Ingeshangaza kama Simba isingebeba ubingwa

Tuesday May 15 2018

 

By EDO KUMWEMBE

HAIJASHANGAZA Simba kuchukua ubingwa. Kama Simba isingechukua ubingwa ningehoji mambo mengi kuhusu soka letu. Walau kwa sasa naweza kumpumzika na nikakosa sababu kadhaa za kuhoji kuhusu mpira.

Yanga ingewezaje kuwa bingwa? Azam ingewezaje kuwa bingwa? Halafu Simba ingekosaje ubingwa? Kwa sababu za kisoka ingeshangaza sana. Hasa pale unapofikiria kwamba Simba walikuwa wameimarika katika kipindi ambacho Yanga na Azam wameanza kufanya masihara.

Mwaka jana, niliandika mahala kwamba Simba walikuwa wamejaza wavulana katika kikosi chao. Katika lugha ya soka, uvulana au uanaume sio umri. Ni tabia yako katika soka. Ni ukosefu wako wa umakini katika soka ndio ambao unasababisha uitwe mvulana.

Angalia safu yao ya ushambuliaji ya msimu uliopita iliyoongozwa na Laudit Mavugo ilivyokuwa imejaa utoto mwingi na kukosa mabao ya wazi. Angalia walivyokuwa wanashindwa kumaliza mechi zao. Kuna wakati waliongoza pointi nane dhidi ya Yanga wakaishia kulingana pointi na kisha kukimbilia FIFA.

Simba hawa walijaza wanaume. Inachekesha zaidi kwamba wanaume wanne walichotwa kutoka Azam. Aishi Manula, Shomari Kapombe, Erasto Nyoni na John Bocco. Hapa kuna mambo mawili. Kwanza ni Simba iliimarika, halafu hapohapo Azam ikapungua nguvu.

Hao wachezaji walikwenda moja kwa moja katika kikosi cha kwanza cha Simba. Hakuna utetezi ambao unaweza kuwapa Azam hata kama mikataba yao ilikuwa imekata roho pale Chamazi. Lazima upambane kuhakikisha wachezaji wako bora wanabakia klabuni.

Unapomruhusu Bocco aondoke ina maana unaruhusu mabao yaondoke. Kuna mshambuliaji gani wa Azam aliyefunga mabao kama ya Bocco pale Chamazi? Hakuna. Hapo hapo unajiuliza, walifikiria nini pindi waliposikia Emmanuel Okwi anarudi Msimbazi na bado wakawapelekea na Bocco?

Hao wawili walikwenda kuungana na Shiza Kichuya ambaye ni mwanaume mwenye umri wa kivulana. Katika misimu miwili iliyopita, Kichuya ndiye ambaye alikuwa anaipa Simba uhai kuliko akina Mavugo kwa maana ya kupambana na kutengeneza nafasi.

Azam ilitazamia vipi Simba isiwe ubingwa hata baada ya kuwapata Aishi, Kapombe, Erasto na Bocco kwa urahisi namna ile? Haijashangaza pamoja na Yanga kuwa wabovu msimu huu, lakini walau waliipa Simba nyakati ngumu za kuusaka ubingwa wao wa kwanza baada ya miaka mitano.

Matatizo ya Yanga yanaeleweka zaidi kuliko ya Azam. Yanga ilifika kileleni na ilipaswa kuanza kurudi chini. Kikosi chake cha miezi 32 iliyopita kilikuwa kimefika juu na kisingeweza kuwa juu zaidi. Kuna wachezaji kama Simon Msuva na Haruna Niyonzima wameondoka.

Kuna wachezaji wamekamatwa na umri. Mfano mmojawapo ni Thabani Kamusoko. Sina uhakika sana kama hata akiwa fiti kama ataweza kurudi kutuonyesha kile alichokuwa anakionyesha katika miezi ya mwanzo ya mkataba wake na Yanga.

Bahati mbaya kwa Yanga ni kwamba tajiri wao aliondoka na hawakuweza kuziba mapengo ya wachezaji hawa kwa kuleta wachezaji wengine wenye umri ule ule. Raphael Daud sio Kamusoko. Pato Ngonyani sio Kamusoko.

Baada ya yote haya, kwanini Simba wasichukue ubingwa? Baada ya wapinzani wako kufika mwisho, baada ya Azam kukuipa wanaume wanne, baada ya maeneo mengine Simba kutumia pesa na kununua wachezaji wenye ubora kama Asante Kwasi, kwanini Simba wasiwe mabingwa? Ingeshangaza.

Wakati mwingine ni vizuri kumpata bingwa anayestahili ili walau tusihoji kuhusu ubora wa soka wa letu. Kwa mfano, pale England kama Pep Guardiola asingekuwepo Man City kuna uwezekano mkubwa Manchester United angechukua ubingwa wa England. Sidhani kama angekuwa bingwa anayestahili.

Simba ilistahili kuwa bingwa kwa heshima ya ligi yetu. Kwa vyovyote vile Kama Azam na Yanga zingeuiba kuwa mabingwa katika mikono ya Simba, na kwa jinsi vikosi vyao vilivyoundwa msimu huu, basi ingeshangaza sana.