Hongereni Simba kwa ubingwa, lakini msisahau ujumbe wa JPM

Muktasari:

Mabingwa hao wapya walikuwa na misimu mitano mfululizo bila kulibeba taji hil, kwani mara ya mwisho walilitwaa msimu wa 2011-2012 na kukabidhiwa rasmi Mei 6, 2012 mara baada ya kuikandamiza Yanga kwa mabao 5-0.

SIMBA wamekabidhiwa taji lao la ubingwa wa Ligi Kuu Bara na kufuta ule ukame wa muda mrefu waliokuwa nao wa kutolibeba taji hilo.

Mabingwa hao wapya walikuwa na misimu mitano mfululizo bila kulibeba taji hil, kwani mara ya mwisho walilitwaa msimu wa 2011-2012 na kukabidhiwa rasmi Mei 6, 2012 mara baada ya kuikandamiza Yanga kwa mabao 5-0.

Simba imefanikiwa kubeba ubingwa huo unaokuwa ni wa 19 kwao tangu Ligi Kuu Bara ilipoasisiwa mwaka 1965, ikiwa ni pungufu ya mataji nane waliyonayo watani zao wa Yanga wanaoshikilia rekodi ya kubeba mara nyingi wakifanya hivyo mara 27.

Kitu kilichosisimua mashabiki wengi wa Simba na hata wanachama, wachezaji, makocha na viongozi wa klabu hiyo ya Msimbazi ni taji lao kukabidhiwa na Rais wa nchi, John Magufuli aliyekuwa mgeni rasmi katika mechi yao dhidi ya Kagera Sugar.

Katika mchezo huo uliochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na mashabiki lukuki, Simba ilipoteza mbele ya Kagera kwa bao 1-0 ikiwa ni kipigo cha kwanza kwao ndani ya mwaka mmoja na mwezi mmoja.

Simba ilikuwa imecheza mechi 34 katika kipindi hicho bila kupoteza tangu walipolazwa mabao 2-1 na Kagera hao hao katika ligi ya msimu uliopita iliyopigwa Aprili 2, 2017 na mechi hizo kuzaa utata kwa Simba kukata rufani ikitaka ipewe ushindi wa mezani.

Tangu kipigo hicho Simba ilikuwa ikizinyoosha timu inazokutana nazo na waliponea chupuchupu walikuwa wakiambulia sare.

Mwanaspoti linarudia tena kuipongeza Simba kwa mafanikio iliyopata mpaka kukata mzizi wa fitina kwa kubeba ubingwa kabla ligi haijamalizika na pia tunawapa pongezi kwa rekodi hiyo ya kucheza mechi mfululizo bila kupoteza, japo haijafikia rekodi ya Azam iliyocheza mechi 38 misimu michache iliyopita bila kupoteza mchezo wowote.

Lakini wakati wadau wa Simba wakiendelea kusherehekea taji lao, licha ya kutibuliwa na kipigo cha Kagera Sugar, Mwanaspoti linataka kuwakumbusha wana Simba juu ya kile alichokisema Rais Magufuli juzi kabla ya kuwakabidhi taji lao.

Rais Magufuli alizungumza mengi katika hotuba yake lakini kubwa ni wito wake kwa klabu ya Simba juu ya kutaka iwe ya kwanza kulileta taji la Afrika Tanzania, huku akikiri wazi kwa soka lililoonyeshwa na timu hiyo mbele ya Kagera ni vigumu kufanikisha hilo.

“Niwaombe Simba muwe wa kwanza kuniletea ubingwa wa Afrika...Kwa mpira huu wa leo (juzi), niliouona hamuwezi kuchukua ubingwa huo wa Afrika, lazima mbadilike.”

Hiyo ilikuwa kauli ya Rais iliyokuwa na mantiki kubwa kwa wana Msimbazi na klabu nyingine wawakilishi wa Tanzania katika soka la kimataifa.

Simba na klabu nyingine ambazo zinaamini kuwa zinacheza soka la kiwango cha juu, lazima zibadilike kweli kama zinataka kuleta ushindani wa michuano ya kimataifa.

Kwa muda mrefu tumekuwa tukishuhudia timu zetu zikiishia njiani katika michuano ya CAF, huku zilizobahatika kuingia makundi zimekuwa kama jamvi la wageni ambayo kila mtu analikalia mfano inavyotokea kwa Yanga sasa ikiwa Kombe la Shirikisho Afrika.

Simba yenyewe ikiwa na kikosi hicho hicho kilichobeba ubingwa wa Tanzania, kiliishia njiani kwenye ushiriki wake wa michuano ya CAF kwa kutolewa raundi ya kwanza na Al Masry ya Misri, huku Zimamoto na JKU zilizowakilisha Zanzibar zikiishia raundi za awali.

Hivyo ni wazi Rais Magufuli alikuwa anafikisha kilio cha Watanzania walio wengi ambao wamekuwa na kiu ya kutaka kuona timu za Tanzania zinatamba katika michuano ya kimataifa ikiwezekana ibebe taji hilo badala ya kuwa washiriki.

Haziwezi kufanya maajabu kama hazitabadilika na kufanya maandalizi ya maana ikiwemo usajili wa nyota wenye uwezo wa kuhimili vishindo vya wenzao wa klabu watakazoumana nazo ama kukutana nazo katika michuano hiyo ya CAF.

Klabu za Tanzania ikiwamo mabingwa wapya Simba, wasiridhike na soka la kutambiana wenyewe kwa wenyewe nyumbani, kwani viwango vya timu shiriki katika Ligi Kuu Bara vinatofautiana kidogo mno, hivyo hawezi kupata kipimo cha ubora.

Ndio maana tunasisitiza Simba na klabu nyingine waichukulie kauli ya Rais Magufuli kama chachu ya kujivua gamba sasa, ili watakapoiwakilisha Tanzania watimize ombi la Kiongozi Mkuu huyo wa nchi na kama itashindikana basi angalau wafike japo fainali.