Messi aibeba Argentina kibabe!

Quito, Ecuador. Lionel Messi amerejesha matumaini ya Argentina kucheza Fainali za Kombe la Dunia, baada ya kufunga mabao matatu 'hat trick' dhidi ya Ecuador.
Argentina ikiwa ugenini ikicheza katika mazingira magumu kutokana na hali ya hewa ya Equador, ilitoka nyuma na kupata ushindi wa mabao 3-1 ugenini.
Endapo Argentina ingeshindwa kushiriki fainali hizo ingekuwa imeingia katika rekodi mpya ya kutocheza tangu mwaka 1970.
Mchezo huo ulikuwa muhimu kwa Argentina kushinda. Kocha Jorge Sampaoli alikuwa na presha kubwa kutoka kwa mashabiki wa Argentina.
Argentina inashika nafasi ya tatu katika msimamo wa kundi ikiwa na pointi 28 nyuma ya vinara Brazil na Uruguay.
Ecuador ilianza kutoa presha kwa wageni, baada ya mchezaji Romario Ibarra kufunga bao dakika ya 40 kabla ya Messi kupiga mabao matatu ugenini.
Mashabiki wa Argentina walikuwa wakitoa matamshi makali kuhusu timu yao kucheza fainali hizo baada ya kuboronga katika mechi zake za awali.
Lakini, Messi juzi usiku aliwaziba mdomo kwa kufunga mabao matatu dakika 12, 20, 62 na kuipeleka Argentina katika fainali hizo zilizopangwa kuchezwa mwakani nchini Russia.