Ronaldo akisema naondoka uwezi kumzuia, Sir Ferguson atajwa kufanikisha kumpeleka Manchester United

Muktasari:

Calderon ndiye aliyemnunua Ronaldo mwaka 2009, kwa pauni 80milioni na amekiri kuwa nyota huyo wa Ureno bado anamapenzi na Man United.

Madrid, Hispania. Rais wa zamani wa Real Madrid, Ramon Calderon amesema Cristiano Ronaldo anamapenzi makubwa na Manchester United, na Sir Alex Ferguson atakuwa na  mchango mkubwa wa kufanikisha uhamisho wake.

Calderon ndiye aliyemnunua Ronaldo mwaka 2009, kwa pauni 80milioni na amekiri kuwa nyota huyo wa Ureno bado anamapenzi na Man United. 

Katika mahojiano yake na SunSport, Calderon alisema: “Nakumbuka wakati namsajili  Cristiano, alinipigia simu na kuniambia kila mtu  wa Manchester United wamekuwa na mapenzi  naye makubwa.

“Sir Alex Ferguson ni kama baba yake na  anawapenda mashabiki wa klabu hiyo.

“Klabu hiyo imekuwa ni muhimu katika maisha  yake ya soka. Manchester United ni klabu ya moyo wake.”

Ron na Fergie bado ni marafiki wa karibu na mwezi uliopita katika fainali ya Ligi ya Mabingwa

mjini Cardiff, alipiga picha ya pamoja na Fergie baada ya kupokea tuzo ya mchezaji bora wa mechi.

Ronaldo anataka kuondoka Madrid kwa sababu anaamini wameshindwa kumsaidia katika kesi yake ya kukwepa kodi pauni 13 milioni anayodaiwa Hispania.

Alisema ameamua kuondoka Bernabeu baada ya miaka nane ya mafanikio katika klabu hiyo.

Calderon aliongeza: “Alikuwa na mazingira kama hayo Manchester United wakati alipoamua kuondoka na kumsajili.

“Anaposema anataka kuondoka anamaanisha, kama rais uwezi kufanya lolote zaidi ya kumwachia aondoke kwa kuangalia uwezekano wa kupata fedha zaidi.”

Ronaldo alisaini mkataba mpya Novemba mwaka jana akiwa anapokea mshahara wa pauni 365,000 kwa wiki, lakini Man United wanaweza kulipa.