Sarri atumia saa 13 kila siku kusoma wapinzani

Muktasari:

Chelsea itacheza mechi saba katika kipindi cha siku 23, mechi hizo itakuwapo dhidi ya mahasimu wao West Ham, watakipiga na Liverpool mara mbili na watakuwa na kipute cha ugenini Ugiriki kwenye Europa League.

KOCHA wa Chelsea, Maurizio Sarri amefichua kwamba amekuwa akitumia saa 13 kwa siku kutazama video za wapinzani wake kwenye Ligi Kuu England.

Kocha huyo Mtaliano alijipa kazi hiyo na kuifanya wakati ligi iliposimama kupisha mechi za kirafiki za kimataifa na alikuwa bize kwa wiki zote hizo mbili kuwasoma wapinzani wake.

Chelsea itacheza mechi saba katika kipindi cha siku 23, mechi hizo itakuwapo dhidi ya mahasimu wao West Ham, watakipiga na Liverpool mara mbili na watakuwa na kipute cha ugenini Ugiriki kwenye Europa League.

Sarri alisema: “Tunapaswa kucheza mechi saba ndani ya siku 23, hivyo ni lazima nifanye kazi. Nina mechi nyingi sana, Cardiff na PAOK, West Ham na Liverpool.

“Wakati mwingine najiandaa kwenye uwanja wa mazoezi, wakati mwingine nyumbani.”

Sarri, aliyewahi kuwa meneja wa benki, alisema amekuwa akijipa kazi binafsi za kutambua mbinu za wapinzani wake kabla hajawakabili.