Sikia hii, eti Chris Smalling kamweka mfukoni Harry Kane

Muktasari:

Tangu fowadi huyo alipokata rufaa kutaka apewe bao ambalo awali lilionekana kufungwa na Christian Eriksen kwenye mechi ya Ligi Kuu England dhidi ya Stoke City ili kujiongezea mabao ya kumfukuzia Mohamed Salah kwenye vita ya Kiatu cha Dhahabu, amekuwa gumzo kwenye mitandao ya kijamii.

LONDON, ENGLAND . KAMA kuna kitu ambacho straika wa Tottenham Hotspur, Harry Kane anakiomba kwa sasa basi huu msimu umalizike haraka asubiri msimu ujao baada ya kuibuka kuwa kituko kwenye mitandao ya kijamii.

Tangu fowadi huyo alipokata rufaa kutaka apewe bao ambalo awali lilionekana kufungwa na Christian Eriksen kwenye mechi ya Ligi Kuu England dhidi ya Stoke City ili kujiongezea mabao ya kumfukuzia Mohamed Salah kwenye vita ya Kiatu cha Dhahabu, amekuwa gumzo kwenye mitandao ya kijamii.

Jambo hilo limechukua sura mpya baada ya FA nao kuhusika katika kumtania mshambuliaji huyo, ambaye anaichezea pia timu ya taifa ya England.

Baada ya mechi ya nusu fainali ya Kombe la FA kati ya Spurs na Manchester United iliyofanyika Wembley Jumamosi, FA ilituma ujumbe kwenye ukurasa wao wa Twitter, ambao ulikuwa kijembe cha moja kwa moja kwa straika Kane.

Katika mechi hiyo iliyomalizika kwa Man United kushinda 2-1, shukrani kwa mabao ya Alexis Sanchez na Ander Herrera, Kane ni kama hakuwapo uwanjani kwa jinsi alivyozimwa na mabeki wa United, hasa Chris Smalling, aliyekuwa amemganda kama kivuli.

Ukweli Kane hakufurukuta na FA walilitafsiri jambo hilo kama vile fowadi huyo aliwekwa mfukoni ya Smalling na kuamua kutwiti, video ya Smalling akitaja jina la “Harry Kane” iliyotanguliwa na swali la “Kitu gani kipo kwenye mfuko wako, Chris?”

Baada ya jambo hilo kudaiwa kuwakera Spurs, Chama cha soka cha England, FA kiliamua kuomba radhi kwa timu zote mbili kutokana na usumbufu wote uliojitokeza.

Kane ameshindwa kurudi kwenye ubora wake tangu aliporejea uwanjani kutoka kuuguza majeruhi na katika kipindi hicho amefunga mabao mawili tu, likiwamo hilo la rufaa.

Msemaji wa FA alisema: “Tumewaandikia klabu zote mbili tukiwaomba radhi kwa usumbufu wowote uliojitokeza.”

Kane anatarajiwa kwenda kuwa nahodha wa England wakati kikosi hicho cha Gareth Southgate kitakapokwenda kwenye fainali za Kombe la Dunia zitakazofanyika miezi miwili ijayo huko Russia.

Kitu kilichomuumiza Kane ni kwamba ujumbe huo wa Twitter ulitumwa upya na watu wasiopungua 40,000 na kila mmoja akiweka komenti anavyojua yeye.