MTAA WA KATI: Afrika na ugonjwa wao uleule Kombe la Dunia

RUSSIA kumenoga. Kuna mengi yanatoa somo. Lakini, si kwa timu za Afrika, bado zinaishi dunia ileile ya miaka iliyopita.

Pengine bora hata zama zilizopita, wakati ziliposhiriki kwenye fainali za Kombe la Dunia. Lakini, kwa sasa, nchi ya kutoka Afrika inapoingia uwanjani kitu unachoweza kukifiria kwa wakati huo, watafungwa ngapi, si kama watafunga au watafungwa.

Hakuna jipya, walau Senegal wameshinda mechi moja. Huku bao moja likiwa la kujifunga na jingine likiwa lenye utata mtupu. Hilo ndilo unaloweza kusema.

Si kwamba nabeza ushindi wa Simba wa Teranga, lakini unaweza kuona hata mabao yenyewe yamekuja tu, hayana ushawishi.

Misri ndiyo hivyo, inasubiri kukamilisha ratiba, wakati Morocco nayo ndiyo kama ulivyosikia.

Hakuna lenye kutia raha. Iran hii leo inapata ushindi kwenye Kombe la Dunia. Mexico inashinda dhidi ya Ujerumani, huku mataifa mengine kama Iceland, Uswisi yanazigomea timu za mataifa makubwa yanayopewa nafasi ya kuwa mabingwa kama Argentina na Brazil.

Sijui Waafrika wanashindwa kitu gani.

Mataifa kama Nigeria, Morocco na hata Misri, ambayo si mara yao ya kwanza kucheza kwenye fainali hizo za Kombe la Dunia, yalitarajiwa kufanya mambo mazuri, lakini yenyewe yamegeuzwa kuwa ngazi ya watu kujichotea tu pointi kirahisi. Inakera kweli kweli.

Iceland inabaki kuwa mfano ambao kwa nchi za Afrika zinazokwenda kupambana kwenye michuano mikubwa kama hiyo zinapaswa kuitazama.

Si taifa linalokubali kushindwa vita kirahisi. Miaka miwili iliyopita, walimdhibiti Cristiano Ronaldo na Ureno yake asipate ushindi kwenye Euro 2016.

Mwaka huu wamemzuia mchezaji mwingine hatari duniani, Lionel Messi na Argentina yake asipate ushindi kwenye Kombe la Dunia. Mechi zote hizo mbili walizocheza na mastaa hao hatari duniani zilimalizika kwa sare huku Ronaldo na Messi wote wakitoka kapa.

Hiyo ina maana kwamba wamejenga uwezo wa kupambana na kufunga pia mabao dhidi ya timu ngumu. Sawa, mpira ni mchezo wenye roho mbaya, kwa sababu unachokidhania kinaweza kisiwe, lakini, jambo hilo linategemea zaidi na timu yenyewe kupambana pia ndani ya uwanja.

Tazama kama Uswisi ilivyopambana kupata matokeo mbele ya Brazil. Tazama Mexico ilivyochimba kwelikweli kushinda mbele ya Ujerumani. Hayo si matokeo yanayokuja kibahati tu, yanahitaji jitihada kubwa. Nilitarajia kuona kitu tofauti kwa Misri.

Nilitaraji kuona Nigeria mpya yenye nguvu tofauti, hata Morocco pia nilijaribu kuipa nafasi baada ya kuona inacheza na Iran. Lakini, ilikuwa kazi bure kuamini mabadiliko kwenye timu hizo. Hili linazidi kuendeleza rekodi ya kufanya Afrika iendelee kuwa na timu za kusindikiza tu na madaraja ya kugawa pointi kwenye fainali za Kombe la Dunia.