BABU SEYA: Bonge la Sapraizi

Muktasari:

>>Ikiwa inaingia siku ya pili ya kuendelea kuvuta hewa ya uraiani, familia ya wanamuziki hao imetoa shukrani kwa kitendo hicho.

SAA 12 jioni ya Desemba 9, 2017 itaendelea kubaki vichwani mwa nyota wa zamani wa muziki wa dansi nchini, Nguza Viking ‘Babu Seya’ na mwanaye, Johnson Nguza ‘Papii Kocha’.

Ndio. Hiyo ni saa ambayo mtu na mwanaye hao walipotoka nje ya Gereza la Ukonga na kuikanyaga ardhi ya uraiani wakiwa raia huru baada ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, John Magufuli kuwapa msamaha.

Wawili hao kwa miaka 13 walikuwa jela wakitumikia adhabu ya kifungo cha maisha kwa kukutwa na hatia ya kuwadhalilisha watoto mwaka 2004.

Ikiwa inaingia siku ya pili ya kuendelea kuvuta hewa ya uraiani, familia ya wanamuziki hao imetoa shukrani kwa kitendo hicho.

Mtoto wa Babu Seya, Mbangu Viking kwa niaba ya familia alisema wanamshukuru Mungu pamoja na Rais Magufuli kwa kuwasamehe ndugu zao kwani kwao ilikuwa sapraizi na wanamuombea JPM azidi kubarikiwa uongozini.

“Kiukweli hatuna la kusema zaidi ya kutoa shukurani kwa Mwenyezi Mungu na Rais Magufuli kwani ni jambo la furaha kwa familia na watu wengine kuungana tena na ndugu zetu, hatukutarajia kabisa..Tunashukuru sana,” alisema Mbangu aliyeachiwa sambamba na mdogo wake, Francis Nguva baada ya kushinda rufaa dhidi ya kesi hiyo iliyohusisha wanafamilia wanne.

“Suala ya kifungo kwa ndugu zetu kweli limetubadilisha maisha tofauti na hapo mwanzo tulivyokuwa tunaishi kabla hakukuwa na kesi. Kwa sasa tumezidi kuwa wacha Mungu kwani kila kukicha tumekuwa tukiomba kwa kusali  na kufunga.”

FURAHA KILA KONA

Baadhi ya mashabiki na wasanii wamefurahishwa kwa kitendo cha wanamuziki hao kuachwa huru baadhi yao wakitabiri ni wakati wa muziki wa dansi kurudi kama zamani kwani Babu Seya na Papii Kocha walikuwa na mchango mkubwa.

PAPII KUWA MCHUNGAJI?

Katika barua yake kwa Rais Magufuli walipokuwa wakiomba waachiwe huru, Papii Kocha kuna kipengele kimoja aliandika kuwa mara akitoka gerezani atakuwa mchungaji na kuhubiri Neno la Mungu mtaani.

Hata walipokuwa wakimuangukia aliyekuwa Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Mrisho, alisisitiza angependa kuja kumtumikia Mungu, japo juzi alipoachiwa Papii alikuwa mgumu kuzungumza lolote, akitaka apumzike kwanza.

Lakini baadhi ya mashabiki wake wa muziki wa dansi, wameomba pamoja na kudai  hivyo, bado wanamsihi aendelee na muziki huku akiendelea kuhubiri.

KESI ILIVYOKUWA

Nguza na wanawe watatu walikamatwa Oktoba 12, mwaka 2003 na kufikishwa Kituo cha Polisi Magomeni, walipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Oktoba 16, mwaka 2003 wakituhumiwa kubaka na kunajisi watoto 10.

Baada ya kusikilizwa kesi hiyo Juni 25, 2004, Hakimu Mkuu Mkazi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar, Addy Lyamuya aliwatia hatiani Babu Seya na wanaye kwenda jela maisha kwenye Gereza la Ukonga, Dar es Salaam.

