VIDEO: Rafu zinauma jamani sijiangushi: Neymar

Muktasari:

Neymar amegeuzwa kituko kwenye fainali za Kombe la Dunia 2018 akidaiwa amekuwa mwigizaji sana kwa kujiangusha kila anapoguswa tu na mabeki wa timu pinzani, jambo linalomfanya awe gumzo kwenye mitandao ya kijamii watu wakimkejeli.

PARIS, UFARANSA. SUPASTAA Neymar amefunguka kwa wanaomsema anajiangusha hawajui walisemalo kwa sababu hawana uelewa wa yale anayokumbana nayo ndani ya uwanja.

Neymar amegeuzwa kituko kwenye fainali za Kombe la Dunia 2018 akidaiwa amekuwa mwigizaji sana kwa kujiangusha kila anapoguswa tu na mabeki wa timu pinzani, jambo linalomfanya awe gumzo kwenye mitandao ya kijamii watu wakimkejeli.

Lakini mwenyewe amedai hajifanyishi, bali amekuwa akipigwa mateke na kuchezewa rafu na mabeki wa timu pinzani na kile anachokifanya si mzaha.

“Mnadhani napenda kufanya vile kila wakati? Hapana, ni maumivu, inauma sana,” alisema mwanasoka huyo ghali duniani.

“Baada ya mechi nimekuwa nikitumia saa nne hadi tano kujikanda na barafu, ni mambo magumu, lakini watu hawaelewi. Naziona kejeli zao, nazichukulia tu kama vichekesho.”

Neymar alikabiliwa na wakati mfupi wa kupona majeraha yake ya kuvunjika mguu Februari ili kuwahi fainali za Kombe la Dunia 2018 jambo ambalo lilitimia licha ya kwamba hakwenda kuwa kwenye makali yake katika fainali hizo za Russia.4