Mama Kanumba ni bonge la mjanja

Muktasari:

  • Kifo chake kilikuwa gumzo kama filamu zake na mwishowe hakikumwacha mtu salama unaambiwa kwani, msanii mwenzake ambaye anatajwa alikuwa mpenzi wake, Elizabeth Michael ‘Lulu’, sasa hivi anatumikia kifungo cha miaka miwili jela kwa kutiwa hatiani na mahakama kuhusika na kifo chake.

KUISHI kwenye Jiji la Dar es Salaam, unahitaji kutumia akili kwelikweli vinginevyo itakula kwako. Si unakumbuka kuwa Aprili 7 ya kila mwaka ni kumbukumbu ya supastaa wa Bongo Movie, Steven Kanumba, aliyefariki dunia miaka sita iliyopita.

Kifo chake kilikuwa gumzo kama filamu zake na mwishowe hakikumwacha mtu salama unaambiwa kwani, msanii mwenzake ambaye anatajwa alikuwa mpenzi wake, Elizabeth Michael ‘Lulu’, sasa hivi anatumikia kifungo cha miaka miwili jela kwa kutiwa hatiani na mahakama kuhusika na kifo chake.

Kanumba anakumbukwa kwa mambo mengi, moja ni kuipaisha tasnia ya filamu kimataifa na kuongeza soko la kazi za sanaa za Tanzania, kipindi cha uhai wake.

Miongoni mwa kazi zake zilizobamba kinoma ni pamoja na Family Tears, A point of no return, The Lost Twins,The Stolen Will, Village Pastor, Magic House, Oprah, Red Valentine, This is it, Uncle JJ, Dar 2 Lagos na ile ya Devil Kingdom alizocheza na mastaa wa Nigeria.

Pia, enzi zake Kanumba aliongeza ushindani kwenye tasnia hiyo na alikuwa akichuana na mkali mwenzake, Vincent Kigosi ‘Ray’ na kuifanya Bongo Movie kuwa na ushindani kama ilivyo sasa kwa mastaa wa Bongo Flava, Diamond na Ali Kiba.

Mwanaspoti lilitia timu nyumbani kwa mama mzazi wa Kanumba, Flora Mtegoa, huko Kimara Temboni, Dar es Salaam na kupiga naye stori ikiwemo kumbukumbu ya staa huyo aliyekuwa kipenzi cha wengi.

Pia, Flora amezungumzia jinsi anavyommisi mwanaye huyo, ishu ya hukumu ya Lulu pamoja na kutemewa shombo na tuhuma zinazomwandama amekuwa akiombaomba pesa ili kuendesha maisha yake.

Kwa Flora, Kanumba alikuwa mtoto, baba na ndugu wa ukweli kwa kuwa, wazazi wake wote walishafariki dunia na hata ndugu zake watano waliozaliwa pamoja amebaki yeye tu, wengine walishatangulia mbele za haki.

Lakini, mbali na yote, mama Kanumba anafichua maujanja aliyoyafanya ili kumwezesha kuishi na kuendesha maisha ndani ya jiji, hasa wakati huu ambao kila mtu amekuwa akilalamikia ukata.

Hukumu ya Lulu

Kwanza amekiri amekuwa akirushiwa lawama nyingi kutokana na hukumu ya kifungo ya Lulu, akionekana ndiye chanzo cha adhabu hiyo. Hata hivyo, ameitaka jamii na watu wanaomwaga sumu wakimtuhumu, kufahamu mhusika wa kesi alikuwa Jamhuri na sio yeye ama familia yake.

“Watu wanashangaza sana, sijamshitaki Lulu iliyofanya hivyo ni Jamhuri. Kwa upande wangu nilishamsamehe kitambo kwani, hata angefungwa miaka 100 isingeweza kumrudisha Kanumba.

“Nimepokea simu nyingi, maneno ya shombo kila kukicha, lakini nilishamwachia Mungu na kufungwa kwa Lulu hakuwezi kubadili ukweli kuwa mwanangu amefariki dunia. Pamoja na matusi yote ya Lulu, nilishasemehe na sina kinyongo kabisa,” amesema.

Ishu ya kuombaomba ikoje

Baada ya kifo cha Kanumba, mengi yalisemwa ikiwemo Flora amekuwa akipiga mizinga (kuomba hela) kwa watu mbalimbali ili kumwezesha kuendesha maisha yake.

Lakini, anasema hilo halina ukweli ni watu waliamua kumwaga sumu kwani, hata Kanumba alipokuwa hai alikuwa akijishughulisha kusaka mkwanja na alijizoesha hivyo miaka mingi.

“Nina nguvu na uwezo wa kufanya kazi ikiwemo kutengeneza filamu, nina mashamba ya kutosha kule Bukoba pamoja na watoto wengine ambao wananipa huduma. Huyu anayesambaza huo uzushi atakuwa anatafuta kiki kupitia jina langu.

“Lulu hakuwa akinipa chochote na kama ana ushahidi na hilo mwambieni autoe, atanipa shilingi ngapi niweze kumsahau mwanangu na hakuna neno lililoniuma kama siku aliyonipigia na kuniita kubwa jinga huku akiniambia haogopi polisi wala mahakama,” anasema.

Atoa ushauri kwa Lulu

Flora anasema kama mzazi anamwonea huruma Lulu na anatamani kumtembelea gerezani na kumpa moyo, lakini kama ndugu zake watakuwa tayari japo hawezi kulazimisha hilo kukubaliwa.

“Mtoto wangu huyu anaweza kurudi mtaani na kushikwa masikio tena na watu kunifanyia vibweka kama alivyofanya awali, wala asithubutu wala kujihangaisha kwa kuwa iliyomshtaki ni Jamhuri hivyo anapaswa kuniheshimu,” anasema.

Auza magari ya Kanumba, anunua nyumba

Pamoja na kupiga mkwanja mrefu, lakini Kanumba hakuwa na mjengo japo alikuwa na ndinga kali hivyo, Flora akafanya ishu moja ya kijanja kwelikweli.

Anasema aliuza ndinga tatu za kijanja za mwanaye huyo na kununua mjengo maeneo ya Kimara Temboni na kwa sasa ndiko yalipo makazi yake na ameondoka kwenye mjengo wa familia uliopo maeneo ya Tandika.

“Kwa sasa nina amani na namiliki nyumba yangu, na nipo tayari kuendelea kupanda bodaboda, bajaji na daladala lakini nina mahali pa kulaza ubavu,” anasema.

Kanumba Day vipi

Kwa mwaka huu, Flora anasema kikundi cha Sanaa cha Soweto alichokuwa akikilea Kanumba kimeamua kubeba jukumu la kusimamia shoo ya maadhimisho hayo.

Pia, siku hiyo ya maadhimisho kutazinduliwa filamu inayoelezea maisha ya Kanumba huku ndani yake kukiwa na filamu mbili alizotengeneza na kufanya vizuri sokoni za ‘Uncle JJ’ na ‘This is It’.