#WC2018: Zamu ya nani kule Russia?

JINA lililokuwa maarufu kwenye fainali za Kombe la Dunia 2014 lilikuwa James Rodriguez.

Umahiri wake kwenye fainali hizo uliwafanya hata watu kuanza kufundishwa namna ya kulitamka jina la staa huyo wa Colombia, kwamba ukitaka kutamka jina lake la ‘James’ basi unapaswa kusema ‘Ha-mess’.

Kipindi anatamba katika fainali hizo zilizofanyika kwenye ardhi ya Wabrazili, alikuwa akikipiga kwenye kikosi cha AS Monaco ya Ufaransa, ambayo yenyewe ilikuwa imemsajili kutoka FC Porto. Asikwambie mtu, wakala wake Jorge Mendez alitumia fursa hiyo ya kung’ara kwenye Kombe la Dunia na kwenda kumpiga bei kwa pesa ndefu huko Real Madrid.

Sasa ni miaka minne imepita na fainali nyingine za Kombe la Dunia zimefika, ambazo zitaanza mwezi ujao huko Russia. Kinachosubiri huko Russia ni kuona itakuwa zamu ya wakali gani kuiteka dunia kama alivyofanya Rodriguez huko Brazil?

Hata hivyo, James Rodriguez hakuwa mchezaji pekee aliyetoboa katika fainali hizo za Kombe la Dunia 2014 baada ya kuwapo na wengine kadhaa, ambao baada ya kukamilika kwa michuano hiyo walinasa dili za maana mezani. Wachezaji waliotoboa Kombe la Dunia 2014.

Keylor Navas (Costa Rica): Ubora wa Keylar Navas akiwa na kikosi chake cha Costa Rica ulimpa dili la kunaswa na klabu kubwa kabisa Ulaya, Real Madrid.

Los Blancos ilinogewa na Navas na kutoa Pauni 10 milioni kunasa saini yake baada ya kufikisha Costa Rica robo fainali huko Brazil.

David Ospina (Colombia): Kipa mwingine aliyefanya kweli kwenye fainali hizo za Brazil, lakini yeye alikuwa kwenye kikosi cha Colombia. Ospina alisimama imara kabisa golini na kuifikisha Colombia nusu fainali na baada ya hapo, Arsenal ikaenda kutoa pesa kumsajili kwa Pauni 3 milioni.

Antoine Griezmann (Ufaransa): Kipindi hicho, Griezmann hakuwa na jina kabisa. Lakini, alicheza vizuri japo Ufaransa haikufika mbali sana katika fainali hizo za Brazil. Lakini, kiwango chake kilimfanya anaswe na Atletico Madrid kwa Pauni 30 milioni ikimtoa Real Sociedad.

Marcos Rojo (Argentina):

Baada ya kusimama vizuri kabisa kwenye safu ya mabeki wa Argentina katika fainali hizo, klabu kibao za Ulaya zilihitaji huduma yake na hatimaye Manchester United ilipiga bao baada ya kumnasa Rojo kwa Pauni 16 milioni akitokea Sporting CP ya Ureno.

James Rodriguez (Colombia): Baada ya Radamel Falcao kuumia na kushindwa kwenda kwenye fainali hizo, Colombia ilimpa majukumu James Rodriguez na hakika hakuwaangusha waliomwamini baada ya kuifikisha timu hiyo nusu fainali huku akiibuka mfungaji bora na kupata dili la kwenda kujiunga na Real Madrid kwa Pauni 65 mil. akitokea Monaco.

Pakua HAPA jarida letu la #KombelaDunia2018 la WIKI HII linaloletwa kwako na magazeti uyapendayo ya MWANANCHI na MWANASPOTI.