Wanatumia pesa hadi kufuru unaambiwa

WASWAHILI wana msemo wao huo, tumia pesa ikuzoee. Basi kama hivyo ni kweli, kuna wanasoka hao wameshindikana kwenye kutumbua pesa zao kwa kufanya matumizi makubwa kuliko kawaida.

Lakini unapokuwa na pesa nyingi matumizi ni jambo ambalo ni kama linashabihiana na hawa ndio mastaa watano wa soka, ambao ni matata kwenye kutumia pesa.

5.Cristiano Ronaldo

Cristiano Ronaldo ni tajiri na analifahamu hilo. Kwa taarifa tu, supastaa huyo wa Kireno hayupo kabisa kwenye hatari ya kufilisika kwa kipindi cha karibuni. Kinachoripotiwa ni kwamba anavuna Dola 40 milioni kila mwaka kwa malipo ya mishahara yake na mapato mengine ya dili za kibiashara.

Unapokuwa tajiri kama Ronaldo, basi unahitaji kutumia pesa yako. Ronaldo hamalizi kununua magari ya kifahari, majumba na kwa mwezi anatumia Pauni 8,000 kwenye mavazi tu. Asikwambie mtu, Ronaldo anajua kutumia pesa bana.

4.Zlatan Ibrahimovic

Kwa mbwembwe zake ingekuwa kitu cha kushangaza kama asingekuwapo kwenye orodha hii ya watumiaji. Zlatan Ibrahimovic amenunua jumba la ghorofa nne huko Stockholm ambalo ni kanisa. Akilinunua kwa Dola 1.7 milioni, Ibrahimovic alilibadili na kulijenga kufanya kuwa nyumba za makazi ya watu. Staa huyo pia ni mtumwa wa magari ya kifahari, ndiyo maana anayo kibao tu, huku akiwa na pikipiki ya Hailey Davidson, ambayo imemgharimu Dola 870,000. Ibrahimovic anataka kuwa na kipindi chake cha televisheni kionyeshwe huko Marekani.

3.Neymar Jr.

Mwanasoka anayelipwa mshahara mkubwa na kijana ambaye ameingia kwenye orodha hiyo ya watu wasiobahiri kwenye kutumia. Neymar ana magari kibao ya kifahari ikiwamo Porsche Panamera Turbo ambazo gharama yake ni kati ya Dola 400,000 hadi 550,000.

Ana hekalu la Dola 2 milioni na mjengo matata kabisa huko Brazil wenye thamani ya Dola 950,000. Hapo hujasema jengo alilopanga huko Paris. Neymar anamiliki boti yake yenye thamani ya Dola 8 milioni, ambayo inamgharimu Dola 230,000 kila mwaka kwa ajili ya kuifanyika matengenezo. Alitumia pia Dola 1 milioni kununua jumba analoishi mpenzi wake wa zamani, ambaye ni mzazi mwenzake na anatumia Dola 30,000 kwa mwezi kwa ajili ya mtoto. Hapo hujasema starehe zake nyingine.

2.Obafemi Martins

Mnigeria, Obafemi Martins alikuwa akiingiza Dola 115,000 kwa wiki alipokuwa kwenye kikosi cha Newcastle United na iliripotiwa alikuwa akitumia pesa hizo kwa siku chache tu.

Kununua magari ya kifahari, kula vyakula matata, kulala kwenye hoteli za kifahari na kuwa na wanawake kila anapokwenda, ilikuwa moja ya matumizi ya mshambuliaji huyo.

Moja ya magari yake ni Porshe Cayenne lenye thamani ya Dola 130,000 na alikuwa akiishi kwenye makazi matata kabisa huko England, akipanga kwenye Jiji la Newcastle, huku akienda kupata mlo kwenye migahawa ya thamani ya juu kila wiki.

1.Mario Balotelli

Mario Balotelli amekuwa mtu wa kutumia pesa nyingi sana japo watu hawalioni hilo.

Staa huyo alitumia Dola 250,000 kwenye kuibadilisha gari yake ya Bentley kuwa na rangi ya magwanda ya kijeshi.

Kuna wakati alijifanya amesahau gari yake ameegesha wapi, hivyo kuepukana na suala la kurudi kwenda kuifuata ilipo, akaamua kumpa tu mchezaji mwenzake bure kabisa.

Mwaka 2011, alikuwa akiegesha gari lake popote pale alipoona inafaa kufanya hivyo na kujikuta akikatwa Dola 15,000 na maegesho na alifanya hivyo zaidi ya mara 27 hakujali makato.