Veterani Dallas akubali yaishe, apisha madogo

Muktasari:

  • Nyota huyo ambaye alisaini kuendelea kuichezea timu hiyo msimu uliopita, anaitafuta rekodi ya kipekee ya kuwa nyota wa kwanza wa kimataifa wa NBA kucheza kwa misimu 21 mfululizo na atafikisha poiti 30,000 tangu aanze kucheza ligi hiyo.

KUBALI yaishe. Ndio, nyota veterani wa Dallas Mavericks, Dirk Nowitzki ameweka wazi msimu ujao hatakuwa na namna zaidi ya kulizoea benchi ili tu kupisha damu changa.

Nyota huyo ambaye alisaini kuendelea kuichezea timu hiyo msimu uliopita, anaitafuta rekodi ya kipekee ya kuwa nyota wa kwanza wa kimataifa wa NBA kucheza kwa misimu 21 mfululizo na atafikisha poiti 30,000 tangu aanze kucheza ligi hiyo.

Nowitzki (40), alikiri kwa sasa hana maajabu tena kwenye mchezo, baada ya kubeba taji hilo kubwa na kupata tuzo ya heshima ya kuwa mchezaji mwenye thamani zaidi katika msimu wa kawaida ‘Regular Season’ na sasa hana budi kupisha wachezaji wapya kupata nafasi ya kuonyesha vipaji vyao.

Mjerumani huyo katika misimu 20 aliyoichezea Mavericks amefanikiwa kuanza kikosi cha kwanza kwenye mechi 1140, katika mechi zaidi ya 1471 na amefanikiwa kutajwa katika kikosi cha wachezaji wa All-Star mara 13.