Huyo Wakukurupuka usimchukulie poa

Tuesday February 13 2018

 

By SADDAM SADICK, MWANZA

BAADA ya jana Jumatatu mchekeshaji, Andrew Ngonyani ‘Brother K’ kufichua jinsi alivyotua kwa mara ya kwanza Futuhi na kazi yake ya kwanza na jinsi alivyoanza kupata umaarufu mkubwa kwa kutumia kipaji chake cha kuzaliwa.

Mvunja mbavu huyo aliweka bayana pia jinsi anavyoyapata mashati yake mapana akidai ni spesho oda na alibuni staili hiyo ili kuwanasa mashabiki wanaomfuatilia kipindi hicho cha Futuhi.

Brother K aliweka bayana namna anavyotofautisha maisha ya usanii na yale ya nje ya kazi hiyo hasa anapokuwa na familia yake.

Katika hitimisho la simulizi la msanii huyo mwenyeji wa Kigoma, aliyeanza kwenye fani ya uimbaji muziki, Brother K amekiri sanaa imempa mafanikio makubwa

kimaisha. Imempa mafanikio gani na changamoto zipi alizokutana nazo kwenye fani hiyo? Endelea naye...!

MAFANIKIO

Ikiwa ni miaka sita sasa tangu aanze kuchekesha msanii huyo anakiri sanaa hiyo imempa mafanikio mengi na anaamini kuna mengine yanakuja.

Anaeleza yeye alitoka Kigoma akiwa hana hili wala lile na haelewi atafanya nini, lakini hadi sasa mambo yanaenda poa kila kukicha milango inafunguka vizuri. “Hadi sasa naweza kusema mafanikio ni mengi, marafiki ninao na wanazidi kujitokeza kwa wingi, nina viwanja zaidi ya viwili hapa Mwanza, pia namiliki gari la maana, nimeoa na kuzaa watoto wawili na nimeanza kujenga mjengo wangu mkali hapa mjini na mengine mengi,” anasema.

Pia anasema ameweza kuongeza ujuzi kwenye kazi yake na kutanua wigo wa kuwa na wenzake ambao humwongezea uwezo wawapo kazini.

“Mengine ni kufanya kazi na makampuni makubwa, ambapo hadi sasa mimi ni Balozi wa Kampuni ya Mchezo wa Kubahatisha wa Tatu Mzuka, Mwanza Pure

Drinking Water na pia nina miradi yangu nayoendesha,” anasema Brother K. Alipoulizwa juu ya thamani ya tenda hizo za matangazo ya biashara, mvunja mbavu huyo alipotezea akidai ni siri yake na sio kila jambo liwe hadharani, ila anamshukuru Mungu.

CHANGAMOTO

Licha ya mafanikio aliyopata, mchekeshaji huyo amekumbana na changamoto nyingi ikiwemo kupata kipato kidogo wakati mwingine kulinganisha na kazi anazofanya.

“Kazi na mapato ni tofauti, tunafanya kazi kubwa lakini unajikuta mfukoni unaingiza pesa kidgo, ila yote kwa yote unashukuru maisha yanakwenda,” anasema.

Kadhalika pia wanajamii wanamchukulia kama mtu anayeringa kwa namna anavyokuwa tofauti nje ya wigo wa uchekeshaji wake.

“Mara nyingi watu hufikiria tunaringa kwani maisha ninayoishi mtaani ni tofauti na yale ya usanii, Nikiwa homu zaidi ya salamu huwa natulia ndani,” anasema Bother K ambaye nje ya sanaa ni fundi nzuri wa umeme wa majumbani.

MIZENGWE FRESHI

Brother K anakiri kuwa licha umahiri wake, lakini analikubali sana kundi la Mizengwe na hasa Mkwere Orijino na Maringo Saba.

“Awali nilikuwa nawakubali Comedy Original, lakini baada ya kusambaratika nakunwa sana na Mizengwe na hasa Mkwere, aisee jamaa anajua sana,” anasema.

Pia anamtaja Mzee Majuto kuwa ni mtu asiyechoka kumfuatilia tangu alipokuwa mdogo kwa umahiri wake. “Majuto anaweza sana, ni mchekeshaji ambaye anajua jinsi ya kuanza na kumaliza, tangu nianze kumfuatilia kazi zake nazielewa, pia amenisaidia sana,” anasema.

Hata Joti, Senga, Pembe na Ben anawakubali vilevile, huku akitaja kazi bora tano kuwa ni pamoja na filamu yake iitwayo Kirungu aliyocheza na Majuto na Hemed ‘PhD’. Nyingine ni Kimbulu,Dosari, Kiss My Pine na tamthilia ya Ligomba.

MIPANGO MINGI

Mchekeshaji huyi anasema ndoto zake ni kufika mbali hasa anga za kimataifa, lakini kubwa analowaza ni kuongeza ubunifu ili azidi kufunika, maisha yaende.

Anafikiria pia kufanya projekti kubwa akishirikisha wavunja mbavu wenzake kadhaa nchini ambao ameshaanza kuzungumza naye, lengo ni kuona Komedi inabamba zaidi, huku akiwataka vijana kuchangamkia dili la kujiunga na studio yao iitwayo Freedom Fighter Film anayoiendesha akisaidiana na Edward Kumalija (mkurugenzi).

KUMBE MJANJA BWANA

Brother K anasema sanaa ni nzuri kama mtu ataitumia vyema, kujijengea maisha na mafanikio kwa ujumla kiuchumi na kijamii, lakini ni mbaya kama ikitumiwa vibaya na kuwataka wasanii wasilemae kwenye kiki. Pia amewataka wasanii kuepuka starehe zisizo na mpango, kwani hazichelewi kuwaharibia.

Brother K, anakiri kwamba yeye ni mtumiaji mzuri wa pombe tena akitumia zile kali, lakini hakuwahi kulewa hadi kugaragara ama kushindwa kuendesha gari, kwa sababu anajidhibiti kwa kujitambua kuwa, yeye ni kioo cha jamii. Kuhusu jina lake la ‘Brother K’, mchekeshaji huyo anafafanua kwa kusema; “Nyumbani nilikuwa nikiitwa Karumanzila jina ambalo ni la Kiha na watu wa Mkoa

wa Kigoma wanajua sana maana yake, hivyo kupitia huko ndipo nikajiita Brother K, ikiwa na maana Kaka Karumanzila.”