Umeneja wa Diamond inabidi pia kuwa mshenga na mlezi

Muktasari:

  • Diamond anakuwa mrefu sana kimafanikio. Urefu wa wa mafanikio ni wenye kasi sawa na Mwanzi wa Kichina (Chinese Bamboo Tree). Wiki sita za kuchomoza kwake, Mwanzi wa Kichina hufikia urefu wa futi 80. Diamond katika umri mdogo wa uwepo wake kwenye game, amewatambuka wengi na kuwapita urefu.

BOSI wa WCB, Nasibu Abdul Juma a.k.a Diamond Platnumz, tukubali tukatae ni ‘Underground king’ wa Bongo kutokana umahiri wake wa kibiashara kwenye muziki. Jinsi familia ya WCB inavyopiga bao, inamweka Dangote wa Bongo Fleva matawi ya juu sana.

Diamond anakuwa mrefu sana kimafanikio. Urefu wa wa mafanikio ni wenye kasi sawa na Mwanzi wa Kichina (Chinese Bamboo Tree). Wiki sita za kuchomoza kwake, Mwanzi wa Kichina hufikia urefu wa futi 80. Diamond katika umri mdogo wa uwepo wake kwenye game, amewatambuka wengi na kuwapita urefu.

Anakua kwa kasi mno, hesabu mwaka 2009 alipotoa Kamwambie hadi alipo sasa akiwa staa mwenye jina kubwa Afrika na maeneo mengine ya dunia.

Anastahili pongezi nyingi kwa mafanikio yake. Ngome imara ya biashara ya muziki na familia inayostawi.

Unawezaje kumchukulia poa Diamond wakati kina Rayvanny, Harmonize na Lavalava ni mastaa waliochanua kupitia mbegu alizopanda, kuziotesha na kuzistawisha yeye mwenyewe? Hapo sijawasema Mboso wa Yamoto Band na Rich Mavoko ambao, sasa wanapata biashara mpya pale WCB.

MUZIKI, MAPENZI NA FAMILIA

Hata mwezi na nuru huangaza ila una upande wenye giza. Ni kule ambako hauangazi. Hivyo, Diamond pamoja na mafanikio yake ambayo yamewezesha kuchangamsha soko la muziki Tanzania, uwekezaji kwenye muziki na kutengeneza ajira nyingi hasa kupitia mitandao ya kijamii, kuna jambo si jema.

Ametengengeneza upacha kati ya muziki, mapenzi na familia yake. Kila kimoja kinatosha kuwa taasisi inayojitegemea, lakini ameshindwa kutenganisha, matokeo yake taasisi hizo tatu amezifanya kuwa moja, na kila moja inategemea nyingine.

Ameshindwa kufanya muziki uwe ni taasisi ya kikazi na isiingiliwe na mapenzi wala mwangwi wa familia. Mwenyewe hudhani ni chachandu ya biashara kuwahusisha wanawake wake kwenye muziki wake. Kilichotokea ni kusababisha mapenzi na wanawake wake kutokeza na kuuweka kati muziki wake.

Palipo na mapenzi ya Diamond na familia yake ipo jirani. Kumekuwa na taarifa nyingi kuonesha kuwa mama wa Diamond, Sanura Kassim na binti yake (dada wa Diamond) anayeitwa Esma, wamekuwa wakijihusisha kwa ukaribu mno na maisha ya kimapenzi ya Diamond. Mpaka hapo unawaona mapacha watatu wa Diamond; Muziki, Mapenzi na Familia.

Hivi karibuni uliibuka mvumo kuhusu mapenzi ya Diamond na familia yake. Wakati mvumo huo ukichukua nafasi, Diamond alitoa wimbo mpya, jina ni Iyena, akimshirikisha Rayvanny ambao ulikuwa na sura yenye kuendana na mzozo wa mapenzi na familia yake. Je, bado huwaoni mapacha watatu ndani ya Diamond?

Mzozo ulianza kwa Esma kuzungumza maneno kana kwamba anamwonea huruma Diamond kwamba, alikuwa akijifulia mwenyewe, akaongeza kuwa mdogo wake (Diamond) amekonda. Tafsiri ya jumla ikawa mwanamke wa Diamond, Hamisa Mobeto hamhudumii ipasavyo.

Kauli hiyo ya Esma ikamwamsha Diamond, aliyeandika kwenye ukurasa wake kwa vijembe kama anamtetea Hamisa kumbe anamuua, akasema kumwambia Esma: “Utadhani siyo wewe uliyekuja na Hamisa kwenye birthday, na arobaini ya Nillan na sare mkashona.”

Ni kusema Diamond alijifanya kumtetea Hamisa kwa Esma, alimbadilikia wakati walikuwa vizuri huko nyuma. Anapotajwa Nillan, anamaanishwa mtoto wa kiume wa Diamond kati ya wawili aliowapata na cheupe wake wa Uganda, Zari The Boss Lady. Mtoto wa Hamisa aliyezaa naye anaitwa Abdul “Dully”. Kuna kitu nitakijengea hoja baadaye.

