Willin presha inapanda, inashuka huko Chelsea

Muktasari:

Mbrazili huyo alitibuana na kocha wa zamani wa The Blues, Antonio Conte msimu uliopita na kudai ataondoka, lakini hata baada ya kuja kocha mpya mchezaji huyo bado ameshikilia mpango wake wa kutaka kuipa kisogo Stamford Bridge.

LONDON, ENGLAND. WILLIAN anaamua tu kumkosesha raha kocha wake mpya wa Chelsea, Maurizio Sarri baada ya kudai mpango wake wa kuachana na timu hiyo bado upo palepale.

Mbrazili huyo alitibuana na kocha wa zamani wa The Blues, Antonio Conte msimu uliopita na kudai ataondoka, lakini hata baada ya kuja kocha mpya mchezaji huyo bado ameshikilia mpango wake wa kutaka kuipa kisogo Stamford Bridge.

Kuwasili kwa Sarri kumebadili ari ya wachezaji kwenye kikosi hicho na kutarajia mambo yatakuwa mazuri, lakini kwa sasa kila kitu kinaonekana kuyumba kutokana na sehemu kubwa ya wachezaji waliokuwa muhimu msimu uliopita kutangaza wanataka kuhama.

Eden Hazard na Thibaut Courtois wameshaweka wazi dhamira yao ya kutaka kuondoka na Willian sasa anataka kufungasha virago vyake na kuondoka kwenye timu hiyo.

Siku si nyingi sana, Willian alikuwa akihusishwa na Manchester United ambako Kocha Jose Mourinho alikuwa akimhitaji winga huyo kuja kuongeza nguvu kwenye kikosi chake huko Old Trafford.

Willian alionekana kufurahishwa na kitendo cha Mbrazili mwenzake, Fred kwenda kujiunga na Man United akielezea ni moja ya klabu kubwa kabisa duniani na hapo inaweza isiwashangaze watu kama atalazimisha kuhamia Old Trafford.

Timu nyingine iliyoonyesha dhamira ya kuhitaji huduma ya Willian ni Barcelona, ambayo pia akienda atakwenda kukutana na Mbrazili mwenzake, Philippe Coutinho, aliyenaswa kwenye dirisha la Januari akitokea Liverpool.

Kama Real Madrid itakamilisha usajili wake kwa mastaa Courtois na Hazard kisha Willian akaondoka, basi Sarri atakuwa kwenye wakati mgumu kwelikweli kuwapoteza wakali wake hao wa kikosi cha kwanza.