Lionel Messi anatia huruma, ila dharau kazitaka mwenyewe

MAISHA yanaenda kwa kasi. Bahati mbaya ni kwamba siku ikipita huwa haijirudii tena. Ila kuna wakati mtu hutamani miaka irudi nyuma ili kusahihisha makosa, japo huwa vigumu kufanikisha ndoto hizo za alnacha.

Naam, wakati akitimiza miaka 31 kamili leo hii tangu aletwe dunia na Jorge Messi na Celia Cuccittin, Juni 24, 1987 Lionel Andres Messi bila shaka huko aliko sasa huenda anajutia ukigeugeu wake.

Ndio, Messi mmoja ya wachezaji waliopata kila kitu katika maisha yake ya soka isipokuwa Kombe la Dunia, anajutia maamuzi yake. Maamuzi ya kuamua kustaafu soka ndani ya La Albiceleste kisha kula matapishi yake kwa kurudi kukichezea kikosi hicho.

Siku mbili tu baada ya kutimiza miaka 29, yaani mwaka 2016 Messi alitangaza uamuzi wa kijasiri wa kuachana na soka la kimataifa baada ya kushindwa kuibeba Argentina katika fainali za Copa America 2016 zilizofanyikia mchini Marekani.

Messi alitangaza uamuzi huo, huku roho ikimuuma kwani licha ya kuona hana bahati na timu hiyo, iliyopoteza mechi ya fainali dhidi ya Chile kwa mikwaju ya penalti, huku yeye akikosa mkwaju wake wa kwanza tu, lakini bado alitamani kuendelea kuitumikia.

Staa huyo aliyekuwa na hiari ya kuichezea Hispania, nchi aliyokulia na kumzoea kuliko taifa aliloling’ang’ania la Argentina alikozaliwa, mwaka huo alikuwa amepoteza fainali yake ya tatu mfululizo kati ya nne alizocheza.

Kwani mwaka mmoja nyuma walipoteza tena kwa Chile kwa penalti, japo alifunga ndipo akaamua kutangaza kujiweka kando baada ya kila mtu kumtuhumu kwamba

amekuwa hajitumi akiwa na Argentina tofauti na anavyoichezea klabu ya Barcelona.

Uamuzi wake wa kustaafu ulikuwa sahihi katika wakati muafaka, lakini kelele za mashabiki na waliotaka aendelee kusumbuana na Cristiano Ronaldo walimgomea.

Ndipo Messi aliamua kula matapishi yake na kurejea tena kikosini wiki chache tu baadaye na bahati mbaya ni kwamba Messi alirejea La Albiceleste akikutana tena na nyota wale wale alioshindwa kushirikiana nao kuipa mafanikio timu hiyo ya taifa.

Hata hivyo ni wazi, Messi alijipa moyo kwa kuwa alikuwa akifanya makubwa Barcelona, basi huenda mambo yangekaa sawa na wachezaji wenzake wangeshirikiana naye upya kufanya mambo.

Alisahau Barcelona na Argentina ni vitu viwili tofauti na hata mfumo wake na aina ya wachezaji aliokuwa anacheza nao ni tofauti. Hata kama aliisaidia kuivusha Fainali za Kombe la Dunia 2018 zinazofanyika Russia, lakini bado Messi alikuwa amejitishwa gunia la misumari kichwani mwake.

Gunia hilo leo limemuaibisha Russia. Dunia yote kwa sasa inamnyooshea kidole na kumzomea kwa vile tu, Argentina imechechemea mikononi mwake kama nahodha.

Mechi mbili na kuvuna alama moja tu na kipigo juu toka kwa Croatia zimengeuka, huku staa huyo akiwa hana hata bao la kuotea. Aibu iliyoje?

Kinachotia uchungu zaidi ni kwamba hasimu wake, Ronaldo na Ureno yake anatakata, kwani bishoo huyo anaongoza orodha ya wafungaji na mabao yake manne, huku timu yake ikiingia mguu mmoja hatua ya 16 Bora.

Inawezekana ni kweli Messi hastahili kulaumiwa kwa kukosa maajabu Russia akiwa na Argentina, lakini upande wa pili ni kama aliyataka mwenyewe dharau hizi anazofanyiwa sasa...!

Baadhi ya mashabiki wanakejeli eti, wakati mwenzake, yaani Ronaldo anafunga mabao Russia, yeye (Messi) anafuga ndevu tu. Naamini kama angeamua kukomalia msimamo wake wa kujiweka kando mwaka juzi kama alivyokomaa Diego Costa kuitosa Brazili na kuing’ang’ania Hispania, huenda leo angekuwa shujaa kwa kuyumba kwa Argentina.

Watu wangeona kuyumba kwa timu hiyo kunatokana na kukosekana kwake kikosini, japo hakuna mwenye hakika kama La Albiceleste ingefuzu hata hizo fainali zenyewe.

Mwenzake, Costa ni kweli alianza vibaya Hispania na kupondwa, lakini kwa sasa jamaa amegeuka lulu na wote waliomponda na kumuona msaliti kwa taifa lake mama la Brazili, wanamshangilia kwa vile anaibeba La Furia Roja a.k.a La Roja katika fainali za Russia. Tayari ana mabao matatu katika fainali hizo akimfukuzia Ronaldo, wakati Messi akipiga miayo!

Ni kweli tunapaswa kumuoneahuruma Messi kwa hali anayokutana nayo Russia, lakini pia tukumbuke kuwa, dharau hizi alizitafuta mwenyewe, hivyo mwache aipate freshi!