Januari 27, mwaka, 2005, Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Thomas Mihayo alitupilia mbali rufaa yao iliyokuwa ikipinga hukumu.

Ndipo 2010 waliomba tena rufaa ambayo marejeo yake yalisikilizwa na kutolewa hukumu Februari, 2010. Mahakama iliridhia hukumu ya kifungo cha maisha kwa Babu Seya na Papii Kocha, ikawaachia huru watoto wake, Mbangu na Francis Nguza.

SAPRAIZI TUPU

Babu Seya na Papii Kocha walikaa gerezani takriban miaka 13 na miezi minne wakikabiliwa kosa la kubaka na kulawiti watoto 10 wa kike ambao ni wanafunzi wa Shule ya Msingi Mashujaa, Sinza Dar es Salaam.

Lakini juzi Jumamosi saa 6 mchana akihutubia wananchi katika maadhimisho ya sherehe za Miaka 56 za Uhuru wa Tanganyika iliyofanyika viwanja wa Jamhuri Mjini Dodoma, Rais John Magufuli alitangaza kutoa msamaha kwa wafungwa 8,157 ikiwamo familia ya Nguza Viking.

Hilo liliwashtukiza Watanzania kwa sababu hakuna aliyekuwa akitarajia jambo hilo litatokea, ikizingatiwa rufaa zote zilizokatwa na kina Babu Seya zikigonga mwamba, lakini juzi ilikuwa ni sapraizi kwa kila mtu.

Mitaani wengi walionekana kufurahia na kumwagia sifa Rais Magufuli, huku kwenye mitandao ya kijamii mijadala ilikuwa msamaha kwa wanamuziki hao.

MKUU WA MAGEREZA

Baada ya Rais Magufuli kutoa kauli hiyo, saa 11 kasoro jioni Gazeti Dada la Mwananchi lilizungumza na Mkuu wa Magereza ya Mkoa wa Dar es Salaam, (DCP), Augustine Mboje aliyesema wapo katika hatua za mwisho za maandalizi ya kuwatoa Babu Seya na Papii Kocha.

Lakini ilipotimu saa 12 na dakika zake unaweza kusema watu waliokuwa nga’mbo ya pili ya Lango Kuu la Gereza la Ukonga walikuwa wanashangilia mpira kumbe sivyo, bali ni baada ya kuziona sura Babu Seya na Papii Kocha ambao walikuwa wakitoka katika gereza hilo.

Wakati wakitoka lango kuu la gereza Babu Seya na mwanaye waliwapungia mikono watu walikwenda kuwapokea huku Nguza Viking aliyevalia kitanashati akionekana kutoamini kilichotokea.

Ilikuwa ni furaha kutoka kwa ndugu na marafiki kutoka kwa wanamuziki hao walikwenda kuwapokea, hali hiyo ilisababisha msongamano wa magari kwa watu hao kutanda barabarani karibu na lango kuu la gereza la Ukonga.

Watu hao walisikikia wakilitaja jina la Rais Magufuli huku wakimkaribisha uraiani Babu Seya kwa jina babu babu babu..., hatua hiyo ililazimu askari

Magereza kuingilia na kati na kuwazuia watu na kuwaingiza wasanii katika gari lao wakishirikiana na ndugu zao wa karibu.

GITAA BEGANI

Wakati wanatoka Babu Seya na Papii Kocha waliendelea kudhihirisha kuwa muziki ni asili yao kwani walikuwa wamebeba gitaa na walionekana watu wenye nyuso za furaha na msafara wao ulielekea moja kwa moja katika Kanisa la Life in Christ Ministries Zoe lililopo Tabata Segera kwa ajili ya maombezi maalumu.

Walifika kanisa hapo saa 1 usiku wakati wakishuka garini kwa furaha iliongezeka kwa ndugu zao wakaribu na wengine waliwakumbatia na kuwapa pole huku wakiwakaribisha kuendelea na maisha ya uraiani.

