Serena Williams apewa Zarina Indian Open

Wednesday March 7 2018

 

New York, Marekani. Mchezaji tenisi nguli wa Marekani Serena Williams, anarajiwa kurejea uwanjani kwa mara ya kwanza kucheza dhidi ya Zarina Diyas.

Serena atacheza mchezo wa kwanza kwa mchezaji mmoja tangu aliposhiriki mashindano ya Australian Open mwaka jana.

Nguli huyo anatarajiwa kumenyana na Zarina katika mashindano ya Indian Wells kesho. Bingwa huyo mara 23, alikuwa nje ya tenisi baada ya kujifungua mtoto wa kike Olympia Septemba, mwaka jana.

Hata hivyo, nyota huyo alirejea kwa mara ya kwanza katika mchezo uliohusisha wachezaji wawili akicheza na dada yake Venus Februari 11.

Kurejea uwanjani Serena, kutaongeza chachu ya ushindani katika mchezo wa tenisi kutokana na uzoefu wake kwenye mashindano mbalimbali duniani.

Pia Victoria Azarenka, ambaye amekuwa nje ya uwanja tangu aliposhiriki mashindano ya Wimbledon mwaka 2017, anatarajiwa kurejea uwanjani kuvaana na Heather Watson.