NYIE VIPI! Ronaldo awashambulia waandishi wa habari

NICOSIA CYPRUS

HALI si shwari sana pale Santiago Bernabeu. Inaonekana upepo bado haujatulia vizuri kama inavyotakiwa. Staa wa timu, Cristiano Ronaldo ameonekana kuwa jazba kwa sasa hasa nyakati hizi anazopitia kipindi kigumu cha maisha yake ya soka.

Ronaldo, juzi aliwashambulia waandishi wa habari mara baada ya kufunga mabao mawili katika ushindi wa mabao 6-0 wa Real Madrid dhidi ya APOEL ya Cyprus, akiwashutumu kubadilisha maneno anayoyasema.

Ronaldo alikatisha katika eneo la waandishi wa habari huku akiwabwatukia kuwa, wanabadilisha maneno yake na kuharibu dhana nzima ya kitu ambacho alikizungumza.

“Sitaongea na nyingi kwa sababu nikifanya hivyo huwa sieleweki. Huwa ninaongea halafu ningi mnafanya kitu ambacho sijasema,” alisema Ronaldo bila ya kusimama katika eneo hilo ambalo wachezaji huzungumza na waandishi wa habari.

Staa huyo wa kimataifa wa Ureno, ambaye ndiye Mwanasoka Bora wa Dunia amewashutumu waandishi kwa kubadili maneno yake aliyosema mara baada ya kumalizika kwa pambano kati yao na Tottenham jijini London wiki chache zilizopita ambapo, walichapwa mabao 3-1.

Ronaldo aliwaambia waandishi wa habari kwamba, kipigo hicho kilichangiwa na kukosekana kwa wachezaji watatu mahiri, Pep, Alvaro Morata na James Rodriguez ambao  walioondoka katika dirisha kubwa lililopita huku klabu hiyo ikishindwa kuingia sokoni kununua wachezaji wenye uzoefu.

“Kama ukiniuliza kiukweli kabisa, basi kila timu ingewakosa wachezaji wenye uzoefu. Ni wazi kwamba Pepe alikuwa mchezaji mahiri, (Alvaro) Morata, James wote walikuwa hodari. Wote hao waliondoka na walipokuwepo walitufanya tuwe imara,” alisema Ronaldo.

Hata hivyo, Gazeti moja la Catalunya liliandika kuwa Ronaldo alikuwa amekosoa sera za uhamisho wa wachezaji Real Madrid hasa ukizingatia kuwa, Madrid walikuwa wamewanunua Theo Hernandez na Dani Ceballos ambao, wote wana umri chini ya miaka 21.

Madai hayo ya Ronaldo inadaiwa yalipokewa vibaya na nahodha wa timu hiyo, Sergio Ramos ambaye mara nyingi amekuwa akikwaruzana na Ronaldo linapokuja suala la misimamo klabuni hapo.

“Sikubaliani naye kwamba eti kikosi ni dhaifu, inaonekana ni mawazo ya kisingizio tu,” alisema Ramos akipinga maoni ya Ronaldo kwamba, kikosi chao msimu huu ni dhaifu kwa sababu ya kuwapoteza mastaa hao watatu.

Fomu ya Ronaldo imekuwa ovyo msimu huu hasa katika La Liga na hadi sasa amefunga bao moja tu huku hasimu wake Lionel Messi akiwa na mabao 12. Ubovu wa kiwango chake umechangia kwa kiasi kikubwa Real Madrid kuachwa mbali kwa pointi 10 na Barcelona katika msimamo wa Ligi.

Hata hivyo, Ronaldo amekuwa fomu katika Ligi ya Mabingwa wa Ulaya na mabao yake mawili aliyofunga juzi dhidi ya APOEL  na kuwa nane hadi sasa.