Wenger Kwa hiki alichoamua hakuna wa kumpinga

Muktasari:

Ni uamuzi uliokuja baada ya malalamiko mengi kutoka kwa washabiki, baadhi wakitaka aachie ngazi tangu mwaka juzi, timu ilipoanza kufanya vibaya.

ARSENE Wenger ameamua kuondoka Arsenal baada ya kuhudumu kwa miaka 22. Anaondoka akiwa bado na kandarasi ya mwaka mmoja, kwa vile alisaini mkataba mpya wa miaka miwili mwaka jana.

Ni uamuzi uliokuja baada ya malalamiko mengi kutoka kwa washabiki, baadhi wakitaka aachie ngazi tangu mwaka juzi, timu ilipoanza kufanya vibaya.

Anaondoka baada ya jitihada mbalimbali za mashabiki, ikiwa ni pamoja na maandamano, kuweka mabango ya ‘Wenger Out’ na ndege kupita juu ya dimba lao zikiacha ujumbe huo huo.

Hata hivyo, kubwa na la mwisho ni mashabiki, hasa wale wakubwa wanaonunua tiketi za msimu mzima kugoma kwenda uwanjani Emirates na viti vingi kubaki wazi.

Ni kweli amekaa muda mrefu na hakuna ubishi ni ngumu kufikiria mtu mpya kwenye nafasi yake pale kwenye benchi la ufundi. Alizoeleka sana hapo, maana miaka 22 si muda mfupi na baadhi ya mashabiki wa Arsenal hawakuwa wamezaliwa alipoanza kuiongoza klabu hiyo.

Ndiyo maana majuzi watoto waliweka bango likisema; ‘Sisi bado ni watoto wadogo lakini baba wametuambia makubwa uliyowafanyia Arsenal. Kwa heri babu’.

Wapo watu wanaoona tabu kuondoka kwa Mfaransa huyu wakirejea ile kauli ya zimwi likujualo, halikuli likakwisha, na wengine wakifananisha na Uingereza kuamua kuondoka Umoja wa Ulaya (EU).

Sasa yanazungumzwa juu ya nani atachukua mikoba yake, wakitajwa wachezaji wa zamani hapo Arsenal, Patrick Vieira, Thierry Henry na Mikel Arteta sambamba na kocha wa zamani wa Borussia Dortmund, Thomas Tuchel, Kocha wa Juventus, Massimiano Allegri, wa Celtic, Brendan Rogers na wa Timu ya Taifa ya Ujerumani, Joachim Low.

Wenger ameamua vyema kwa sababu aliongoza klabu miaka 20 wakiwa katika Ligi ya Mabingwa Ulaya (UCL) lakini msimu jana na huu wameshindwa, kwa maana hawakufanikiwa kuwa kwenye timu nne bora za juu katika Ligi Kuu England (EPL).

Wenger alitawala hasa, akawa ni kana kwamba ni kila kitu Arsenal na akawa hasimu mkubwa kwa baadhi ya makocha kama Alex Ferguson wa Manchester United enzi hizo na Jose Mourinho wa sasa, wote wakisema kuwa bwana huyo sasa ni rafiki yao wala hawana tatizo naye.

Fergie amefika mahali na kusema kwamba amefurahishwa sana na hatua aliyofikia Wenger na uamuzi wake kwa sababu ni makubwa na mengi aliyowafanyia Arsenal tangu 1996.

Mourinho naye anampongeza Wenger, akisema ni rafiki yake na asingekuwa anamheshimu wasingeweza kuwa mahasimu. Anasema ikiwa Wenger amechukua uamuzi huo kwa raha, naye anafurahi naye. Mashabiki wa Arsenal sasa watakuwa wanamsubiri kwa hamu kocha mpya.