Bila nidhamu Waafrika wataburuzwa milele!

MIAKA kadhaa nyuma, Waafrika wengi walipiga kelele kutaka bara lao liongezewe timu za uwakilishi wa Fainali za Kombe la Dunia. Wengi waliamini Afrika ilikuwa inatengwa na kubaguliwa kwa kupewa uwakilishi mdogo. Wapo walioamini Marais waliopita wa FIFA walikuwa wakiibania Afrika. Wengi waliamini idadi ya timu kuanzia moja iliyokuwa awali na kuja kuongezwa baada ya muda mrefu kuwa mbili na kisha tatu iliyodumu kwa muda mrefu hasa chini ya Rais wa Saba wa FIFA, Joao Havelange ililinyima Afrika nafasi ya kufika hatua za mbali katika fainali hizo.

Rais wa Nane, Joseph ‘Sepp’ Blatter, alisikiliza kilio cha Waafrika na kuiongezea timu mbili zaidi na kufikia tano zilizopo sasa.

Hata hivyo licha ya ongezeko la idadi ya timu za Afrika katika fainali za Dunia, bado hakuna maajabu yoyote yanayokea katika fainali hizo. Mafanikio makubwa ni kutinga robo fainali kwa Cameroon mwaka 1990, Senegal mwaka 2002 na Ghana mwaka 2010.

Ipo tofauti kubwa ya timu za Afrika na za mataifa mengine yanayoshiriki fainali hizo. Timu za Afrika na hasa wachezaji wake hawana nidhamu uwanjani. Nidhamu ya kupambana na adui. Nidhamu ya kuziheshimu bendera zao za taifa na nidhamu ya kuzipa mafanikio timu zao za taifa. Wengi wa mastaa wa Afrika wanaenda katika fainali hizo kuuza sura na sio kupambana ndio maana miaka nenda rudi wanashindwa kufanya maajabu.

Ukiviangalia vikosi vya timu za Afrika na aina wachezaji walionao wanaotamba katika klabu mbalimbali Ulaya, unaweza kutishika na kuwapa turufu ukiwatabiria watafika fainali na hata kubeba taji.

Lakini linapokuja suala la kucheza uwanjani ndipo utabaini kuwa, bado tuna kazi ndefu ya kupanda mlima wa mafanikio.

Ubishoo, kiburi na kuamini wamemaliza kila kitu ni kati ya mambo yanayowangusha nyota wengi wa Afrika. Huwezi kuwalinganisha na wachezaji wa timu za mataifa mengine yasiyo na nyota wanaotisha duniani ambao wanacheza jihadi.

Kwa jinsi Waafrika wasivyopenda kubadilika ni wazi tunaendelea kuburuzwa kinyonge katika fainali hizo na sio ajabu miaka ijayo idadi ya timu zetu za uwakilishi zikaja kupunguzwa kwa mkakati wa kijanja kutokana na ukweli tunaonekana hatuna jipya.