Wapo 7 tu spesho,Lukaku na Lacazette hawahusiki

Muktasari:

Vita iliyobaki kwa sasa ni ya kusaka Top Four, ambayo inahusu timu za Man United, Liverpool, Tottenham na Chelsea.

LONDONENGLAND. LIGI Kuu England bingwa ndo hivyo keshapatikana, Manchester City. Man City wametangaza ubingwa wiki iliyopita baada ya Manchester United kukutana na kichapo cha bao 1-0 kutoka kwa West Brom, kipindi ambacho kimewafanya hata washinde mechi zote wasingeweza kufikia pointi za wakali hao wanaonolewa na Pep Guardiola.

Vita iliyobaki kwa sasa ni ya kusaka Top Four, ambayo inahusu timu za Man United, Liverpool, Tottenham na Chelsea.

Vita nyingine ni ile ya kujinusuru na balaa la kushuka daraja. Lakini, kushinda vita hizo unahitaji kushinda mechi na kushinda mechi unahitaji kufunga mara nyingi kwenye mechi kuliko mpinzani wako. Jambo hilo limefanya kupatikana wakali wa kupiga nyingi kwenye mechi moja kwenye Ligi Kuu England msimu huu.

Hawa hapa wakali waliofunga mara tatu katika mechi moja ya ligi msimu huu, yaani hat-trick na kwa taarifa yako, wapo wachezaji saba tu waliofanya hivyo kwa msimu huu matata. Kitu kinachovutia, mastraika walionaswa kwa pesa nyingi huko Arsenal, Alexandre Lacazette na huko Man United, Romelu Lukaku, hawapo. Hawahusiki.

7. Callum Wilson- Hat-trick 1

Fowadi huyo wa Bournemouth, Callum Wilson Jumatano iliyopita aliwapa wakati mgumu sana mabeki wa Man United, Phil Jones na Chris Smalling, licha ya kwamba hakufanikiwa kutikisa nyavu siku hiyo na Man United ilishinda 2-0, shukrani kwa mabao ya Smalling na Romelu Lukaku. Lakini, Novemba 18 mwaka jana, kwenye mechi dhidi ya Huddersfield, Wilson alipiga hat-trick wakati Cherries iliposhinda 4-0 kwenye Uwanja wa Vitality.

6. Alvaro Morata- Hat-trick 1

Mashabiki wa Chelsea walikuwa kwenye furaha kubwa wakati straika wao mpya, Alvaro Morata alipopiga hat-trick yake ya kwanza akiwa na jezi za wababe hao wa Stamford Bridge.

Baada ya kutua tu kwenye kikosi hicho cha Chelsea, Morata alihitaji mwezi mmoja tu kupiga bao tatu katika mechi moja, ambapo alifanya hivyo Septemba 23 mwaka jana kwenye mechi dhidi ya Stoke City. Morata alifunga bao la kwanza dakika ya pili yay a mchezo na bao lake la tatu alifunga kwenye dakika 82 kukisaidia kikosi hicho cha Antonio Conte kushinda 4-0 ugenini.

5. Aaron Ramsey- Hat-trick 1

Kiungo mchezeshaji wa Arsenal, Aaron Ramsey alikuwa moto kweli kweli, Februari 3, mwaka huu kwenye mechi dhidi ya Everton. Staa huyo wa kimataifa wa Wales alipiga hat-trick matata ndani ya dakika 68 kuisaidia Arsenal kushinda 5-1 huko Emirates.

Ilikuwa furaha kubwa kwa mashabiki siku hiyo, lakini mambo yao kwenye msimu katika michuano hiyo ya Ligi Kuu England hayapo vizuri kwa sababu wanashika nafasi ya sita na wanaweza kumaliza kwenye nafasi hiyo hiyo kwenye msimamo labda kama muujiza utokee.

4. Wayne Rooney- Hat-trick 1

Fowadi wa Everton, Wayne Rooney naye ni moja kati ya wale spesho waliopiga hat-trick kwenye Ligi Kuu England msimu huu. Staa huyo wa zamani wa Man United alifunga mabao matatu kwenye mechi moja wakati Everton ilipocheza na West Ham. Mechi hiyo ilipigwa Novemba 29 mwaka jana uwanjani Goodison Park. Katika mechi hiyo, Rooney alifunga kwa staili kubwa ikiwamo bao lake alilofunga akiwa katikati ya uwanja. Bao hilo liliwafanya mashabiki uwanja mzima kusimama kumshangilia na hakika lilishinda tuzo ya bao bora la mwezi Novemba.

3. Mohamed Salah- Hat-trick 1

Kwa msimu huu, kwenye Ligi Kuu England, staa wa Liverpool, Mohamed Salah ndiye kinara wa mabao akiwa ametupia wavuni mara 31 na hakika Kiatu cha Dhahabu cha kwenye ligi hiyo kinamhusu msimu huu. Lakini, katika mabao yote hayo, Salah alifunga mara moja tu mabao matatu katika mechi moja ya ligi na hiyo ilikuwa Machi 17 mwaka huu, wakati Liverpool ilipokipiga na Watford. Hakika siku hiyo, Watford walishindwa kabisa kumdhibiti Salah na alipiga bao lake la tatu katika dakika ya 73. Siku hiyo Salah alifunga mabao manne pekee yake.

2. Harry Kane- Hat-trick 2

Straika wa Tottenham Hotspur, Harry Kane amekuwa akimfukuzia Mohamed Salah kwenye mbio za Kiatu cha Dhahabu, lakini kwa hali ilivyo kwa sasa, mbio hizo zinaonekana kuelekea kumshinda. Kwa sasa amefunga mabao 26, matano nyuma ya mpinzani wake huyo. Lakini, kwa msimu huu Kane amekuwa kwenye ile orodha ya watu spesho waliopiga hat-trick Ligi Kuu England, Mwingereza huyo alifanya hivyo mara mbili katika mechi mfululizo, dhidi ya Burnley, alifunga mabao yote kwenye mechi hiyo na nyingine ni ushindi wa 5-2 dhidi ya Southampton uwanjani Wembley.

1. Sergio Aguero- Hat-trick 3

Kinara wa mabao wa nyakati zote huko Manchester City, Sergio Aguero ndiye mchezaji aliyepiga hat-trick nyingi zaidi Ligi Kuu England msimu huu. Muargentina huyo ametupia hat-trick tatu. Dhidi ya Watford Septemba 16 mwaka jana wakati timu yake iliposhinda 6-0, dhidi ya Newcastle United, Januari mwaka huu na dhidi ya Leicester City, Februari 10 mwaka huu wakati Man City iliposhinda 5-1. Katika mechi hiyo alihitaji dakika 29 tu kukamilisha hat-trick yake.