Urafiki uliishia huko, hapa ni kazi tu

Muktasari:

Hii hapa orodha ya wachezaji marafiki walioshibana, ambao kwenye fainali za Kombe la Dunia huko Russia wameenda kuwa wapinzani wakubwa kwa sababu kila mmoja ana timu yake ya taifa.

MOSCOW, RUSSIA. UPINZANI wa ndani ya uwanja kwenye mchezo wa soka unaufanya mchezo huo kuwa na mvuto zaidi, lakini kwa wachezaji kuwa marafiki walioshibana ni jambo linalofanya mchezo huo kupendwa zaidi.

Hii hapa orodha ya wachezaji marafiki walioshibana, ambao kwenye fainali za Kombe la Dunia huko Russia wameenda kuwa wapinzani wakubwa kwa sababu kila mmoja ana timu yake ya taifa.

5.Mohamed Salah na Sadio Mane

Kwenye uhusiano wao wakiwa timu moja katika klabu ya Liverpool, Mohamed Salah alizungumzia urafiki wake na Sadio Mane aliposema:

“Tangu siku ya kwanza nilipojiunga na Liverpool, uhusiano wangu na Sadio umekuwa mzuri kwelikweli. Tumekuwa marafiki wa karibu na tunasaidiana kufikia mafanikio sisi binafsi pamoja na timu.”

Lakini, jambo baya ni kwamba marafiki hao hawapo pamoja kwenye fainali za Kombe la Dunia huko Russia, Salah akiwa na Misri na Mane akiwa kwenye kikosi cha Senegal. Wakati Salah na timu yake Misri akifungwa kwenye mechi zote mbili, Mane ameanza vizuri baada ya kushinda mechi ya kwanza na hivyo kuwa na matumaini ya kufanya vizuri katika fainali hizo za Russia. Mashabiki wanakosa utamu wa kuwashuhudia wakali hao wakicheza timu moja.

4.Lionel Messi na Luis Suarez

Pengine hujawahi kuwaza kama wachezaji wawili wanaocheza nafasi moja, tena ya ushambuliaji wanakuwa marafiki wazuri. Basi hilo kwa Luis Suarez na Lionel Messi halijawahi kuwa jambo gumu.

Suarez alizungumzia urafiki wake na Messi: “Kwenye soka ni ngumu sana kuwa na rafiki wa kweli, hasa yule ambaye mtacheza nafasi moja. Siku zote lazima chuki iiingie kati yake, lakini hilo ni tofauti kwangu mimi na Messi pale. Hakuna wivu kabisa na tumekuwa tukishiriki mambo yetu pamoja kama marafiki ndani na nje ya uwanja.”

Uhusiano huo uliwafanya Suarez na Messi kutengeneza kombinesheni matata kabisa katika safu ya ushambuliaji ya Barcelona na kuwa tishio ikiwa inafunga mabao yanayofanya timu hiyo kubeba mataji.

Kwa bahati mbaya, kwenye fainali za Russia, Messi yupo na Argentina na Suarez anaichezea Uruguay. Maswahiba hao, mmoja hali yake ni mbaya, mwingine mambo yake ni mazuri.

3. Cristiano Ronaldo na Marcelo

Ni tukio lililotokea mara chache sana kwa Cristiano Ronaldo afunge bao huko Real Madrid kisha ashangilie bila ya swahiba wake, Marcelo kuwapo kwenye tukio hilo.

Wawili hao ni marafiki wakubwa sana na wanapokutana utani umekuwa mwingi sana.

Hata wanapokuwa mazoezini wamekuwa wakitaniana sana ukiweka kando kushangilia mabao yao uwanjani pamoja.

Lakini kwenye fainali hizo za Russia marafiki hao kila mmoja ana mambo yake.

Mmoja Ronaldo yupo na Ureno, wakati mwingine Marcelo anakipiga kwenye kikosi cha Brazil. Hakuna mwenye mambo matamu sana kwenye fainali hizo jambo ambalo linamfanya kila mmoja kupambana kuhakikisha timu yake inafanya vizuri na kuibuka na ushindi.

Kwa jambo hilo uswahiba utawekwa kando kama wakali hao wawili wa Bernabeu watakutana kwenye moja ya mechi katika fainali hizo za Russia.

2. Paul Pogba na Romelu Lukaku

Watu wengi wamekuwa wakiufahamu urafiki wa Paul Pogba na Romelu Lukaku kwa siku za karibuni, lakini ukweli ni kwamba wawili hao wamekuwa marafiki kwa muda mrefu sana.

Wamekuwa wakifuatana hata kipindi ambacho Pogba alikuwa Juventus na mwingine Lukaku akiwa Everton kabla ya kuja kukutana pamoja kwenye kikosi cha Manchester United na kuendelea urafiki wao.

Lakini kwenye fainali za Kombe la Dunia urafiki wao hautakuwapo kwa sababu mmoja, Lukaku anakipiga kwenye kikosi cha Ubelgiji na mwingine, Pogba anaichezea Ufaransa.

Timu hizo mbili kila moja inapewa nafasi ya kuchukua ubingwa na hilo ndilo litakalofanya kwamba Lukaku na Pogba timu zao zitakapokutana, basi kila mmoja atahitaji kushinda kuisaidia timu yake, hapo ushkaji utawekwa kando kwa ajili ya manufaa ya taifa kwa kila mmoja.

1.Mesut Ozil na Sergio Ramos

“Nilikuwa na nyakati nzuri sana pale Real Madrid,” alisema supastaa wa Arsenal, Mesut Ozil na kuongeza.

“Nilikuwa na uhusiano mzuri pia na wenzangu. Rafiki yangu mkubwa alikuwa Sergio Ramos, bado tunawasiliana hadi sasa. Nilipokuwa Madrid, Ramos alikuwa akiishi barabara moja na tulifanya mengi sana. Alinionyesha Madrid na alinisaidia kuzoea mazingira kwa haraka.”

Hayo ni maneno ya Ozil, akimzungumzia Ramos, ambaye walikuwa pamoja Real Madrid kabla ya kuondoka kwenda Arsenal na wawili hao bado wapo na uhusiano mzuri.

Kwenye fainali za Kombe la Dunia huko Russia haitarajiwi wawili hao kama wataendelea kuwa marafiki wazuri hasa ukizingatia wapo kwenye timu tofauti. Ozil yupo kwenye kikosi cha Ujerumani na Ramos ni beki wa Hispania.

Urafiki wao utavunjika kwa muda kama timu zao zitakutana kwenye fainali za Kombe la Dunia kwa sababu hapo kitakachotazamwa ni utaifa kwanza.