Ronaldo ampa Neymar mzuka wa kuhamia Italia

Muktasari:

Neymar alisema ndoto zake za utotoni zilikuwa kwenda kucheza kwenye soka la Italia siku moja na sasa baada ya Ronaldo kujiunga na Juventus jambo hilo limempa hamasa kubwa ya kuhamia kwenye Serie A.

KITENDO cha supastaa Cristiano Ronaldo kuhamia kwenye Serie A kinaweza kubadili upepo na kumshawishi staa wa Kibrazili, Neymar na kuchukua uamuzi wa kwenda kujiunga na moja ya klabu kubwa kwenye soka la Italia.

Neymar alisema ndoto zake za utotoni zilikuwa kwenda kucheza kwenye soka la Italia siku moja na sasa baada ya Ronaldo kujiunga na Juventus jambo hilo limempa hamasa kubwa ya kuhamia kwenye Serie A.

Ronaldo alihitimisha miaka yake tisa huko Real Madrid kwa kuamua kwenda kujiunga na Juventus, jambo ambalo linadaiwa litawafanya kuwapo na mvuto mkubwa wa soka la Italia kupanda upya na kuvutia wakali wengine wa maana.

Kwenye kosi cha Real Madrid, Ronaldo alifunga mabao 450 katika mechi 438 alizocheza huku akiweka rekodi zake matata kabisa kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya kubeba taji hilo mara nne.

Staa wa Paris-Saint Germain, Neymar - ambaye alichuana na Ronaldo mara nyingi tu kwenye El Clasico kipindi hicho alipokuwa kwenye kikosi cha Barcelona amesema staa huyo wa Ureno anakwenda kulibadili soka la Italia.

Ronaldo na Neymar walimenyana msimu uliopita kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya.

“Nadhani Cristiano Ronaldo atalibadili soka la Italia,” alisema Neymar wakati ambao alizima ripoti za mpango wa kuhamia Real Madrid .

“Litakuwa tena lile soka la Italia ambalo nilikuwa nalitazama nilipokuwa mdogo kwa sababu Cristiano Ronaldo ni mchezaji mkubwa. Nimefurahishwa na uamuzi wake. Nadhani ni uamuzi mgumu sana kuufanya, hivyo namtakia kila la heri, lakini si kwenye mechi dhidi ya PSG.”