Ronaldo asaka rekodi mpya

Muktasari:

  • Nahodha huyo wa Ureno leo ameweza kufikisha mabao 84 baada ya kuifungia Ureno bao la kuongoza katika mchezo unaoendelea kupigwa dhidi ya Morocco, ukiwa ni mchezo wa raundi ya pili wa fainali za Kombe la Dunia 2018.

Moscow, Russia. Kinara wa mabao katika mechi mbali mbali za timu za Taifa ni mshambuliaji nguli wa Iran, Ali Daei, aliyefunga mabao 109, lakini sasa anafukuziwa kwa kasi na Cristiano Ronaldo wa Ureno.

Nahodha huyo wa Ureno leo ameweza kufikisha mabao 84 baada ya kuifungia Ureno bao la kuongoza katika mchezo unaoendelea kupigwa dhidi ya Morocco, ukiwa ni mchezo wa raundi ya pili wa fainali za Kombe la Dunia 2018.

Renaldo ameifikia nafasi iliyokua ikishikiliwa na mchezaji wa zamani wa Hungury, Ferenc Puskas aliyestaafu akiwa ameifungia nchi yake mabao 84.

Aidha Ronaldo anaonekana kuanza kuitafuta kwa kasi rekodi ya inayoshikiliwa na Mjerumani Miroslav Klose ya ufungaji bora wa muda wote wa fainali za Kombe la Dunia.

Wakati Klose alifunga mabao 16 katika fainali nne alizoitumikia Ujerumani, Ronaldo kwa upande wake amefikisha mabao saba katika fainali nne za Kombe la Dunia.

Kabla ya fainali za mwaka huu alikua amefunga mabao matatu, alifunga bao moja katika kila fainali kuanzia zile za mwaka 2006, 2010 na 2014.

Ronaldo alizianza fainali za mwaka huu kwa kishindo alifunga mabao matatu ‘hat trick’ Ureno ilipolazimisha sare ya mabao  3-3 na Hispania na leo tayari amefunga bao moja kabla ya mapumziko hivyo kufikisha jumla ya mabao saba.

Akiiwezesha Ureno kutinga hatua ya pili ya michuano hiyo atakua anajiwekea nafasi kubwa zaidi ya kuifikia au kuivunja rekodi ya Klose.