Miongoni mwa marafiki wa karibu walioambatana na Papii Kocha na Babu Seya ni mwanamuziki wa dansi Nyoshi El Sadat ambaye kila wakati alionekana kuwa mtu mwenye furaha na kumshukuru Mungu na Rais Magufuli kwa kuachilia huru wanamuziki wenzake.

“Namshukuru sana ndiyo maana nipo hapa. Nilikuwa nimelala nilipoamka saa 9 alasiri na nilivyoangalia simu nikakuta kuna idadi kubwa ya watu walionipigia

na kunitumia ujumbe mfupi, ikanibidi nichukue gari na kwenda gerezani na tumetoka tupo hapa kanisani.

“Tuna mshukuru Mwenyezi Mungu na Rais Magufuli kwa kuwaseheme wote na siyo familii hii pekee,” lisema Nyoshi ambaye aliwahi kufanya kazi na Papii Kocha wakiwa katika bendi ya FM Academia ‘Wazee wa Ngwasuma’.

“Nikiongelea familia hii watasema napendelea ila tunashukuru kwa Rais kwa kuwaseheme wote.”

Wakiwa katika sehemu ya mapokezi kanisani hapo, Babu Seya na Papii Kocha walionyesha furaha kila wakati na baada ya kufika sehemu huku Nyoshi akiwaongelesha lugha ya Kikongo kwa maneno ya ‘Papaa mapasa’Papaa na Blandii, huku Sadat akiitia bie bie...

KULONGA LEO

Francis Nguza ambaye kwa sasa ni Mchungaji, alisema kuwa kwa kuwa ndugu zake wametoka kifungoni bila kutarajia ni vema waachwe wapumzike na leo Jumatatu huenda wakazungumza kutoa shukrani zao rasmi.

UTABIRI WATIMIA

Kama hufahamu ni kwamba kuachiwa huru kwa kina Babu Seya ni utabiri tu, kwani Sheikh Yahya Hussein enzi za uhai wake aliwahi kutabiri wanamuziki hao watakuja kuachiwa huru hata kama makosa yao ni makubwa kisheria.

Utabiri huo ulitolewa mapema Februari mwaka 2010 na hata alipokuwa mrithi wake, Hassan Yahya Hussein alirejea tena utabiri huo Machi 2016 alinukuliwa

akisisitiza utabiri wa baba yake, utatimia na wanaodhani ni uongo wasubiri.

“Watu wengi wamekuwa wakiniulizia juu ya utabiri wa marehemu Sheikh Yahya kuhusu Babu Seya, jibu ni hili kwamba ipo siku wataachiwa na watu watakuja kushangazwa.”

“Unajua tabiri inapofanyika sio lazima itimie siku ileile au mwaka uleule, unaweza kudumu kwa miaka hata 50 lakini ipo siku hutimia na watu kuukumbuka, “ aliwahi kunukuliwa Maalim Hassan.

KIMUZIKI

Wanamuziki hao waliowahi kutamba kwenye bendi mbalimbali za muziki wa dansi na kufunika na kibao cha ‘Seya Tutoke Wote’ wakiimba kwa kushiriki ikiwa ni marudio wa kibao cha Seya alitunga Nguza akiwa Orchestra Marquiz, walikuwa wakiendelea kupiga muziki hata walipokuwa jela.

Wakati huohuo, Nabii  Joseph wa Kanisa la Life in Christ Ministries Zoe, alisema Jumapili Papii Kocha na Baba yake wataimba wimbo maalumu wa ‘Siku za Maisha Nilizokuwa Jela’ waliotungiwa na kanisa hilo.

Nguza ambaye ni muimbaji anakumbukwa kwa kazi nzuri alizofanya enzi hizo kupitia bendi kadhaa zikiwamo FM Academia na TOT -Plus. Baba yake mbali ya utunzi na uimbaji, ni mahiri kwa kucharaza gitaa la solo akiwahi kutamba na nyimbo kadhaa.