VIDEO:Bila muziki ningepiga soka la uhakika-3

"Siku nyingine naweza kuamka nisitake kuzungumza na  mtu nikajifungia ndani siku nzima, lakini kuna wakati napenda kuzungumza na washkaji mambo kibao maskani."
ALI KIBA

Muktasari:

  • Anakiri na ana machaguo yake anapotaka kufanya kolabo na sio kila msanii tu anaweza kufanya kazi naye.

LEO Kiba anatamba na wimbo wa Seduce Me ambao ni wa karibuni zaidi kuutoa lakini kamwe hajasahau alikotoka. Anakumbuka nyimbo nyingi zilizomuweka katika chati ya muziki nchini na Afrika kwa jumla.

“Cinderella ilinitoa, lakini na Ali Kiba nalia nayo ilinitoa, baada ya tatu ambazo hazikufanya vizuri ila zilinitambulisha na kunipa shoo. Lakini, Cinderella ilibadilisha maisha yangu. Mac Muga pia, Mapenzi yanarun Dunia nazo zilibadilisha maisha yangu, lakini Aje ilileta sura mpya kabisa, ni kama hii Seduce Me,” anasema Kiba.

Pia, amekuwa akivuma katika nyimbo kibao za wanamuziki wenzake. ‘Mboga Saba’ alioshirikishwa na Mr Blue ni miongoni mwa nyingi ambazo Kiba amekuwa akiwapa kampani wasanii wenzake.

Hata hivyo, anakiri na ana machaguo yake anapotaka kufanya kolabo na sio kila msanii tu anaweza kufanya kazi naye.

“Siwezi kufanya kolabo na mtu, ambaye sijisikii kufanya naye kazi, pili kuna kipindi nilikuwa na mkataba ambao unanibana kufanya hivyo, sababu ya mlolongo mrefu hata ukifanya hivyo, kolabo kiasi cha malipo huwa na makato mengi.

“Nimesainiwa Global International Sony kwa hiyo inategemea na msanii sifanyi tu ili mradi ninafanya,” anaongeza Kiba.

“Hata hivyo, kuna vijana wengi huwa nawapa ushauri. Nikiona kama kuna sehemu amekosea huwa nawambia warekebishe na baadaye mambo yanakuwa sawa na inakuwa faida kwake,” anasema Kiba.

Katika kumalizia suala la maisha yake ya muziki, Kiba anajitazama na kuhisi atakuwa tofauti zaidi ndani ya miaka mitano ijayo.

“Nitakuwa msanii mkubwa duniani, nimeshafanya nyimbo na wasanii wakubwa duniani na nimefungua njia kwa wasanii wengine nchini. Nina lebo yangu (Kings Music) na ina wasanii kama sita ambao, nitawatambulisha karibuni,” anafunguka.

Katika  maisha binafsi, Kiba anakiri ana watoto watatu kwa mama tofauti huku wa kwanza akiwa na umri wa miaka tisa, wa pili akiwa na miaka saba na watatu akiwa na miaka minne.

Pia, kwa wanaomjua tangu anakua mitaa ya Kinondoni,  Kiba ni mwanasoka mahiri. Anatumia guu la kushoto na muziki ndio uliokatisha ndoto zake za kuwa staa mkubwa.

“Naamini nisingekuwa msanii ningekuwa mchezaji makini wa soka. Sijui ningefikia kiwango gani Mungu ndiye anayejua nilipotaka kuingia katika soka muziki ukaingia katikati na mwalimu wangu ni Mwanamtwa Kihwelo,”

“Alikuwa na connection Yanga na alikuwa anayecheza huko na ndiye aliyekuwa anataka kunipeleka huko msimu huo wa  2005-06. Nilikuwa kijana ila sasa hivi nimezee kidogo. Ila bado naendelea kucheza soka mpaka sasa hivi na hata nikiingia Ligi Kuu hata leo naweza sema mazoezi tu ndio tatizo,” anaongeza.

Anapenda kucheza kama mshambuliaji mwenye kumiliki mpira kwa sababu ni moja kati ya sifa ya mastraika wanaojiamini.

Mtaani kwake, ni mtu wa kawaida tu. Hata katika maisha yake ya kijamii, anakiri yuko vizuri na jamii na hushiriki misiba na harusi, ingawa hapendi kwenda harusini kwa kuogopa kuangaliwa sana.

“Ninashiriki vyote ila harusi inakuwa ngumu wakati mwingine,  unapokuwa pale macho yote kwako hivyo, nadhani watu inabidi waangalie wahusika. Katika msiba ni lazima kwenda kwa sababu watu wanakuwa katika majonzi.”

Huwa anaamka akiwa na mood tofauti kutegemeana na tu na jinsi hali ilivyo.

“Siku nyingine naweza kuamka nisitake kuongea na mtu nikajifungia ndani siku nzima. Siku nyingine najisikia kuongea na washkaji tu.”

Pia, anaamini muziki mzuri hauandaliwi ghafla ghafla bali unahitaji hisia. Anaamini anaishi maisha tofauti na wasanii wengi ambao huwa wanaswaga za kujifanya wapo bize na muziki kila siku na kila saa.

“Mimi studio naenda mpaka nijisikie. Siendi kila siku na huwezi ukanichukua tu, ukanipeleka huko siwewezi kufanya chochote nitakwenda tu, ukitaka nifanye vizuri lazima nijisikie, huwezi kuniletea chakula ukanilazimisha kula kama sina hamu ya kula.”

Kufikia hapo Kiba anakaribia kufunga mazungumzo yake. Anakaribia kupasua jipu katika orodha ya wasanii anaowakubali.

“Abdul Kiba (mdogo wake), Ommy Dimpoz, Mwana FA na Nuhu Mziwanda,” anamalizia Kiba na kunyayuka kabla ya kuanza kupata selfie na watu mbalimbali.

Mpaka anafika geti la kuondokea tayari watu zaidi ya 30 wanakuwa wameshapata fursa ya kupiga naye Selfie. Hapana shaka ni kwa sababu yeye ni Ali Kiba, lakini hapana shaka zaidi kwa sababu wimbo wa Seduce Me umemweka katika chati ya ajabu tena!.