Samatta Mkali ndani,mje ya uwanja

HAKUNA anachokipenda nahodha wa Taifa Stars, Mbwana Samatta, kama kucheka na nyavu na tabia hiyo alianza tangu akiwa Mbagala Market ambako alicheza soka la kueleweka kabla ya kutua African Lyon na Simba alikojipatia umaarufu.

Tabia hiyo ya kucheka na nyavu Samatta alienda nayo pia TP Mazembe, klabu ambayo ilimfanya aweze kutwaa tuzo ya Mchezaji Bora wa Afrika kwa wachezaji wa ndani.

“Kama mshambuliaji najivunia kufunga, kutengeneza huwa ni ziada kwangu lakini kazi yangu ya kwanza ni hiyo. Ukame wa kufunga ni kitu kibaya ambacho kinaweza kumuathiri mshambuliaji yeyote,” anasema Samatta.

Unajua kinachoendelea? Unaambiwa ile tabia yake ya kucheka na nyavu tayari imeifanya klabu yake ya KRC Genk ya Ubelgiji kutanguliza mguu mmoja ndani kwenye hatua ya mwisho ya kutinga makundi ya Kombe la Europa Ligi.

Samatta aliiongoza KRC Genk kwenye mchezo wa raundi ya tatu kuwania kuingia makundi ya Europa Ligi dhidi ya Lech Pozna iliyotoka Poland na kufunga bao moja kati ya mawili ambayo walishinda nyumbani, Luminus Arena mjini Genk.

Mbele ya watazamaji 13, 540, Samatta aliihakikishia ushindi KRC Genk wa mabao 2-0 baada ya kufunga bao la pili dakika ya 56 huku bao la kwanza likifungwa na Ruslan Malinovskiy dakika ya 44.

Ushindi huo umeifanya KRC Genk anayoichezea kuwa na nafasi ya kuvuka hatua hiyo licha ya kuwepo kwa mchezo wa marudiano ambao utachezwa Ahamisi kwenye uwanja wa INEA mjini Pozna nchini Poland.

Kama KRC Genk itawaondoa Wapoland hao kwa matokeo ya jumla, watakuwa na kikwazo kimoja tu ili watinge hatua ya makundi ambayo itakuwa na jumla ya timu 48.

Kikwazo hicho ni kucheza dhidi ya timu ambayo watapangiwa nayo kwenye hatua hiyo ya mchujo wa mwisho ambao utakuwa na jumla ya timu 42 ambazo zitacheza kwa mtindo ule ule wa mechi za nyumbani na ugenini na mshindi wa jumla anapata ticketi ya kuingia makundi.

Bao alilofunga Samatta dhidi ya Lech Pozna ni bao la 34 kuifungia KRC Genk katika mashindano yote tangu ajiunge na timu hiyo Januari 29, 2016 akitokea TP Mazembe ya DR Congo.

Akiwa ameichezea klabu hiyo ya Ubelgiji jumla ya mechi 115 za mashindano yote, zikiwamo 87 za Ligi Kuu alikoifungia jumla ya mabao 26, ndani ya msimu wa kwanza wa 2015/16, Samatta alifunga mabao matano na kutengeneza mengine matatu kwenye michezo 18.

Samatta alifunga bao lake la kwanza KRC Genk Februari 28 kwenye mchezo dhidi ya Club Brugge, bao hilo liliamua matokeo ya ushindi kwa Genk ambao walishinda kwa mabao 3-2.

Msimu wa 2016/17, Samatta alicheza jumla ya michezo 59 kufunga mabao 20.

Msimu wake wa tatu wa 2017/18, Samatta alifunga jumla ya mabao manane kwenye michezo 34 huku akitengeneza mengine manne na kwenye msimu wake huu wanne ndiyo ameanza hivyo kwa kupachika bao lililoiweka Genk mguu sawa.

Katika msimu huu ambao Ligi ya Ubelgiji ikianza kushika kasi, Samatta ameshuka uwanjani mara mbili bila kufunga (kabla ya mchezo wao wa jana Jumapili), huku katika mechi za Europa kacheza pia mechi mbili na kufunga bao 1.

Kwa ujumla anatarajia kuwa na msimu wa mafanikio zaidi kutokana na jinsi alivyo na uzoefu wa kutosha sasa wa ligi hiyo ya Ubelgiji.