NINAVYOJUA: Tunaweza kupata wachezaji wenye maumbo mazuri!

FAINALI za soka za Kombe la Dunia zinaendelea kule Russia. Watanzania nasi ni sehemu ya wafuatiliaji wa michuano hiyo. Hatuna timu huko ila baadhi yetu wapo huko. Wapo walioenda kwa kualikwa, pia wapo waandishi wa habari. Lakini wengi wetu tupo nchini tukifuatilia kupitia runinga zetu.

Yapo mengi ya kujifunza na kuyaandikia ikiwa ni kama funzo kwa vijana wetu na viongozi wetu wanaotakiwa kusimamia soka nchini. Kombe la Dunia ndio kioo cha soka.

Kati ya mambo yaliyovutia wengi wetu ni jinsi nchi kupitia kwa wataalamu wa mabenchi ya ufundi, wanavyoamua kwenda na mfumo wautakao huku wakiteua wachezaji wanaofaa kutumika kwenye mifumo hiyo, lakini pia umuhimu wa kuamua nani acheze wapi kulingana na umbo alilonalo, na je, kuna faida ya kumchezesha mchezaji wa aina fulani kwenye maeneo tofauti.

Hapa ndipo tunapoona jinsi gani wenzetu walivyochagua kuwatumia wachezaji wenye maumbo mazuri ya mpira, namaanisha wachezaji warefu na wenye uwezo wa kucheza aina ngumu za mpira uwanjani, yaani ama kutumia mipira mirefu kuelekea mbele ama pia kutumia nguvu nyingi kwenye kugombania mipira.

Zipo nchi ambazo zimekuwa na bahati ya kuwa na wachezaji wenye vimo vifupi na kutumia aina tofauti ya mchezo ili kukabiliana na wapinzani. Argentina ni moja kati ya nchi zenye kuzalisha wachezaji wenye vipaji vya hali ya juu, lakini wakiwa na vimo vifupi kabisa.

Mastaa kama Diego Maradona, Lionel Messi ,Carlos Teves, Sergio Aguero, Paul Dybala na wengineo, wengi hawana vimo virefu tofauti zao ni jinsi walivyojengeka kwenye misuli yao ya miguu.

Kutokana na hilo ni mara chache kuwaona Argentina wakitumia mipira ya krosi au mipira ya juu, badala yake wamejikita katika kutandaza soka la chini.

Nchi kama Hispania nayo ina mchanganyiko wa wachezaji wenye vipaji vya hali ya juu, lakini wakiwa na vimo vifupi. Waangalie Andre Iniesta, kipindi hicho Xavi Hernandez, Isco, David Silva na wengineo.

Hawa wote niliowataja hapo juu, tangu mwanzo wamekuwa hawana wasiwasi na makuzi yao, kuanzia vyakula wanavyokula na aina ya mazoezi wanayofanya.

Unaweza kuuona mguu wa Sergio Arguero ukaufaninisha na mguu wa Shiza Kichuya? Ni watu wawili tofauti au mguu wa Jordi Alba ukawa sawa na wa Hassan Kessy? Ni mbingu na nchi japo wote ni wafupi.

Lakini angalia maumbo ya wenzetu wa Afrika Magharibi, umewaona Senegal jinsi walivyo na vimo, angalia jinsi vimo vinavyowasaidia kukabilana na timu zenye wachezaji wenye nguvu, unaona jinsi wenzeu wanavyojua kuchagua maumbo ya wachezaji wenye vimo ambao wanakuwa msaada mkubwa kwenye timu.

Sisi Watanzania tuna mataizo mengi na mengine yapo kweye ufundi zaidi pamoja na kusemwa kuwa wachezaji wengi wa Tanzania wenye maumbo mazuri warefu wamekuwa wavivu sana wa mazoezi na huwa hawajitumi.

Angalia jinsi kipaji cha Jerry Tegete kilivyopotea, umbo lile na uwezo ule unapoteaje kirahisi, angalia urefu wa Ibrahimu Ajibu, angalia urefu wa kina Gaudence Mwaikimba, angalia urefu wa kina Matheo Antony unaweza kukubaliana kuwa kweli wachezaji wetu warefu hawajitumi na kujitambua.

Lakini kingine na kikubwa kutoka kwetu ni kwa wataalamu wetu wengi hasa makocha tumekuwa kama si wavivu wa kuchagua maumbo mazuri ya wachezaji, basi ni waoga, tunaogopa kumchagua mchezaji mwenye kimo kizuri asiye na kipaji kikubwa tunakimbilia kuchagua mchezaji mfupi mwenye kimo cha kawaida tukitegemea zaidi kutoka kwenye kipaji chake. Tunasahau kuwa ni rahisi kumwendeleza mchezaji mwenye kimo kirefu na akakupa faida ya muda mrefu huko baadaye. Ni kweli wachezaji warefu wazuri wamepungua lakini bado hata kuwachagua wachezaji kulingana na nafasi zao napo hatufanyi hivyo. Unawezaje kumchagua na kumchezesha mchezaji mfupi kwenye nafasi ya beki wa kati, au kwenye nafasi ya ushambuliaji wa kati?

Hapo zamani ilikuwa si rahisi kumuona beki wa kati mfupi akicheza katikati, ilitokea tu wenzetu wanaita ‘exceptional’ kwa George Masatu wa Pamba, Simba na Taifa Stars kwa kuwa tu kipindi kile kulikuwa na mfumo wa kumtumia ‘Libero’ na kulikuwa na kitu kinaitwa ‘Offside Position’ hivyo kwa kuwa kwake na kipaji fulani Masatu aliweza kucheza kama beki wa kati.

Wengine waliobaki walikuwa mapandikizi ya watu kina Jela Mtagwa, Mohamed Bakari “Tall’, Athumani Juma, Leodegar Tenga na wengineo wengi, usingemkuta mchezaji mfupi katikati, yaani kina Yussuf Mlipili, Andrew Vincent haikuwezekana.

Kwa sasa Watanzania tumekuwa wavivu wa kuwachagua wachezaji kulingana na maeneo yao. Mbona Prisons iliweza kwa miaka mingi, Mtibwa pia, Prisons iliwapata wapi kina Gerald Hilu, Olaph Mwamlima leo kuna kina Jumanne Elfadhil, Nurdin Chona kina Dick Daudi wote hawa hawana vipaji sana lakini wanakusaidia kukupa kile kinachotakiwa kutoka kwa mabeki wa kati.