Conte apoteza matumaini ya ubingwa kwa Man City

Muktasari:

Baada ya timu hiyo kuchapwa bao 1-0 na West Ham katika mchezo uliopita, Conte alisema matumaini ya kutetea ubingwa yameyeyuka huku akiipa nafasi Manchester City.

London, England. Kocha Antonio Conte amewapuuza wabaya wake wanaomkosoa kuhusu mwenendo wa timu ya Chelsea katika mashindano ya Ligi Kuu England msimu huu.
Baada ya timu hiyo kuchapwa bao 1-0 na West Ham katika mchezo uliopita, Conte alisema matumaini ya kutetea ubingwa yameyeyuka huku akiipa nafasi Manchester City.
“Kila kona watu wanaizungumzia vibaya Chelsea. Ni kweli vigumu kuizungumzia kutwaa ubingwa mbele ya timu bora kama Manchester City,”alisema Conte.
Hata hivyo, ushindi wa juzi umefufua matumaini ya kutoa upinzani katika mchuano huo msimu huu licha ya kukabiliana na Man City inayopewa nafasi ya kutwaa ubingwa.
Mtaliano huyo alisema watu wamekuwa wakiisema vibaya Chelsea, lakini hatajali na ataendelea na harakati za kutoa ushindani katika mashindano hayo.
Pia kocha huyo alisema ushindi wa jana Jumanne umetokana na kazi nzuri ya kiwango wa kimataifa wa Ufaransa Tiemoue Bakayoko.
Bakayoko alifunga bao la kwanza dhidi ya Huddersfield na kucheza kwa kiwango bora mchezo ambao Chelsea ilikuwa ugenini. Katika mchezo na West Ham, Bakayoko alicheza chini ya kiwango.
“Amenionyesha jinsi gani alivyojiandaa kubadilika. Nilimpanga kwa kuwa hakucheza vibaya sikuona sababu kwanini asianze,”alisema Conte akimzungumzia Bakayoko aliyetua Chelsea majira ya kiangazi kutoka Lyon.