na matangazo mbalimbali.

Lakini bado hajiamini hadi ajiongezee kupaka mekapu usoni ndio anajiona anakuwa na sura ya mvuto zaidi.

“Mie napaka mekapu kama kuweka sura yangu iwe na mvuto na sio kwanza bila mekapu sura yangu inatisha, ila siwezi kutoka bila make up kwa kweli napenda sana urembo na mekapu naziuza mwenyewe,” anasema.

AUNT EZEKIEL

Mara nyingi staa huyu anapenda kuwa na mwonekano wake halisi, ila linapokuja suala la kutoka kwenye katika sherehe huwa anabadilika na kupaka mekapu anayoamini inamweka vizuri sura yake.

“Napenda mekapu kama urembo mwingine, sababu inanifanya ngozi iwe laini na kung’aa, ndiyo maana katika hafla yoyote huwa naanza kujiandaa mapema kupaka mekapu ili kupata yenye rangi yangu.”

WEMA SEPETU

Mara nyingi Wema upendelea zaidi kujikwatua na vipodozi vya gharama, tena anaamini kabisa bila kupaka mekapu katika matembezi yake bado hajaonekana mrembo.

“Mie siwezi ficha, kweli kabisa bila mekapu najiona sijawa Wema, tena sipaki tu nikitaka kutoka bali hata nikiwa nyumbani huwa napenda kupaka bwana!”

JACKQUILINE WOLPER

Achilia mbali staa huyu mwenye mvuto wa aina yake kupendelea kujikwatua mara mara kwa mara, ila yeye bila mekapu bado anaona hajakaa vyema usoni.

“Mimi ni mrembo siku zote, ila napenda mekapu kwa ajili ya kuifanya ngozi yangu kuwa na mvuto, hata nikiwa na kipele ukipaka mekapu inafukia kile kipele na kuonekana softi na huwa napenda kutumia mekapu yenye rangi yangu ili isipishane na ngozi yangu.”

RIYAMA ALLY

Mwigizaji kiwango Bongo, naye anaingia kwenye listi ya wapenda mekapu kwani hata yeye anajiona hajakaa vyema usoni licha ya umri kumtupa mkono bado anaonekana ni mrembo zaidi usoni na mwenye sura ya kitoto (baby face).

“Mekapu hufanya ngozi yako kuwa ya kitoto kila kukicha na ndiyo maana ukitaka kupaka mekapu inabidi uchague ya rangi yako, mie napenda kupaka pindi napotoka katika pati.”

UWOYA

Staa wa filamu nchini, Irene Uwoya naye anaingia katika listi ya wapenda mekapu, anaamini bila make bado hajawa na mvuto.

“Natumia mekapu kuweka sura yangu iwe na mvuto, usaidia sana wasichana hasa ukiwa na sura yako ikiharibika na vipele, pia kuna aina ya mekapu ukitumia inapendezesha zaidi, yaani bila mekapu hunitoi ndani.”

LULU MICHAEL

Akiwa katika umri mdogo tu wa miaka 20, staa wa filamu Bongo, Lulu Michael, anatajwa kuwa ndiye staa mwenye mvuto zaidi kuliko mastaa wenzie.

Kadri siku zilivyokuwa zinaenda mbele nae akajiingiza katika masuala ya kupaka mekapu na alishawahi kusema yeye bila hiyo kitu (make up) hatoki ndani, kwani zinamsaidia kuwa na mwonekano mzuri.