Wenger amtaja mrithi wake Arsenal

LONDON, ENGLAND

SI unajua mabosi wa Arsenal kwa sasa wanakuna vichwa kumtafuta kocha wa kuja kumrithi Arsene Wenger? Basi Wenger mwenyewe hataki kulifanya jambo hilo kuwa gumu, baada ya kuwatajia mabosi hao mtu ambaye anadhani anafaa kwenye kurithi mikoba yake huko Emirates.

Wenger ameripotiwa kumtaja staa wa zamani wa Arsenal, Giovanni van Bronckhorst anafaa kwenda kuwa kocha wa timu hiyo baada ya wakati wake kufika tamati.

Kocha huyo Mfaransa alisaini mkataba wa miaka miwili wa kuendelea kuinoa timu hiyo Mei, lakini amefichua atajifanyia tathmini mwishoni mwa msimu kama kweli anapaswa kuendelea kubaki au kupisha wengine kufanya mabadiliko katika timu.

Van Bronckhorst, 42, anaifundisha Feyenoord na Wenger alisema anakoshwa na staili ya Van Bronckhorst na namna alivyowaongoza Feyenoord kubeba ubingwa wao wa ligi baada ya miaka 18. Mabosi wa Arsenal wanasikiliza maoni ya Wenger juu ya mtu wa kumrithi.