Sikia hii, usajili England majanga

Muktasari:

Mabadiliko ya kufunga dirisha la usajili kabla ya msimu mpya wa ligi haujaanza, imedaiwa kuwavuruga wacheza kamari na hivyo mpango unaelezwa kuna ishu ya chinichini ya kuzisukuma klabu kupambana ili ilirudi kama zamani.

KLABU za Ligi Kuu England zimepanga kufanya mpango wa kuhakikisha dirisha la usajili wa majira ya kiangazi linarudi kama zamani kufungwa Agosti 31 baada ya kudai kile kilichotokea mwaka huu ni majanga.

Mabadiliko ya kufunga dirisha la usajili kabla ya msimu mpya wa ligi haujaanza, imedaiwa kuwavuruga wacheza kamari na hivyo mpango unaelezwa kuna ishu ya chinichini ya kuzisukuma klabu kupambana ili ilirudi kama zamani.

Kwa Ligi Kuu England, dirisha la uhamisho wa wachezaji katika majira ya kiangazi lilifungwa Agosti 9, jambo lililozua utata mkubwa huku klabu za ligi nyingine, ambazo ziliendelea kusajili hadi Agosti 31, zilikuwa bado zinaendelea kunasa wachezaji tena kwa bei rahisi kwa sababu timu za England zilikuwa haziruhusiwi tena kununua wachezaji.

Jambo jingine klabu hizo za England zinakuwa kwenye presha kubwa kuhusu wachezaji wao kuwindwa na klabu za nje na kama zitafanikiwa kuwasajili, wao watakuwa kwenye matatizo kwa sababu hawatakuwa na nafasi ya kusajili wa kuziba mapengo yaliyoachwa.

Kinachoelezwa klabu moja inapaswa kutoa pendekezo hilo kisha nyingine zitatoa michango yao kama zinaafiki au la, huku mjadala mzima wa jambo hilo ukidaiwa utazungumzwa ndani ya mwezi huu.