Niliseme lingine lililovuma kuwa mama wa Diamond alimpa kibano Hamisa na kumtoa ‘mkwewe’ huyo kwenye nyumba. Hamisa naye alipoona maneno ya Diamond, akaposti ujumbe mrefu familia ya Diamond ndiyo haimtaki, wanasema yeye ni mchafu. Akasema hata mameneja wa Diamond hawamtaki. Hamisa aliandika kumwambia Diamond:

Kamilisha simulizi ya pacha watatu wa Diamond kwa kuzingatia video ya Iyena ambayo iliachiwa katikati ya mzozo wa Hamisa na familia ya Diamond, yumo Zari ambaye ni mama wa watoto wawili wa staa huyo, Tiffah na Nillan. Maudhui ya wimbo ni kwamba Diamond amemuoa Zari.

Video ilipotoka, mama Diamond aliposti Instagram picha ya Zari na kummwagia sifa kisha Esma akaongeza mapambio kwamba, Zari ni mwanamke msafi sana. Hapo zingatia kuwa Hamisa alipondwa kwa uchafu na kutomhudumia ipasavyo Diamond yeye kama mwanamke.

UMENEJA WA DIAMOND

Baada ya simulizi hiyo yote lakini sikuachi bila kukupa hii; wakati Iyena yenye Zari ndani yake ikitamba, Hamisa akikwaruzana na familia ya Diamond, huku akiwataja mpaka mameneja wa Diamond, hapohapo ikavuma mmoja wa mameneja wa Diamond, Hamis Taletale ‘Babu Tale’, alikwenda Afrika Kusini kuomba suluhu na Zari.

Kwamba Tale ilibidi afanye kazi ya ushenga kuhakikisha Diamond anarejea kwa Zari. Hapo ukiunganisha alama, unaweza kupatia ukisema kuwa mwanamke anayetakiwa na familia ya Diamond pamoja na mameneja wa mwanamuziki huyo ni Zari kama alivyosema Hamisa.

Kwa tafsiri hiyo, tukubaliane umeneja wa Diamond ni zaidi ya kazi za muziki. Inabidi kuvaa uhusika wa ushenga kama Tale alivyofanya kwa Zari, maana hakuna namna nyingine. Sababu kubwa, wakimwacha peke yake anaharibu. Mwenyewe alishaimba hakomi, wimbo unaitwa Sikomi. Ukiwa meneja wa Diamond inabidi kuwa mlezi, maana dogo wa Tandale anafanya ‘utoto’ mwingi. Mfano, dada yake anakwenda kuhojiwa kwenye televisheni na kuyazungumzia maisha yake ya ndani na mwanamke wake, halafu naye anajifanya kumtetea Hamisa ile kitoto. Nidhamu ya wapi? Esma kama yalimkera walipaswa kuzungumza ndani, siyo runingani.

Mwanamke akiwa wako hata akiwa na upungufu ni wajibu wako kumstahi. Mnazungumza kifamilia. Hata kuachana inapobidi unapaswa kuwa uamuzi wa mwanaume au mwanamke husika. Kuachana kwa sababu ya shinikizo la ndugu na mameneja ni kosa. Familia na mameneja wanapaswa kushauri, waamuzi ni wapendanao wenyewe.

Katika hili, ukiwa meneja wa Diamond inabidi pia umlee kitabia ili awe mwanaume na siyo mtoto wa kiume. Tabia za Diamond zinampambanua zaidi kama mtoto wa kiume na sio mwanaume. Jinsi Diamond alivyobwagana na Hamisa, inaonesha bado anazo za “ntakusemea kwa mama”. Kitendo cha mama Diamond kumpa kibano Hamisa, kinadhihirisha anamwona mwanaye bado ni wa “tema mate nimchape”.

Diamond alimtolea kauli za kibabe Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Juliana Shonza. Matamshi yale yalionesha bado anahitaji kulelewa. Mameneja wa Diamond inabidi wamlee kijana wao ili awe mwanaume na si mtoto wa kiume. Ajue kutenganisha maisha ya kazi zake, mapenzi na familia.

Ile kauli ya Diamond kuwa Hamisa na Esma walishona sare katika arobaini ya mtoto wa Zari ni kipimo cha wazi kuwa Diamond anahitaji kujengwa kitabia. Dada yake anamuona mtoto ndiyo maana anampeleka kitoto.

Mara nyingi meneja mwingine wa Diamond, Sallam SK huingia kwenye migogoro na wagomvi wa Diamond. Ilishatokea kwa Ali Kiba na Ommy Dimpoz. Ndiyo kusema huwa ‘anamgombelezea’, ukiwa meneja wa Diamond inabidi kuvaa ushenga, ulezi na kumgo mbelezea inapobidi.