Msipoteze muda kumtusi Kiba-2

Muktasari:

KIba alifunguka mambo mengi, lakini leo katika muendelezo wa makala zake anafichua jinsi makundi ya wasanii (Team) zilipotokea na athari zake katika muziki wa Tanzania. Endelea naye...!

JANA tulianza makala iliyotokana na mahojiano maalumu na nyota wa muziki wa kizazi kipya nchini, Ali Kiba kuelezea namna wimbo wake wa Seduce Me ulivyomshangaza hata yeye mwenyewe.

KIba alifunguka mambo mengi, lakini leo katika muendelezo wa makala zake anafichua jinsi makundi ya wasanii (Team) zilipotokea na athari zake katika muziki wa Tanzania. Endelea naye...!

Mwanaspoti ilimchomkea swali kutaka kujua yalipoanzia na kutokea makundi hayo na Kiba kwa ustadi na uangalifu wa hali ya juu anajikohoza kabla ya kulijibu kwa umakini;

“Hizo timu zipo nadhani mashabiki wenyewe ndiyo waliotengeneza. Sidhani kama kuna msanii aliyesimama na kuunda timu hizo, kunapokuwa na mahaba zaidi kwa wasanii watu hujua wanataka nini wenyewe, huwa wanajua namna ya kufanya ili kuwaunganisha na kuwachangamsha katika gemu, japo sitaki kusema kwamba nazikubali au nazikataa.”

AWAPOTEZEA WATUKANAO

Mitandaoni mashabiki wengi huwa wanatukana. Kuna mashabiki ambao moja kwa moja hulenga kumtukana matusi makali Kiba kupitia kurasa zake za mitandaoni au nyingineo. Kiba anatoboa siri kwamba huwa hana muda wa kupoteza wa kupitia kile ambacho kinaandikwa na mashabiki, hasa wale ambao wanamtukana.

“Hapana comment huwa sisomi sana, ila nina watu ambao huwa wanaangalia zipo nyingi ila ninachoambiwa ni kwamba huwa kunakuwa na matusi mengi sana.

Sina haja ya kusoma lakini watu ambao wanasoma huwa wanarudisha majibu kwangu, sana sana watu wa Menejimenti yangu,” anasema Kiba, huku akionekana kufadhaishwa mno na jambo hilo.

“Mimi nadhani bado hawajaelimika. Kitendo cha kumtusi mtu inaonyesha wazi kwamba wewe bado hujaelimika na haisaidii kitu, sanasana huwa inamuongezea nguvu halafu unamfanya awe proud ajue kwamba unamfuatilia kwa hiyo watu wote ambao huwa wananitukana mimi si mashabiki wangu japo najua huwezi kupendwa na wote.

“Nawakaribisha tu, ila ikiwezekana waendelee wapoteze muda wao, lakini mimi sina muda nao, nina imani kwamba nina sapoti ya wenye akili timamu.”

MAZURI WALA HAYAACHI

Hata hivyo Kiba anakiri kwamba watu wake wa Menejimenti pia huwa wanamfikishia mambo mazuri au ushauri mzuri ambao umetoka kwa mashabiki wake na kuna wakati anaufanyia kazi.

“Niliacha kusoma comment sababu ya matusi ni mengi, lakini uongozi wangu huwa unapitia, hivyo najua kitu gani cha kufanyia kazi na pia kusikiliza mashabiki wamesema hiki na hiki kwa hivyo lazima nipewe taarifa hizo na mazuri nayafanyia kazi.”

HURUMA ZA MASHABIKI?

Kuna hoja zimeibuka kutoka kwa baadhi ya mashabiki wa muziki kwamba Kiba amekuwa akipokelewa vema kwa sababu wengi wanachukia na jinsi anavyoshambuliwa na maadui zake huku akionekana akipambana peke yake. Ni kweli kuna huruma kutoka kwa mashabiki?

Kiba analijibu swali hili huku akishangaa kwa aliyeuliza.

“Nani ananionea huruma? Hamna mtu anayenionea huruma, watu wanafurahia muziki wangu na sijasikia. Kwanza sitaki kuonewa huruma mimi nafurahisha watu bwana unanioneaje huruma haina haja ya kunionea huruma furahia muziki wangu enjoy tu.”

Vipi kuhusu Kiki? Ungana na Kiba keshokutwa Alhamisi. Itaendelea.