Zaza apiga hat trick Valencia ikiiua Malaga 5-0

Muktasari:

Zaza jana usiku katupia nyavuni mabao matatu 'hat trick' ndani ya dakika tisa tu Valencia ikiibuka na ushindi wa mabao 5-0 dhidi ya Malaga katika mchezo wa La Liga katika uwanja wao wa nyumbani wa Mestalla.

Unamkumbuka Simone Zaza, yule mshambuliaji aliyekuwa akikipiga zamani West Ham kabla ya kuondoka na kujiunga na Valencia. Basi unaambiwa jamaa huko Hispania kawa moto balaa.
Zaza jana usiku katupia nyavuni mabao matatu 'hat trick' ndani ya dakika tisa tu Valencia ikiibuka na ushindi wa mabao 5-0 dhidi ya Malaga katika mchezo wa La Liga katika uwanja wao wa nyumbani wa Mestalla.
Karamu hiyo ya mabao ilianza kufunguliwa na Santi Mina dakika ya 17, kabla ya muitaliano huyo, Zaza kufunga hat trick hiyo kati ya dakika ya 54 hadi 63, kisha Rodrigo kumaliza hesabu baada ya kumalizia pasi murua kutoka kwa Goncalo Guedes katika dakika ya 86 na kuifanya Valencia kuibuka na ushindi huo mnono.
Kwa ushindi huo, Valencia imepanda katika msimamo wa La Liga hadi nafasi ya tatu, ikiachwa nyuma kwa pointi sita na vinara Barcelona.